Naibu Katibu JUVICUF |
Ni hivi karibuni watanzania walishuhudia mauaji ya kikatiri
ya kiongozi wa vijana wa CHADEMA kule Arusha mara baada ya uchaguzi mdogo wa
Jimbo la Arumeru Mashariki. Lakini pia tumeshitushwa na mauaji mengine ya
kijana kiongozi wa CCM jimboni Iramba Magharibi juzi baada ya mkutano wa
hadhara wa CHADEMA.
Mauaji ya namna hii huleta hofu kwa vijana kushiriki siasa
za moja kwa moja kwa kuogopa kuuawa. Iwapo mauaji haya ya vijana wanasiasa
hayatapatiwa ufumbuzi kuna hatari ya vijana wenye uwezo kuikimbia siasa na
hatimaye Taifa likakosa viongozi bora wa sasa na baadaye.
Jumuiya ya Vijana ya CUF inaamini kuwa bila kuwa na
utamaduni wa kuvumiliana japokuwa
tunatofautiana kimtazamo, itkikadi, dini na kabila zetu , kamwe hatutaifikia
demokrasia ya kweli. Uvumilivu ni msingi mkuu wa Demokrasia ha hivyo ni wajibu
wetu vijana kuacha kutumikia hisia na mihemko ya miili yetu na vyama vyetu na
kuutanguliza Utanzania wetu na udugu wetu mbele.
Jumuiya ya Vijana ya CUF inawaomba vijana wa CCM na CHADEMA
kuwa makini wakati tukiwa katika mchakato huu wa kuitafuta Demokrasia ya kweli
inayojali misingi ya Haki za binadamu, utawala bora na ushindani wa hoja bila
kuchukiana na kujenga uadui baina yetu kwani sote tuna nia ya kuijenga Tanzania
yenye neema ambayo rasilimali zake zitawafaidisha watanzania wote.
Jumuiya ya Vijana ya CUF imesikitishwa sana na mauaji hayo
ya vijana yanayofanywa na vijana wenyewe kwa wenyewe. Hii ni ishara kuwa Vijana
wa CCM na CHADEMA hawajaiva kisiasa kwani wanashindwa kutofautisha Upinzani na
Uadui. Na kutokana na mauaji haya ni wajibu wa watanzania kutambua kuwa CCM na
CHADEMA hawana dira na sera za kuwafikisha watanzania kwenye neema bali wana
nia ya kuwamaliza kwa kuwaua kikatiri.
Jumuiya ya Vijana ya CUF inawaomba watanzania wawe macho na
mienendo ya vijana wa CHADEMA na CCM maana mauaji wanayoendelea kulipizana
hayatakwisha leo wala kesho. Kwa hiyo wanapaswa kukigeukia chama chao kipenzi
cha Wananchi –CUF ambacho ni chama cha makabwela na wanyonge wa Tanzania.
Imetolewa na:
Thomas D.C Malima
Naibu Katibu Mkuu
Sekretarieti ya
Vijana-Taifa
CUF-Chama Cha Wananchi.
No comments:
Post a Comment