Hamida Hassan na mitandao ya kijamii
DAWA mpya inayokinga na kuua kwa kasi virusi vinavyosababisha ugonjwa wa Ukimwi, tayari imeshaanza kutumika, hii ni kwa mujibu wa ripoti za mitandaoni.
Dawa hiyo ambayo toleo lake la kwanza ipo kwenye muundo wa vidonge, inaitwa Truvada na tayari imekwishaanza kufanya kazi nchini Marekani.
Kitendo cha Truvada kukubalika na Mamlaka ya Usimamizi wa Chakula na Dawa nchini Marekani (FDA), kinatoa picha kuwa sasa vidonge hivyo vinaweza kuuzwa sehemu yoyote duniani.
Kamishna wa FDA, Margaret Hamburg, amesifu Truvada na kueleza kwamba itapunguza wastani wa maambukizi mapya pamoja na vifo vinavyotokana na ugonjwa wa Ukimwi.
Hamburg alisema kuwa hivi sasa nchini Marekani kumekuwa na kasi ya maambukizi mapya, kwani kila mwaka kumekuwa na wastani wa watu 50,000 wanaobainika kupata Virusi Vya Ukimwi (VVU).
Watafiti waliogundua Truvada wanaeleza kuwa dawa hiyo kwa sehemu kubwa inakinga VVU na upande mwingine inasaidia kuua virusi vya Ukimwi kwa mtu ambaye tayari amekwishaathirika.
Hata hivyo, FDA na watafiti hao, hawajaeleza kama Truvada inatibu moja kwa moja, isipokuwa wanasisitiza: “Inamkinga mtu kupata maambukizi mapya, inamsaidia mwathirika kwa kuua VVU pamoja na kumkinga dhidi ya magonjwa nyemelezi.”
No comments:
Post a Comment