Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Friday, August 24, 2012

Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Maalim Seif azungumza na Waislamu, Mwakilishi wa UN nchini


Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Shariff Hamad akizungumza na waumini wa dini ya Kiislamu baada ya Swala ya Ijumaa kwenye Msikiti wa Mtoro, mtaa wa  Mahiwa Kariakoo jijini Dar es Salaam leo.


Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Shariff Hamad, akisalimiana na waislamu mbalimbali baada ya Swala ya Ijumaa huko msikiti wa Mtoro, mtaa wa Mahiwa, Kariakoo jijini Dar es Salaam leo. 



Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Shariff Hamad, akisalimiana na Mwakilishi wa kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako Manongi walipokutana katika hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam leo kwa ajili ya kuagana. Kulia ni Naibu Mwakilishi wa kudumu wa Tanzania Katika Umoja huo, Ramadhan Muombwa Mwinyi.
,

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Shariff Hamad akizungumza na Mwakilishi wa kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako Manongi na Naibu wake Ramadhan Muombwa Mwinyi (katikati), walipokutana katika hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam leo. (Picha zote na Salmin Said, OMKR)

Na Hassan Hamad, OMKR.


DAR  ES SALAAM
  24/08/2012.

MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad amesema kazi kubwa inayowakabili wawakilishi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa ni kutetea maslahi ya Tanzania katika Umoja huo.

Amesema Tanzania pamoja na nchi nyengine zinazoendelea zinakabiliwa na changamoto nyingi, lakini njia pekee ya kutatua changamoto hizo ni kushirikiana na kutetea maslahi ya nchi zao na Afrika kwa ujumla.

Maalim Seif ametoa changamoto hiyo katika hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam leo, alipokutana na Mwakilishi wa kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa balozi Tuvako Manongi na msaidizi wake Mhe. Ramadhan Muombwa Mwinyi walioteuliwa hivi karibuni kushika nyadhifa hizo.
Amesema licha ya kuwa wana kazi kubwa ya kufanya kutokana na changamoto nyingi zilizopo, lakini wanaweza kufanikisha majukumu yao vizuri iwapo watashirikiana vyema na wawakilishi wengine  kutoka nchi zinazoendelea.
“Nchi zinazoendelea ni nyingi mno, nazo zina wawakilishi wao katika Umoja wa Mataifa, iwapo mtashirikiana vyema na wenzenu hawa wan chi nyingine, mtaweza kutatua kero zilizopo kwa urahisi”, alinasihi Maalim Seif.
Amesema nchi zinazoendelea zinakabiliwa na matatizo yanayofanana, na kwamba masuala yanayopaswa kupewa kipaumbele kwa sasa ni pamoja na mapambano dhidi ya janga la UKIMWI pamoja na mabadiliko ya tabia nchi.
Amewatakia kheri wawakilishi hao wa Umoja wa Mataifa, na kuahidi kutoa ushirikiano unaohitajika wakati wowote   katika kusogeza mbele maendeleo ya Tanzania kwenye Umoja huo.
Kwa upande wake balozi Manongi amesewa watatumia uzoefu walionao katika kufanikisha majukumu waliyopewa, na kuomba ushirikiano wa karibu kutoka kwa viongozi wa nchi.

Nae Naibu Mwakilishi wa kudumu wa Tanzania katika Umoja huo Mhe. Ramadhan Muombwa Mwinyi amepongeza kitendo cha kukutana na viongozi mbali mbali wakiwemo Makamu wa Kwanza na Makamu wa Pili wa Rais, na kwamba mawazo waliyoyapata kutoka kwao yatakuwa ni dira ya utekelezaji wa majukumu yao.

Wawakilishi hao wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa walionana na Makamu wa Kwanza wa Rais kwa ajili ya kuagana nae wakati wakijiandaa kuelekea katika kituo chao kipya cha kazi mjini New York, Marekani mwishoni mwa mwezi huu.

Wakati huo huo Makamu wa Kwanza wa Rais ametoa wito kwa waislamu kuungana na kuwa kitu kimoja ili kuipa nguvu zaidi dini hiyo.
Amesema ni jambo la kusikitisha kuona waislamu nchini wamekosa mshikamano, umoja na upendo, na hatimaye kushabikia mifarakano isiyokuwa na manufaa yoyote kwa waislamu.

Maalim Seif ametoa kauli hiyo, wakati akiwasalimia waislamu baada ya sala ya Ijumaa huko msikiti wa Mtoro mtaa wa Mahiwa, Kariakoo jijini Dar es Salaam.
Amesema wakati umefika kwa Waislamu kushikamana, na kutoa wito kwa Masheikh kuwaunganisha wafuasi wao, ili kuwa kitu kimoja kwa lengo la kuongeza nguvu katika kuuendeleza Uislamu.

Pia Makamu wa Kwanza wa Rais amewataka waislamu kuitumia fursa iliyopo ya kutoa maoni katika tume ya mabadiliko ya katiba, ili kuelezea kero zinazowakabili na kupelekea kupatikana kwa katiba itakayojali matakwa yao.
Amesema katika kufikia matarajio hayo, viongozi wa dini wana wajibu wa kuwaandaa wafuasi wao katika kutoa maoni ya katiba, kwa vile wengi wao hawaifahamu katiba ya sasa na changamoto zilizopo.

Katika hotuba yake Imamu wa Msikiti huo Sheikh Zubeir Yahya amesema kuna haja kwa viongozi wa kiislamu kukaa pamoja na kutoa msimamo wa pamoja juu ya masuala mbali mbali ya kijamii likiwemo la sense, ili kuepuka kuwapotosha wananchi kwa kutolewa misimamo tofauti ya viongozi wa dini moja.
Aidha Sheikh Zubeir amewatanabahisha waislamu kujipanga ili kuanzisha vyuo vikuu vya kiislamu nchini pamoja na vyuo vya taaluma mbali mbali, ili kuwaandaa vijana wa kiislamu kuifahamu dini yao na kuwawekea misingi imara ya kuiendeleza.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...