Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Friday, August 31, 2012

WAHANDISI KUADHIMISHA SIKU YAO MWEZI SEPT, JIJINI DAR


Mhandisi Prof. Ninatubu Lema
- Wawataka Watanzania  kutumia Wakandarasi Waliosajiliwa
Na Aron Msigwa – MAELEZO.

Dar es salaam.

Katika kuelekea maadhimisho ya Siku ya Wahandisi nchini Bodi ya Usajili wa Wahandisi nchini imewataka watanzania kutumia huduma za  wakandarasi waliosajiliwa kisheria ili kuepuka kupata maafa na hasara inayotokana na ujenzi hafifu usiokidhi viwango.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam mwenyekiti wa bodi hiyo Prof. Ninatubu Lema amesema  kuwa wakati umefika kwa watanzania kuwaamini wahandisi wa ndani kutokana na kazi nzuri zinazofanyika na  hatua kubwa iliyofikiwa katika utoaji wa huduma bora  za ushauri na ujenzi tofauti na kipindi kilichopita.

Amesema katika kuimarisha  na kuboresha huduma za ushauri na ujenzi  nchini Bodi ya Usajili wa Wahandisi nchini kwa kushirikiana na wadau wengine wa taasisi za kihandisi  pamoja na wale wa Jumuiya ya Kihandisi watakutana jijini Dar es salaam kwa lengo la kuoinyesha jamii kile ambacho wahandisi wa Kitanzania wanaweza kukifanya katika kuleta maendeleo nchini.

Ameeleza kuwa hivi sasa kuna wahandisi wengi wanaofanya shughuli za usimamizi wa miradi mbalimbali ya ujenzi wa miundombinu nchini ikiwemo miradi ya barabara , gesi na shughuli za uchimbaji wa madini pia wapo wahandisi wa kitanzania wanaofanya kazi za ushauri katika mataifa mbalimbali ndani na ne ya bara la Afrika.

‘’Kwa upande wetu Tanzania wakati tunapata uhuru tulikua na wahandisi 2 na sasa wako zaidi ya elfu kumi ,jambo hili ni kubwa kwa sababu mchango wa wahandisi sasa tunauona katika kuleta maendeleo ya taifa maana bila ya kuwa na wahandisi vitu vyote tunavyoviona kama barabara, majengo, na miundombinu mbalimbali haviwezi kuwepo”

Prof. Lema amesema maadhimisho ya Siku ya Wahandisi nchini yanalenga kuwatambua wahandisi na makampuni  na mashirika ya Kihandisi yaliyotoa mchango mikubwa ya kihandisi katika maendeleo ya taifa na kuwahamasiha wahandisi wengine kufanya shughuli zao vizuri zaidi.

Ameongeza  kuwa maadhimisho yataambatana na tuzo mbalimbali zenye lengo la kuwatia Moyo wanafunzi wahitimu kutoka vyuo vikuu na Taasisi za Uhandisi nchini pamoja na taasisi zitakazotia fora kwenye maonyesho ya ufundi pia kuwafanya vijana washawishike kusomea taaluma ya uhandisi.

Kwa upande wake msajili wa Bodi ya Usajili wa wahandisi Eng. Steven Mlote akizungumzia kuhusu ubora wa majengo yanayoendelea kujengwa kwa wingi jijini Dar es salaam amesema kuwa wamiliki wa majengo hayo wanao mchango mkubwa katika kuhakikisha kuwa ujenzi wa majengo yao unazingatia viwango.

Amesema yeye kama msajili anawashauri wamiliki wa majengo kuhakikisha kuwa majengo yao yanayojengwa hivi sasa yanajengwa na wahandisi waliosajiliwa huku akitoa tahadhali kwa wale wanaokiuka kanuni zilizowekwa katika kusimamia ujenzi wa majengo nchini.

“Nawaomba wamiliki wote kuhakikisha kuwa pindi wanapoanza ujenzi wa majengo yao wahakikishe kuwa wanawatumia makandarasi waliosajiliwa, na mtu yeyote anayeruhusu jingo lake kujengwa na watu au kandarasi zisizosajiliwa anakiuka sheria na anastahili kushtakiwa” amebainisha Mlote.

Kwa upande wake Eng. Benedict. Mukama amewataka wananchi kutoa ushirikiano katika kuyabaini majengo yote yanayojengwa nchini chini ya viwango na kutoa taarifa kwa mamlaka husika ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya makandarasi wanaohusika na ujenzi wa miradi hiyo huku akieleza kuwa katika mwaka wa fedha 2011/2012 zaidi ya miradi 164 iliyokuwa inajengwa kinyume cha utaratibu bila kuzingatia viwango ikiwemo ya barabara imesimamishwa.

Aidha amesema maadhimisho haya ya siku ya wahandisi 2012 ambayo yanaadhimishwa nchini kwa mara ya 10 yatakuwa na mvuto wa pekee kwa kuwa yanawawahusisha washiriki kutoka kutoka nchi za Maziwa Makuu,Afrika ya Mashariki na zile za Jumuiya ya Maendeleo ya  kusini mwa Afrika (SADC).

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...