Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Wednesday, August 29, 2012

SIMBA YAICHAPA OLJORO ARUSHA


Akuffo; Habari picha kwa hisani ya bongostaz.blogspot.com
Na Prince Akbar
SIMBA imeibuka na ushindi wa mabao 2-1 jioni hii kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha dhidi ya wenyeji JKT Oljoro katika mchezo wa kirafiki wa kujipima nguvu kabla ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, inayotarajiwa kuanza katikati ya mwezi ujao.
Mshambuliaji kutoka Stella Abidjan ya Ivory Coast, Mghana Daniel Akuffo ameendelea kutunisha akaunti yake ya mabao Msimbazi, akifikisha mawili wakati Mrisho Khalfan Ngassa amefungua rasmi akaunti yake ya mabao leo katika mchezo huo.
Akuffo aliifungia bao la kwanza Simba SC dakika ya 25, akiunganisha pasi ya Ngassa- hilo likiwa bao lake la pili tangu aanze kuichezea timu hiyo mwezi huu, baada ya awali kufunga kwenye Uwanja huo huo Jumapili dhidi ya Mathare United ya Kenya katika ushindi kama wa leo, 2-1.
Ngassa alifungua akaunti yake ya mabao Simba SC dakika ya 76 akiunganisha pasi ya Abdallah Juma ‘Dullah Mabao’ na Oljoro ilipata bao la kufutia machozi dakika ya 89 kwa penalti iliyotiwa nyavuni na Markus Mpangala baada ya Paschal Ochieng kumuangusha mchezaji huyo wa timu ya Maafande wa Jeshi la Kujenga Taifa kwenye eneo la hatari.   
Simba itakuwa na mechi nyingine ya kujipima nguvu Jumapili, Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam dhidi ya Coastal Union ya Tanga, kabla ya kumenyana na Azam katika mechi ya Ngao ya Jamii Septemba 8, mwaka huu, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kihistoria hiyo itakuwa mechi ya tano ya Ngao ya Jamii kuchezwa nchini na ya pili kuishirikisha timu nje ya wapinzani wa jadi wa soka ya Tanzania, Simba na Yanga.
Mtibwa ilicheza na Yanga mwaka 2009, baada ya Simba kugoma na ikashinda mabao 2-1 na kutwaa Ngao, wakati kabla ya hapo, mwaka 2001, Ligi Kuu ya Tanzania ikiwa bado inadhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kupitia bia ya Safari Lager, ilichezwa mechi ya kwanza ya Ngao kihistoria.
Katika mechi hiyo, Yanga ilishinda mabao 2-1 dhidi ya Simba na mwaka juzi Yanga iliifunga tena Simba kwa penali 3-1 kufuatia sare ya 0-0 na mwaka jana, Simba ilitwaa Ngao ya kwanza katika historia yake, kwa kuifunga Yanga mabao 2-0. 

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...