Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Sunday, February 9, 2014

Yanga jamani mbona utaipenda Afrika



Haruna Niyonzima akiwajibika uwanjani

Wanaume kazini leo uwanja wa Taifa


MABINGWA wa soka nchini, Yanga wameendelea kunyanyasa timu za Comoro baada ya leoi kuwanyuka Komorozine kwa mabao 7-0, huku winga Mrisho Ngassa akiondoka na mpira kwa kufunga hat trick.

Yanga ilipata ushindi huo katika mechi ya mkondo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika katika pambano lililochezwa uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Yanga ilienda mapumziko ikiwa mbele kwa mabao 2-0 yaliyofungwa na Mrisho Ngassa dakika ya 13 na beki Nadir Haroub 'Cannavaro' dakika ya 20.


Ngassa alifunga bao lake kwa kichwa akiunganisha krosi ya Mbuyu Twite, huku bao la Haroub pia likifungwa kwa kichwa kutokana na krosi ya David Luhende.

Kipindi cha pili Yanga walibadilika na kuongeza kasi kwa kuwashambulia wapinzani wao walioonekana wachovu na kupata mabao ya haraka haraka.
Didier Kavumbagu alifunga bao la tatu dakika ya 57 kabla ya Hamisi Kiiza kufunga la nne dakika ya 59.
Ngassa aliongeza mengine mawili na kumfanya afikishe mabao matatu (hat-trick) dakika ya 64 na 68, huku bao la mwisho la Yanga likifungwa tena na Didier Kavumbagu dakika ya 80.
Wacomoro hawakufanya mashambulizi ya nguvu, hivyo kumfanya kipa Juma Kaseja wa Yanga kutokuwa na kazi kubwa.
Matokeo ya mchezo huo yamedhihirisha ubabe wa Yanga kwa timu za Comoro, ambayo haina historia nzuri katika soka kimataifa.
Komorozine inakuwa timu ya tatu kukutana na Yanga kwenye michuano ya Afrika baada ya AJSM na Etoile d'Or Mirontsy.
Januari 27, mwaka 2007 katika Ligi ya Mabingwa Afrika, raundi ya awali Yanga iliifunga AJSM mabao 5-1 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na moja kwa moja kufuzu Raundi ya Kwanza, kwa sababu hakukuwa na mchezo wa marudiano kwa kuwa Comoro hawakuwa na Uwanja wenye kukidhi sifa za michuano ya Afrika.
Mwaka 2009, waliitoa timu nyingine ya Comoro, Etoile de Mironsty kwa jumla ya mabao 14-1, ikianza kushinda 8-1 Januari 31 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kabla ya kwenda kushinda 6-0 ugenini, wakati huo ikiwa chini ya kocha Mserbia, Dusan Kondic.
Hata hivyo mbio za Yanga ziliisha baada ya kutolewa na mabingwa wa kihistoria Afrika, Al Ahly ya Misri kwa jumla ya mabao 4-0, ikianza kufungwa 3-0 Machi 15 mjini Cairo  na baadaye 1-0 wiki mbili baadaye Dar es Salaam.
Kutokana na matokeo hao Yanga sasa wanahitaji ushindi wowote, sare ama wasifungwe zaidi ya mabao 7-0 ili waingie raundi inayofuata, ambapo watacheza na Ahly , ambao ndio mabingwa watetezi wa Afrika.

Yanga: Juma Kaseja, Mbuyu Twite, Oscar Joshua, Nadir Haroub, Kevin Yondan/Rajab Zahir, Frank Domayo, Simon Msuva/Hassan Dilunga, Haruna Niyonzima, Hamisi Kiiza, Mrisho Ngassa na David Luhende/Didier Kavumbangu.
Komorozine; Attoumani Farid, Ali Mohamed Mouhousoune, Nizar Amir, Abdou Moussoidi Kou, Ahamadi Houmadi Ali, Moidjie Ali, Mourthadhoi Fayssol, Attoumane Omar, Mohamed Erfeda/Imroina Ismael dk30, Mouyade Almansour Nafouondi na Ahmed Waladi Mouhamdi/Ghaidane Mahmoud dk80.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...