Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Wednesday, February 19, 2014

UWF yahimiza wanawake kushiriki Siku ya Wanawake Dunia Mar.15



  MENEJA wa Tuzo ya Mwanamakuka ambaye pia ni Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Marafiki (UWF) Mariam Shamo akifafanua jambo mbele ya washindi wa tuzo hiyo wa mwaka juzi na jana pamoja na wanahabari kuhusiana na hafla yao wanayoitarajia kuifanya siku ya Wanawake Duniani mnamo Machi 15 mwaka huu,ambayo imepangwa kufanyika ndani ya kiota kipya cha maraha na burudani Escape One Mikocheni jijini Dar, pembeni yake ni  Mdau mkubwa wa tuzo hizo na Mkurugenzi wa Benki ya Wanawake Tanzania Margareth Chacha.

Mjumbe wa Mradi wa Mwanamakuka (Mwanamakuka Awards) na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Wanawake Tanzania,Bi. Margareth Chacha akisisitiza jambo mbele ya washindi wa Mwanamakuka mwaka 2012 na 2013 alipokuwa akiongelea siku ya wanawake Duniani tarehe 15 mwezi ujao mbele ya waandishi wa habari jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki. Kushoto ni Meneja wa Mradi wa Mwanamakuka ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kituo cha Wanawake Marafiki (Unit of Women Friends),Bi Maryam Shamo.
WASHINDI wa Tuzo ya Mwanamakuka mwaka 2012 na 2013 wakiwa pamoja wakati walipokutana na waratibu wa shindano hilo kwa ajili ya kujipanga na Siku ya Wanawake Duniani inayotarajiwa kufanyika mnamo Machi 15 mwaka huu.
WANAWAKE nchini wamehamasishwa kushiriki Siku ya Wanawake Duniani itakayofanyika Machi 15, mwaka huu jijini Dar es Salaam na kujadili masuala mbalimbali ya kumwezesha mwanamke.
Mjumbe wa mradi wa Mwanamakuka (Mwanamakuka Award) na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Wanawake Tanzania, Margareth Chacha, aliwaambia waandishi wa habari mwishoni mwa wiki kuwa siku hiyo ni ya muhimu kwa wanawake kwa vile itawaleta pamoja na kujadili masuala mbalimbali.
“Tutakutana Siku ya Wanawake Duniani na kujadili namna bora zaidi ya kumuwezesha mwanamke kujiinua kiuchumi,” alisema.
Alisema benki yake inafadhili washindi wanawake wajasiriamali kupitia mradi huo na inafanya hivyo kwa ajili ya kumwinua mwanawake kupitia benki yao ya wanawake.
Alisema benki hiyo inataka kuona wanawake wengi wanaingia katika shughuli za kijasiriamali na pia imejipanga kutumia matawi yake nchini kupanua wigo wa zawadi ya Mwanamakuka.
Alisema mpaka sasa ni asilimia mbili tu ya wanawake wanaotumia huduma za kibenki kati ya asilimia nane ya Watanzania wote wanaotumia huduma hizo, na sasa wakati umefika kuongeza idadi ya wanawake.
“Hali hiyo ni ya kihistoria lakini kwa sasa wanawake tunashukuru hali imebadilika tunaweza kufanyakazi mbalimbali zikiwamo za biashara,”aliongeza.
Alisisitiza umuhimu wa wanawake kujiunga katika vikundi kwa ajili ya kupata mikopo kutoka katika benki yao kufanyia shughuli zao za kijasiriamali.
Naye Meneja wa mradi wa Mwanamakuka ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kituo cha Wanawake Marafiki (UWF),  Maryam Shamo, alisema Siku ya Wanawake Duniani kutakuwa na maonyesho ya kazi za kijasiriamali za wanawake na michezo mbalimbali.
“Siku hiyo washindi wa mwaka huu watapatiwa zawadi zao, na pia mshindi wa jumla wa mwaka 2012 na 2013 atapatiwa zawadi kati ya washindi kumi waliokwisha pata zawadi,'' alisema.
Alifafanua kuwa katika kusherehekea ya siku hiyo, watu wengi wamealikwa wakiwamo akinamama wajasiriamali na wanasiasa wanawake.
Kwa upande wake, mjasiriamali mkazi wa Dar es Salaam na mshindi wa nyuma wa mradi huo, Tatu Ngao, alisema alishinda Shilingi  milioni sita ambazo zimemwezesha kufanya biashara yake kwa ufanisi.
“Nilishinda kupitia biashara yangu ya kutengeneza keki...nimepanuka kwa kiwango cha kuridhisha hadi sasa,” alisema.
Zawadi ya Mwanamakuka ni mradi uliobuniwa na Kituo cha Wanawake Marafiki kwa ajili ya kuwawezesha wajasiriamali wanawake kwa ufadhili wa Benki ya Wanawake Tanzania na wadau wengine.

Naye mshindi wa pili wa mwaka jana , Leila Mwambungu alisema anashukuru mradi huo umemfanya apanuke kiakili katika ujasiriamali pamoja na kuweza kuwasaidia wanawake wenzake na kiu yake kubwa kuzidi kusonge mbele ili kuwa mfano kwa wengine.
"Nashukuru waandaji wa tuzo hii, shukrani zangu za pekee ziende kwa Mariam Shamo, Mama Margareth Chacha kwa namna wanavyowasaidia wanawake wenzao, najisikia furaha na fahari kuwa Mwanamakuka namba mbili wa mwaka 2013 na kiu yangu nifike mbali zaidi baada ya kuwezeshwa na mradi huu," alisema Leila. 

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...