Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Saturday, December 14, 2013

Mama Kikwete: Watanzania tumieni Maktaba kwa kujisomea



Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akikata utepe ikiwa ni ishara ya uzinduzi rasmi wa maktaba ya Shule ya Msingi ya Mzimuni iliyoko Magomeni. Kushoto kwa Mama Salma ni Mheshimiwa Balozi Young-Shim Dho, Mwanzilishi wa Step Foundation na Balozi wa Mradi wa Utalii endelevu kwa ajili ya kuondoa umasikini wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii Duniani ambaye ndiye aliyefadhili maktaba hiyo.PICHA/JOHN LUKUWI

 ^^^^^^^^^^^^^^
Na Anna Nkinda – Maelezo

Watanzania wametakiwa kutumia maktaba zilizopo kusoma vitabu na machapisho yaliyopo ili waweze kujiongezea elimu na ufahamu zaidi wa masuala mbalimbali yahusuyo maisha na elimu kwa upana wake.

Wito huo umetolewa jana na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati akifungua maktaba ya watoto iliyojengwa na Serikali ya Korea Kusini  kupitia Taasisi ya Step katika shule ya msingi Mzimuni iliyopo wilaya ya Kinondoni jijinii Dar es Salaam.

Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alisema elimu ni ufunguo wa maisha na kwa njia hiyo Taifa linaweza kupambana na kushinda vita dhidi ya maadui wakubwa watatu ambao ni ujinga, umaskini na maradhi na matokeo ya ushindani huo ni kupatikana kwa maendeleo.

“Pamoja na mafunzo tunayoyapata shuleni, vyuoni na sehemu za kazi bado tunapaswa kuendelea kusoma zaidi ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kupambana na adui ujinga, maradhi na umaskini”, alisema Mama Kikwete.

Mwenyekiti huyo wa Wama pia aliwataka walimu wa shule hiyo kutunza maktaba hiyo ili iweze kukidhi malengo ya kuanzishwa kwake kwa kuandaa taratibu bora za kusimamia matumizi na kuzuia upotevu na uharibifi wa vitabu na vifaa vingine.

Kuhusu suala la utandawazi Mama Kikwete  alisema ni muhimu jamii  ikatunza  na kuimarisha utamaduni ili hali wamo katika utandawazi kwani hivi sasa Dunia imekuwa kama kiganja cha mkono kutokana na kukua kwa Sayansi ya Teknolojia ila hayo yote yanawezekana ikiwa watasoma zaidi eneo husika kulingana na mabadiliko yaliyopo.

Mama Kikwete alisema, “Leo hii tumepata maendeleo kwa ajili ya Sayansi na Teknolojia kwani ukitaka kujua chochote kinachoendelea Duniani ni rahisi kwa kuwa unaingia katika mitandao na kuona, hili ni jambo zuri lakini liendane na mila na utamaduni wetu siyo kila jambo unalichukua, chukua yale mazuri ambayo yatakusaidia na yale mabaya ambayo hayana maslahi kwa taifa  yaache”.
Kwa upande wake  Balozi Young –Shim Dho ambaye ni Mwanzilishi wa Taasisi ya Step na Balozi wa mradi wa Utalii endelevu kwa ajili ya kuondoa umaskini wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii Duniani alimshukuru Mama Kikwete kwa kuifungua maktaba hiyo na kuwataka wanafunzi kuitumia kwa kujisomea.

Balozi Young –Shim Dho alisema miaka michache iliyopita nchi ya Korea Kusini ilikuwa ni moja ya nchi  maskini Duniani lakini kupitia tabia ya kupenda kusoma vitabu wamefanikiwa kuwa miongoni mwa nchi zilizomo ndani ya G20 na kuwataka watanzania kutumia vitabu hivyo kusoma.

“Kujengwa kwa maktaba hii na zingine 23 na kupatikana kwa vitabu pamoja na vifaa vingine vya maktaba ni jitihada za Mama Kikwete  ambaye alizunguka huku na kule kuomba msaada ambao leo hii umefanikiwa na kuweza kuwasaidia watanzania wengi”, alisema Balozi Young –Shim Dho.

Ndani ya eneo la  shule ya Msingi Mzimuni kuna shule ya Msingi Mikumi ambapo Mama Kikwete alimuomba balozi Young –Shim Dho kujenga maktaba kama hiyo kwa ajili ya shule hiyo na  Balozi huyo alikubali na kusema kuwa ifikapo mwakani maktaba hiyo itakuwa imekamilika.

Hii ni maktaba ya 24 kujengwa hapa nchini kwa ajili ya watoto wa shule za msingi moja kati ya hizo ni maktaba ya watu wazima iliyopo ndani ya Jengo la Makumbusho jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...