Mbunge
wa Kitope Balozi Seif ali Iddi akizungumza na wanamichezo mara baada ya
kumalizika kwa fainali ya mashindano ya Zaweda Cup, yaliyofanyika
kwenye uwanja wa michezo wa Kitope Wilaya ya Kaskazini “ B”. Katikati ni Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kaskazini “ B “ Ndugu Hilika Khamis Fadhil.
Balozi
Seif akikabidhi zawadi za mipira na jezi kwa timu shiriki za mashindano
ya Zaweda Cup yaliyofanyika ndani ya Jimbo lake la Kitope.
Balozi
Seif akikabidhi zawadi za mipira na jezi kwa timu shiriki za mashindano
ya Zaweda Cup yaliyofanyika ndani ya Jimbo lake la Kitope.
Timu
ya Soka ya African Boys ya Kijiji cha Kitope imetawazwa ubingwa wa
mashindao ya Kombe la Zaweda baada ya kuitandika timu ya New Star ya
Kiwengwa kwa Magoli 4 -3 katika pambano la fainal ya mashindano hayo
yaliyoshirikisha Timu 12 za Soka za Jimbo la Kitope.
Pambano
hilo la fainal lililoshuhudiwa na mamia ya wapenzi wa soka wa Wilaya ya
Kaskazini “B“ lilifanyika katika uwanja wa michezo wa Santiago Benabao
uliopo Kitope ambapo mgeni rasmi alikuwa Mbunge wa Jimbo la Kitope
Balozi Seif Ali Iddi.
African
Boys ya Kitope ilibeba kombe hilo la Zaweda baada ya kutoka suluhu ya
bila kwa bila na wapinzani wake New Star ya kiwengwa kwenye dakika 90 za
mchezo huo na kulazimika kupigiana Penalti zilizoibua mshindi wa
pambano hilo.
Huu
ni mwaka wa tatu kwa jumuiya isiyo ya kiserikali inayojishughulisha na
utoaji wa taaluma ya mapambano dhidi ya dawa za kulevya na virusi vya
ukimwi kwa vijana { ZAWEDA } kuandaa mashindano hayo yanayoshirikisha
pia timu rafiki zilizo nje ya Jimbo la Kitope.
Mgeni
rasmi wa Fainali hiyo Mbunge wa Jimbo la Kitope ambae pia ni Makamu wa
Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alikabidhi zawadi kwa
mshindi wa kwanza African Boys ya Kitope ambayo ilipata fedha taslim
shilingi Laki 500,000/-, Seti ya Jezi, Kikombe, Mipira pamoja na Seti ya
Tv na Dikoda yake iliyotolewa na Mke wa Mbunge wa Jimbo hilo Mama Asha
Suleiman Iddi.
Mshindi
wa Pili New Star ya Kiwengwa ikazawadiwa shilingi Laki 300,000/-
taslim, Jezi, Kikombe pamoja na Mipira wakati mshindi wa tatu Timu
iliyoalikwa ya soka ya Mahonda Kids akajinyakulia shilingi Laki
200,000/- Taslim, jezi pamoja na mpira.
Balozi
Seif pia akakabidhi zawadi ya mipira kwa timu zote 12 zilizoshiriki
mashindano hayo ya mchezo wa soka za Jimbo la Kitope zikiwemo pia mbili
za kualikwa nje ya Jimbo hilo za Mahonda Kids na Kilimani City.
Mapema
Balozi Seif alikabidhi zawadi ya fedha taslim kwa washindi wa
mashindano ya mchezo wa pete { netball } ulioshirikisha timu sita za
jimbo la kitope yaliyokwenda sambamba na mchezo huo wa soka wa jimbo
hilo.
Mshindi
wa kwanza ni timu ya wanawake ya Biasha Kitope, mshindi wa Pili alikuwa
timu mualikwa wa mashindano hayo Mahonda na wa Tatu alikuwa Timu ya
Mabanati wa Kitope “ B “.
Zawadi
nyengine zikawashukia Timu yenye nidhamu kwa mchezo wa pete
ilichaguliwa Fujoni, mfungaji bora alifanikiwa kupata Dawa Vuai wakati
uchezaji bora ukamshukia mwanadada Leila Ismail.
Kwa
upande wa mchezo wa Soka Timu bora na yenye nidhamu ya Mashindano hayo
ilifanikiwa kuwa Zaweda iliyoandaa mashindano hayo wakati mfungaji bora
alinyakua Said Abdulla.
Akizungumza
na wana michezo hao wa mashindano ya Zaweda Cup Mbunge wa Jimbo la
Kitope Balozi Seif alielezea furaha yake kutokana na zoezi zima la
mashindano hayo lililoonyesha nidhamu ya hali ya juu na kutoa burdani
kwa wapenzi wa michezo ndani ya Wilaya ya Kaskazini “ B”.
Balozi
Seif aliwataka wanamichezo hao kuhakikisha kwamba nidhamu
waliyoionyesha kwenye mashindano hayo wanaichukulia kuwa kigezo cha
kuiendeleza katika michezo mengine itakayowakabili hapo baadaye.
Alisisitiza
kwamba wakati umefika kwa wachezaji hao kuongeza juhudi na maarifa
kutokana na kiwango walichofikia ili wajijengee mazingira mazuri ya
kufuzu kucheza kwenye vilabu vikubwa jambo ambalo litawapa fursa nzuri
ya ajira kupitia fani hiyo ya michezo.
Timu
zilizoshiriki mashindano hayo kwa upande wa soka zilikuwa ni Kitope
United wenyeji wa mashindano hayo, African Coast ya Upenja,African Boys
ya Kazole, Matetema ya Kazole, New Star ya Kiwengwa, Kichungwani, Lindi
Boys, Mbuyuni Star, Kombora,Zaweda ambao ndio wasimamizi wa ligi hiyo
pamoja na timu mbili zilizoalikwa ambazo ni Mahonda Kids na Kilimani
City.
Kwa
upande wa mpira wa pete { Netball } wanawake timu sita ziliwania kombe
la Zaweda ambazo ni pamoja na Asha Queen iliyotawadhwa ubingwa wa kombe
hilo,Kitope a, Kitope B, Fujoni, Upenja pamoja na Timu mbili alikwa za
Mahonda na Kizimbani.
Mabingwa
wapya wa kombe la Zaweda African Boys ya Kitope wakishangiria ushindi
wao dhidi ya New Star ya Kiwengwa kwa mikwaju ya Penalti 4-3 baada ya
kumaliza muda wa dakika 90 bila kufungana.