Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Sunday, December 15, 2013

MAWAZIRI WAHENYA NA MAFAILI KUHOJIWA NA KAMATI KUU YA CCM MJINI DODOMANA BASHIR NKOROMO

Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), katika kikao chake kilichofanyika jana mjini Dodoma chini ya Mwenyekiti wake Rais Jakaya Kikwete imeibuka na masuala mazito kadhaa, ambayo leo, Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi Nape Nnauye (pichani) ameyaeleza wakati akizungumza na waandishi wa Habari, Katika Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Lumumba jijini Dar es Salaam.
Moja ya mambo ambayo Nape amezungumzia, ni kuhusu Kamati Kuu hiyo kuwahoji Mawaziri saba, kujibu kero au mambo kadhaa ambayo yaliibuliwa wakati wa ziara ya Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana iliyomalizika hivi karibuni katika mikoa ya Mtwara, Ruvuma, Mbeya na Njombe.
Nape  alisema, Kamati Kuu iliwahoji mmoja baada ya mwingine, kuanzia saa tano asubuhi hadi jioni, baada ya kila mmoja kufika akiwa ameandaa majibu ya tuhuma au hoja alizokuwa ametakiwa kujibu mbele ya Kamati Kuu hiyo.
"Kwa kuwa mawaziri hao tulikuwa tumeshawapelekea hoja zinazowahusu ambazo tulizipisha kwa kiranja wao Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, wengi wao walifika wakiwa na mafaili yenye majibu, ambapo waliingia na kujieleza mmoja baada ya mwingine, na baada ya maelezo ya kila mmoja wajumbe walitoa mapendekezo kwa Mwenyekiti, Rais Jakaya Kikwete", alisema Nape.
Hata hivyo Nape alisema, si vema kueleza kwenye vyombo vya habari kuhusu mapendekezo ambayo Kamati Kuu ilimshauri Mwenyekiti kuchukua, akisema kufanya hivyo itakuwa sawa na kumshinikiza kiongozi huyo kutekeleza mapendekezo yao kwa lazima na hivyo kuharibu maana nzima ya ushauri.
"Sisi tulichofanya ni kumpa mapendekezo, naye kwa mujibu na namna atakavyoona inafaa, atachukua hatua, ambavyo si lazima kumfukuza Waziri Kama wengi wanavyotaka iwe, bali anaweza kuchukua hatua yoyote ili mradi yeye mwenyewe kwa mamlaka aliyo nayo ataona ina manufaa yatakayotoa majibu ya kero zilizosaababisha kila mmoja wa mawaziri hao kuitwa mbele ya Kamati Kuu", alisema Nape.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...