Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Monday, June 30, 2014

BALOZI IDDI AKABIDHI ZAWADI YA MIPIRA NA JEZI KWA WASHINDI WA MICHUANO YA KOMBE LA ZAWEDA


 Mbunge wa Kitope Balozi Seif ali Iddi akizungumza na wanamichezo mara baada ya kumalizika kwa fainali ya mashindano ya Zaweda Cup, yaliyofanyika kwenye uwanja wa michezo wa Kitope Wilaya ya Kaskazini “ B”. Katikati ni Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kaskazini “ B “ Ndugu Hilika Khamis Fadhil.
 Balozi Seif akikabidhi zawadi za mipira na jezi kwa timu shiriki za mashindano ya Zaweda Cup yaliyofanyika ndani ya Jimbo lake la  Kitope.
 Balozi Seif akikabidhi zawadi za mipira na jezi kwa timu shiriki za mashindano ya Zaweda Cup yaliyofanyika ndani ya Jimbo lake la  Kitope.
 Timu ya Soka ya African Boys ya Kijiji cha Kitope imetawazwa ubingwa wa mashindao ya Kombe la Zaweda baada ya kuitandika timu ya New Star ya Kiwengwa  kwa Magoli 4 -3 katika pambano la fainal ya mashindano hayo yaliyoshirikisha Timu 12 za Soka za Jimbo la Kitope.
Pambano hilo la fainal lililoshuhudiwa na mamia ya wapenzi wa soka wa Wilaya ya Kaskazini  “B“ lilifanyika katika uwanja wa michezo wa Santiago Benabao uliopo Kitope ambapo mgeni rasmi alikuwa Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif Ali Iddi.
African Boys ya Kitope ilibeba kombe hilo la Zaweda baada ya kutoka suluhu ya bila kwa bila na wapinzani wake New Star ya kiwengwa kwenye dakika 90 za mchezo huo na kulazimika kupigiana Penalti zilizoibua mshindi wa pambano hilo.
Huu ni mwaka wa tatu kwa jumuiya isiyo ya kiserikali inayojishughulisha na utoaji wa taaluma ya mapambano dhidi ya dawa za kulevya na virusi vya ukimwi kwa vijana { ZAWEDA } kuandaa mashindano hayo yanayoshirikisha pia timu rafiki zilizo nje ya Jimbo la Kitope.
Mgeni rasmi wa Fainali hiyo Mbunge wa Jimbo la Kitope ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alikabidhi zawadi kwa mshindi wa kwanza African Boys ya Kitope ambayo ilipata fedha taslim shilingi Laki 500,000/-, Seti ya Jezi, Kikombe, Mipira pamoja na Seti ya Tv na Dikoda yake iliyotolewa na Mke wa Mbunge wa Jimbo hilo Mama Asha Suleiman Iddi.
Mshindi wa Pili  New Star ya Kiwengwa ikazawadiwa shilingi Laki 300,000/- taslim, Jezi, Kikombe pamoja na Mipira wakati mshindi wa tatu Timu iliyoalikwa ya soka ya Mahonda Kids akajinyakulia shilingi Laki 200,000/- Taslim, jezi pamoja na mpira.
Balozi Seif pia akakabidhi zawadi  ya mipira kwa timu zote 12 zilizoshiriki mashindano hayo ya mchezo wa soka za Jimbo la Kitope zikiwemo pia mbili za kualikwa nje ya Jimbo hilo za Mahonda Kids na Kilimani City.
Mapema Balozi Seif alikabidhi zawadi ya fedha taslim kwa washindi wa mashindano ya mchezo wa pete { netball } ulioshirikisha timu sita za jimbo la kitope yaliyokwenda sambamba na mchezo huo wa soka wa jimbo hilo.
Mshindi wa kwanza ni timu ya wanawake ya Biasha Kitope, mshindi wa Pili alikuwa timu mualikwa wa mashindano hayo Mahonda na wa Tatu alikuwa Timu ya Mabanati wa Kitope “ B “.
Zawadi nyengine zikawashukia Timu yenye nidhamu kwa mchezo wa pete ilichaguliwa Fujoni, mfungaji bora alifanikiwa kupata Dawa Vuai wakati uchezaji bora ukamshukia mwanadada  Leila Ismail.
Kwa upande wa mchezo wa Soka Timu bora na yenye nidhamu ya Mashindano hayo ilifanikiwa kuwa Zaweda  iliyoandaa mashindano hayo wakati mfungaji bora alinyakua Said Abdulla.
Akizungumza na wana michezo hao wa mashindano ya Zaweda Cup Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif alielezea furaha yake kutokana na zoezi zima la mashindano hayo lililoonyesha nidhamu ya hali ya juu na kutoa burdani kwa wapenzi wa michezo ndani ya Wilaya ya Kaskazini “ B”.
Balozi Seif aliwataka wanamichezo hao kuhakikisha kwamba nidhamu waliyoionyesha kwenye mashindano hayo wanaichukulia kuwa kigezo cha kuiendeleza katika michezo mengine itakayowakabili hapo baadaye.
Alisisitiza kwamba wakati umefika kwa wachezaji hao kuongeza juhudi na maarifa kutokana na kiwango walichofikia ili wajijengee mazingira mazuri ya kufuzu kucheza kwenye vilabu vikubwa jambo ambalo litawapa fursa nzuri ya ajira kupitia fani hiyo ya michezo.
Timu zilizoshiriki mashindano hayo kwa upande wa soka zilikuwa  ni  Kitope United wenyeji wa mashindano hayo, African Coast ya Upenja,African Boys ya Kazole, Matetema ya Kazole, New Star ya Kiwengwa, Kichungwani, Lindi Boys, Mbuyuni Star, Kombora,Zaweda ambao ndio wasimamizi wa ligi hiyo pamoja na timu mbili zilizoalikwa ambazo ni Mahonda Kids na Kilimani City.
Kwa upande wa mpira wa pete { Netball } wanawake timu sita ziliwania kombe la Zaweda ambazo ni pamoja na Asha Queen iliyotawadhwa ubingwa wa kombe hilo,Kitope a, Kitope B, Fujoni, Upenja pamoja na Timu mbili alikwa za Mahonda na Kizimbani.
Mabingwa wapya wa kombe la Zaweda African Boys ya Kitope wakishangiria ushindi wao dhidi ya New Star ya Kiwengwa kwa mikwaju ya Penalti 4-3 baada ya kumaliza muda wa dakika 90 bila kufungana.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...