Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Monday, June 9, 2014

Vyombo vyaikwamisha Bombastic Modern Taarab


KUNDI jipya la miondoko ya taarab lililokuwa limeanza kuwashika mashabiki, Bombastic Modern, limesitisha shughuli zake kutokana na ukosefu wa vyombo vya muziki.
Bombastic linalomilikiwa na nyota wa zamani wa kundi la Babloom Modern na Dar Modern Taarab, Mridu Ally 'Tx' lilikuwa likijipanga kuingia studio kurekodi nyimbo zake mpya baada ya kufanya maonyesho kadhaa na kuwavutia mashabiki wa muziki huo.
Hata hivyo akizungumza na MICHARAZO, Mridu alisema wamesitisha shughuli ili kujipanga kusaka vyombo vya muziki kwa vile gharama za kukodisha vyombo pamoja na zile za usafiri wamejikuta wakifanya kazi ya bure.
"Tumesitisha shughuli zote za muziki kutokana na tatizo la vyombo, tumekuwa tukikodi na kubeba gharama kubwa ambazo zikichanganyikana na usafiri na malipo kiduchu ya kutoa burudani nahisi wasanii wataona kama wanadhulumu hivyo nimeamua tutulie tujipange kusaka vyombo vyetu wenyewe," alisema.
Mridu alisema mara baada ya kufanikiwa kupata vyombo watarejea kwa kishindo kutoa burudani kwenye kumbi mbalimbali kabla ya kuingia studio kurekodi nyimbo zao mpya ambazo walikuwa wameanza kuzifanyia mazoezi.
Mtunzi, muimbaji na mcharaza gitaa huyo alisema hataki kuja kuona kundi likiyumba na kuwaacha wasanii wake katika hali mbaya ya kifedha ndiyo maana anaona bora watulie na kujipanga upya akidai ushindani kwenye soko la miondoko hiyo linataka mtu kuwa makini na siyo kukurupuka na kutaka kushindana bila kuwa na misingi imara.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...