Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Tuesday, August 28, 2012

NIGER, GHANA MABINGWA WAPYA AIRTEL RISING STARS AFRIKA 2012


Niger wakishangilia ubingwa wa Airtel Rising Stars Afrika 2012
NAIROBI, Kenya

MASHINDANO ya Airtel Rising Stars Afrika 2012 yaliyoshirikisha mataifa 15 barani humu yamehitimisha juzi jijini hapa, ambapo mgeni rasmi wa fainali na nyota wa zamani wa ManchesterUnited, Peter Schmeichel, alikabidhi medali na zawadi kwa washindi upande wa wavulana na wasichana.

Niger walifanikiwa kutwaa ubingwa wa kwanza wa michuano ya kwa wavulana, katika fainali ya michuano hiyo, huku Ghana wakitawazwa mabingwa upande wa wasichana katika mashindano hayo – yaliyoanza na timu 18,000 na kujumuisha vijana walio chini ya miaka 17 wapatao 324,000 Afrika nzima.

Niger iliifunga Zambia kwa penati 5-4 kushinda ubingwa Airetl Rising Stars 2012 kwa wavulana, baada ya kumaliza dakika 90 bila ya kufungana licha ya kosa kosa nyingi kwa kila timu, ambapo pia dakika 30 za nyongeza pia hazikutoa mshindi na kulazimika kupigiana penati.

Mamane Karibou, Issa Souleymane, Abubacar Timbo, Idrissa Amadou na Issifou Garba wa Niger walifunga penati, kama ilivyokuwa kwa Wazambia Timothy Sakala, Thomas Juma Mutale, Dennis Chebuye na Albert Bwalya, huku Shadrack Chimanya akikosa mkwaju wake muhimu.

Katika fainali ya wasichana, Ghana walitoka nyuma na kuwafunga wenyeji Kenya waliokuwa wakipewa nafasi kubwa ya kushinda na kuwachapa mabao 2-1.

Kenya walipata bao la uongozi lililowekwa nyavuni na Vivian Odhiambo dakika ya 27, kabla ya Emelia Lokko kuisawazishia Ghana 43 na pambano kuingia mapumziko kwa sare ya bao 1-1. Ghana ikarejea kipindi cha pili ikiwa tishio zaidi, ambapo Patience Narh aliifungia bao la ushindi 56 na kuwaduwaza Wakenya.

Wachezaji vijana 432 walishiriki fainali hizi jijini Nairobi kwa wiki nzima, wakiwezeshwa katika kila mahitaji na wadhamini, waratibu na waendeshaji wa michuano hiyo kampuni ya simu za mkononi ya Airtel, huku vijana hao wakionyesha vipaji vya hali ya juu na kutoa taswira njema ya soka la Afrika.

Mabingwa Niger na Ghana walizawadiwa fedha taslimu dola za Kimarekani 10,000 kila moja, huku zikipata fursa kwa wachezaji wake wote kushiriki Kliniki Maalum itakayofanyika hapa Nairobi na Accra, Ghana, chini ya wakufunzi wa soka kutoka klabu za Arsenal na Manchester United za England.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...