Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Thursday, November 6, 2014

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARISHIRIKA LA MADINI LA TAIFA

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Balozi Alexander A. Muganda, Mwenyekiti mpya Bodi ya Wakurugenzi ya STAMICO
Rais Jakaya Mrisho Kikwete amemteua Balozi Alexander A. Muganda kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Taifa la Madini (STAMICO) akichukua nafasi iliyoachwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi Bw. Rumisha H. Kimambo aliyestaafu kwa hiari.
Rais Kikwete amefanya uteuzi huo kwa mujibu wa mamlaka aliyonayo chini ya kifungu cha 6 namba (2) (b) cha Tamko la Rais namba 163 la Sheria ya Mashirika ya Umma ya mwaka 1969 iliyotolewa tarehe 18 Agosti 1972. Sheria hiyo inamwezesha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kumteua Mwenyekiti wa Bodi wa Mashirika ya Umma.Uteuzi huo wa Balozi Muganda unaanzia mwezi Juni, 2014 alipostaafu Bw. Kimambo hadi Aprili, 2015 muda wa Bodi hiyo utakapoisha.
Uteuzi wa Balozi Muganda unatokana na utendaji wake mzuri wa kazi na imani kubwa aliyonayo Mheshimiwa Rais.
Kabla ya uteuzi huo, Balozi Muganda alikuwa Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya STAMICO kuanzia Mei, 2013 hadi alipopata uteuzi huo.
Balozi Muganda ameshika nyadhifa mbalimbali katika utumishi Serikalini kwa miaka 35 iliyopita, mpaka hapo alipostaafu rasmi katika utumishi wa umma mwezi Novemba mwaka 2006.
Nyadhifa alizowahi kushika Balozi Muganda ni pamoja na Mwanasheria wa Serikali, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu (1971 – 1976); Mkurugenzi Msaidizi wa Kikosi cha Kupambana na Rushwa (1976-1979); Naibu Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia Rushwa (1980 – 1997); na Balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe na Rwanda (1997-2006).
Balozi Muganda amebobea katika fani ya Sheria kwa miaka 39 sasa, ambapo mwaka 2007 alijikita zaidi katika kazi za sheria kupitia sekta binafsi baada ya kustaafu rasmi kazi Serikalini.
 Akizungumza kufuatia uteuzi huo, Mwenyekiti huyo mpya wa Bodi ya Wakurugenzi ya STAMICO Balozi Muganda amemshukuru Mheshimiwa Rais Kikwete kwa uteuzi huo na imani aliyokuwanayo kwake na ameahidi kutekeleza majukumu yake kwa ueledi na uaminifu kwa kadri awezavyo, ili kuiwezesha STAMICO kutimiza majukumu yake na kuleta tija kwa Taifa.
“Nitaendelea kuwa msikivu kwa maelekezo na ushauri wa Rais na wa Wizara ya Nishati na Madini katika kutimiza wajibu wangu wa kuiongoza bodi hii ili iweze kusimamia ipasavyo uendeshaji wa Shirika, Shirika ambalo ni tumaini kubwa kwa taifa katika uchangiaji wa ukuaji uchumi na kuondokana na umaskini.” Alifafanua Balozi Muganda.
Amesema kwa kuwa Serikali ni mmiliki mkuu wa hisa za STAMICO, hivyo kupitia wadhifa huo mkuu atajitahidi kuhakikisha kuwa Shirika hilo linatoa gawio Serikalini ili kuchangia katika mfuko wa Serikali na kuleta maendeleo ya Taifa.
“ingawa STAMICO iko  katika hatua ya ukuaji katika uzalishaji wa madini, Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika chini ya usimamizi wangu, itahakikisha inaboresha mbinu za usimamizi wa STAMICO na utekelezaji wa majukumu yake  ili kuliwezesha Shirika kufikia dira, mwelekeo na malengo ya uanzishwaji wake” aliongeza Balozi Muganda.
Amesema katika kipindi  chake cha uongozi wa Bodi ya STAMICO, atajitahidi kuhakikisha kuwa Shirika pia linachangia katika kuongeza nafasi za ajira katika sekta ya madini na  linajenga uwezo wa kiteknolojia na kifedha kwa wachimbaji wadogo ili waweze kuchangia  katika kukuza uchumi wa taifa.” Alibainisha Balozi Muganda.
Balozi Muganda amesema Serikali imempa dhamana kubwa Mtendaji Mkuu wa STAMICO katika kuliongoza Shirika hilo, hivyo ni matumaini ya Watanzania kuona kuwa Shirika hilo na wafanyakazi wake wanajituma kwa uadilifu, uaminifu na mshikamano katika kutekeleza malengo ya Shirika na hivyo kutoa matokeo ya kazi yanayopimika, kwa wakati muafaka.
Amewataka wafanyakazi wa STAMICO na wa Kampuni yake Tanzu ya STAMIGOLD,  kushiriki katika kukabiliana na changamoto inayoikabili STAMICO ya kukuza pato la Taifa, kwa kujituma kufanyakazi kwa bidii, kujiepusha na vitendo vya wizi na kutokomeza ubadhirifu wa mali ya umma, ili kuliwezesha Shirika hilo kuongeza mapato na kukuza pato la Taifa.
Shirika la Madini la Taifa lilianzishwa rasmi mwaka 1972 chini ya Sheria ya Mashirika ya umma ya mwaka 1969 kwa lengo la Kusimamia hisa za Serikali kwenye migodi mikubwa nchini; kuwekeza katika sekta ya madini kupitia utafiti, uchimbaji, biashara na uendelezaji wa madini; kutoa huduma za uchorongaji, utafiti na ushauri wa kitaalamu kwenye sekta ya madini na kuratibu shughuli za uendelezaji wachimbaji wadogo ili kuwajengea uwezo katika uzalishaji wa madini na kuboresha masoko.
Imetolewa na
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji,
Shirika la Madini la Taifa,
Plot No 417/418,
UN Road,
S.L.P 4958,
Dar es Salaam,
Tanzania.
Barua Pepe: Info@stamico.co.tz
Simu: +255-22-2150029

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...