Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Tuesday, May 13, 2014

Mama Kikwete ataoa changamoto kwa wanafunzi


Mama Salma Kikwete

Na Anna Nkinda- Maelezo, Bagamoyo
Wanafunzi wa shule za Sekondari  wilayani Bagamoyo wametakiwa kusoma kwa bidii na kufanya vizuri kwenye mitihani  yao  kwa kufanya hivyo wataweza kufanikiwa katika maisha yao kwani elimu ni mkombozi wa maisha ya binadamu.
Mwito huo umetolewa hivi karibuni na Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) Mama Salma  Kikwete wakati akiongea kwa nyakati tofauti na wanafunzi wa shule ya Sekondari ya wasichana ya Mandera na Mboga zilizopo wilayani Bagamoyo mkoa wa Pwani.
Mama Kikwete ambaye pia ni Mke wa Rais Dkt.  Jakaya Mrisho Kikwete alisema kama wanafunzi hao watasoma  na kufanya vizuri katika mitihani yao wataweza kufanikiwa  kimaisha, watapata kazi na  kuwasaidia ndugu zao na hivyo kupunguza tatizo la umaskini ndani ya jamii zao. 
“Mjenge tabia ya kusoma kwa makundi msione fahari kukaa nyumbani hasa mwisho wa wiki tumieni muda wenu wa ziada  kusoma  kwa pamoja , mchague viongozi wa makundi na kila mmoja wenu awe na somo la kuwafundisha wenzake hii itasaidia kila mtu kufaidika  na  mwenzake”, alisema Mama Kikwete.
Mwenyekiti huyo wa WAMA aliwaasa wanafunzi wa kike kutokubali kudanganywa na wanaume na kujiingiza katika mahusiano ya kimapenzi wangali wanafunzi kwa kufanya hivyo watapata mimba zisizotarajiwa na ugonjwa wa Ukimwi hivyo kukatisha masomo yao na kutotimiza ndoto zao .
Alionya, , “Msikubali kudanyanywa na wanaume na kujiingiza katika mahusiano ya kimapenzi wakati uko shule hata kama mzazi wako hana hela za kutosha za kukupatia usikimbilie kwa mwanaume bali unaweza ukatumia kipindi cha likizo kufuga kuku wa asili na unaporudi shuleni unawaomba walezi wako wanakuangalizia kuku hao wakikua utawauza na kujipatia pesa”.
Mama Kikwete pia aliwaasa wanafunzi hao kuvaa mavazi ya heshima na kujiheshimu na kuacha kuiga mambo ambayo hayawasaidii katika maisha yao ambayo yanaonyeshwa katika Televisheni  bali wapambane katika masomo ili waweze kufanikiwa katika maisha yao na kama wataona  wenzako hawahudhurii darasani kwa ajili ya utoro wawakanye.
Kwa upande wa walimu aliwata kuwalea wanafunzi hao kama kama watoto wao wa kuwazaa kwani wao ndiyo wanadhamana kubwa katika malezi ya wanafunzi.

Aidha Mama Kikwete alitumia muda huo kuwataka wanafunzi hao kuchukua tahadhari  dhidi ya ugonjwa wa Dengue ambao na hauna kinga na unaenezwa na mbu aina ya Aedes Egyptiae  ambaye hupenda kuuma watu nyakati za mchana.
“Chukueni hatua dhidi ya ugonjwa huu kwani unaua watu kwa kusafisha mazingira na kuua mazalia yote ya mbu kwani mbu huyu mazalia yake ni maji masafi meupe yaliyotuama pia huweza kuwepo hata ndani ya nyumba. 
Alizitaja dalili za ugonjwa huo ni kuumwa kichwa, maumivu ya viungo na uchovu, homa kali, dalili hujitokeza siku ya tatu hadi ya 14 tangu kuambukizwa na kutokwa damu sehemu mbalimbali za mwili.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo  Ahmed Kipozi alimshukuru Mama Kikwete kwa kazi kubwa anayoifanya  na moyo alio nao wa kuwalea na kusimamia elimu ya watoto wa kike jambo ambalo linawapa nguvu  watendaji wa Serikali na kuwapa moyo wanafunzi  ambao wapo katika safari ya kujijengea maisha yao ya baadaye.
Akisoma taarifa ya Shule ya Sekondari ya wasichana Mandera Mkuu wa Shule Rose Umila alisema shule hiyo ina wanafunzi 428 wa kidato cha kwanza 144, cha pili 107, cha tatu 84 na cha nne 93 na walimu 22 kati ya hao walimu wa wasanaa 17, biashara mmoja na sayansi wanne.
Mwalimu Umila alisema, “Kwa upande wa taaluma bado tuna changamoto ya wanafunzi kutofanya vizuri sana ukilinganisha na matokeo ya mwaka juzi ingawa tulijitahidi kupunguza daraja la sifuri. 
Tatizo kubwa lilikuwa ni upungufu wa walimu pamoja na wanafunzi kutokuwa makini kwenye masomo yao, wanafunzi kuchelewa kurudi  kutoka likizo fupi na ndefu hata kwa wale wanaofadhiliwa na mashirika kama CAMFED na wale wanaotoka katika kijiji cha Mandera wanachelewa kurudi bila sababu yoyote”
Alizitaja changamoto zinazowakabili kuwa ni pamoja na  uhaba wa mabweni, ukosefu wa bwalo la chakula, walimu ya Fizikia na Hisabati, nyumba za walimu na shule kutokuwa na usafiri ni tatizo hasa pale wanafunzi wanapoogua ghafla na hasa usiku kwani huduma inapatikana  Hospitali ya Miono.
Naye Mkuu wa Shule ya Sekondari Mboga George Elias alisema Shule hiyo ni shule ya kata ya Msoga inajumla ya wanafunzi 273 kati ya hao wavulana ni 162 na wasichana 111, walimu 23 na watumishi wasio walimu wanne.
“Tunakabiliwa na tatizo la  kuripoti kwa wanafunzi wanaopangwa kuanza kidato cha kwanza ,  uongozi wa Shule na Kata unashirikiana kwa karibu kudhibiti suala zima la kutoripoti na utoro wa wanafunzi Shuleni  kutokana na matatizo hayo wapo wazazi waliofikishwa Polisi na Mahakamani”, alisema Mwalimu Elias.
Alisema kutokana na idadi ya wanafunzi na mikondo iliyopo ambayo ni sita hakuna upungufu wa vyumba vya madarasa kwani wanavyumba saba lakini  kulingana na mpango wa maendeleo wa shule bado kuna upungufu wa majengo.
Changamoto zingine ni upungufu wa vitabu, vifaa vya michezo, walimu wa Sayansi, vifaa vya kufundishia na kujifunzia na vifaa vya mabara, kutokuwa na nyumba za walimu na kutokuwa na nishati ya umeme. 
Mama Kikwete ni Mlezi wa Shule ya Sekondari ya wasichana Mandera na katika shule ya Sekondari Mboga anawalea wanafunzi wa kike. Akiwa katika shule hizo aliwapatia zawadi za vyakula kama mchele, maharage, unga wa ugali, mafuta ya kupikia, sukari, majani ya chai,  vyombo vya kupikia ikiwa ni pamoja na majiko, masufuria na vyombo vya kulia vyakula ambavyo ni sahani, vijiko, vikombe, majagi, majaba ya kuhifadhia maji na kandambili.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...