Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Saturday, September 21, 2013

Lipumba, Mbowe, Mbatia wapigwa stop  • Ni maandamano ya kesho
  • Polisi wadai wamepata taarifa za kiinterijensia
Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, limezuia maandamano yaliyopangwa kufanywa kesho na vyama vya Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi kwa lengo la kupinga mchakato wa Katiba mpya. Maandamano hayo pia yana lengo la kumshinikiza Rais Jakaya Kikwete asiusaini Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kwa madai kuwa umehodhiwa na Chama Cha Mapindizi (CCM).

Hata hivyo, polisi imeruhusu vyama hivyo kufanyika mkutano wa hadhara kwenye viwanja vya Jangwani kesho lakini havitaruhusiwa kufanya maandamano. 
Maandamano hayo ambayo yangewashirikisha viongozi, wanachama na wafuasi wa vyama hivyo, yalipangwa kuanzia eneo la Tazara Veterani kupitia Barabara ya Mandela hadi Buguruni Sheli, Uhuru kupitia Malapa, Karume, mzunguko wa Shule ya Msingi Uhuru, Msimbazi, Fire Barabara ya Morogoro hadi viwanja vya Jangwani.
Kamanda wa Polisi Kanda hiyo, Kamishna Suleiman Kova, akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, alisema Jeshi la Polisi halioni umuhimu na sababu za msingi za kufanya maandamano hayo kwani kuna uwezekano mkubwa wa kutokea uvunjifu wa amani.
Kamishna Kova alisema sehemu ambazo maandamano hayo yalipangwa kupita kuna mkusanyiko mkubwa wa watu ambao watakuwa katika shughuli mbalimbali za kiuchumi, usafirishaji na mahitaji mengine ya kila siku ya kibinadamu.
Aidha, Kamishna Kova alisema Jeshi la Polisi limepata taarifa za kiintelijensia kuwa vyama hivyo vimeandaa  uhamasishaji mkubwa kwa watakaotumia pikipiki, guta na watembea kwa miguu.
Kabla ya Kova kutoa uamuzi huo, alikutana katika kikao cha ndani na viongozi wa vyama hivyo.
Katika mkutano huo, CUF kiliwakilishwa na Naibu Katibu Mkuu Bara, Julius Mtatiro na Hamidu Bobali wakati Chadema kiliwakilishwa na Mwenyekiti wa Baraza la Vijana (Bavicha), John Heche na  Mkurugenzi wa Oganaizesheni na Mafunzo, Singo Benson.  Hata hivyo, NCCR-Mageuzi hakikuwakilishwa na kiongozi yeyote.
Kamishna Kova alisema vyama hivyo vikifanya mkutano kwenye viwanja hivyo inatosha kupeleka ujumbe kwa wananchi na maudhui katika kusudio la la kuwashirikisha wananchi katika mchakato wa kuandika Katiba Mpya.
Alisema kama vyama hivyo havijaridhika na makubaliano ya mkutano waliokaa kwa zaidi ya saa mbili na kuafikiana kusitisha maandamano hayo waende kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi, ambaye ndiye atatoa maamuzi zaidi.
“Jeshi letu limejipanga kupeleka askari wa kutosha na katika viwanja hivyo kwa ajili ya usalama zaidi na iwapo kutakuwa na mabadiliko kutoka ngazi za juu, sisi tutatii,” alisema Kamishna Kova.

MBOWE: TUTAANDAMANA
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, akizungumza na NIPASHE kufuatia uamuzi huo wa polisi, alisema ni bahati mbaya kwamba Jeshi la Polisi limeamua kuwa tawi la chama cha siasa badala ya kusimamia sheria za nchi.
Alisema jeshi hilo halijatoa sababu za msingi za kuzuia maandamano hayo zaidi ya kudai yatasababisha msongamano wa magari na kwamba kutokana na hali hiyo maandamano yaliyopangwa kufanyika yako pale pale.
“Tunaendelea kuwasiliana na viongozi wa juu wa Jeshi la Polisi kuwaeleza kuwa maandamano yapo pale pale zaidi watupe ulinzi ili kuyafanikisha kwani yatakuwa ya amani,” alisema Mbowe.
Naibu Katibu Mkuu wa CUF Bara, Mtatiro, alisema chama hicho kitafanya mkutano na waandishi wa habari leo kwa ajili ya kutoa msimamo wa chama.


VIONGOZI WAENDELEZA MASHAURIANO


Katika hatua nyingine, vyama hivyo jana viliendelea na harakati zake za kutembelea taasisi mbalimbali kuomba kuungwa mkono kupinga mchakato wa Katiba mpya kwa kutembelea Shura ya Maimamu. 
Aidha, viongozi wa vyama hivyo wametoa tamko kuwa watawala wasifikirie kwamba kuna nguvu yeyote ya dola  inayoweza kupambana na nguvu ya umma katika suala la Katiba.
Wenyeviti wa vyama hivyo, James Mbatia (NCCR-Mageuzi), Profesa Ibrahim Lipumba (CUF) na Mbowe (Chadema) wameshatembelea Jukwaa la Katiba Tanzania na Shirikisho la Vyama vya Walemavu Tanzania (Shiviwata) na wamepanga kufanya ziara ya kuzungumza na wananchi mikoani.
Amir Mkuu wa Jumuiya ya Taasisi za Kiislamu, Sheikh Mussa Kundecha, alisema baada ya kikao cha ndani na viongozi hao kuwa Shura ya Maimamu imefurahishwa na moto uliowashwa na vyama hivyo katika suala la Katiba na kwamba watawaunga mkono.
Alisema Watanzania ni lazima watambue kuwa suala la Katiba siyo la CCM, hivyo watawala wajifunze kukubali maoni ya wananchi ili kufikia mwafaka.
Sheikh Kundecha alisema Shura ya Maimamu inashangazwa kwani kila wanapopeleka maoni yao katika Tume ya Mabadiliko ya Katiba, tume hiyo imekuwa haileti mrejesho kuhusu nini kinachoendelea, hali ambayo inawapa mashaka.
Kwa upande wake, Mbowe alisema kauli yeyote ya kubeza, kudharau au vitisho haitasaidia, bali inatakiwa itumike njia ya maridhiano ili kumaliza suala hilo kwa amani.
Alisema Katiba mpya ndiyo njia pekee  ya kutibu majeraha yaliyopo, hivyo serikali lazima itambue haiwezi kupunguza makundi mbalimbali ya kiimani kama Shura ya Maimamu, Baraza la Maaskofu na Taasisi nyingine kwani kufanya hivyo kutaleta vurugu nchini. 
Naye Profesa Lipumba alisema uthibitisho kwamba kuna matatizo katika mchakato wa Katiba umethibishwa na Shirikisho la Vyama vya Walemavu Tanzania ambao walieleza kuwa katika majina waliyoyapendekeza hakuna hata mmoja aliyeteuliwa kuingia katika Bunge Maalum la Katiba.
CHANZO: THE GUARDIAN

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...