Na Mwandishi Wetu
Ili kuepukana na hujuma
ambazo zinaweza kutokea kwenye mpambano wao, bendi ya Msondo Ngoma itatumia
jenereta dhidi ya mahasimu wao wa jadi Mlimani Park Orchestra “Wana Sikinde”
utakaofanyika siku ya Iddi Mosi katika viwanja vya Leaders Club, Kinondoni.
Meneja wa bendi hiyo, Said Kibiriti, amesema wameamua
kufanya hivyo ili kuepuka hujuma ambazo zinaweza kufanywa na wapenzi wa
wapinzani wao ya kukata umeme na kama
ilivyotokea kwenye pambano la Desemba 25 mwaka jana.
“Tunakumbuka sana
kwenye pambano letu lililopita wakati wa Krismasi mwaka jana pale TCC Club
Chang’ombe, wapenzi wa Sikinde walitukatia umeme kwa makusudi ili tukose
ushindi,” alisema Kibiriti.
Alisema kwa kuepuka hilo
watatumia genereta kubwa kuanzia mwanzo wa shindano hadi mwisho.
Amewatoa wasiwasi wapenzi wa Msondo kuwa jenereta hilo ni kubwa na lenye
uwezo wa kuwasha hata kijiji kizima, hivyo hata kiwango cha muziki utakaopigwa
utakuwa mkubwa. “Jenereta letu litakuwa chini ya ulinzi mkali ili kuepuka
usumbufu,” alisema Kibiriti.
Kwenye pambano la mwaka jana, Msondo ilitumia umeme wa
kawaida ambao ulikuwa ukikatika mara kwa mara, kitu ambacho kilidaiwa kuwa ni
hujuma kutoka kwa wapenzi wa Sikinde ambao wao walikuwa wanatumia umeme wa
jenereta.
Pambano la Msondo na Sikinde tayari limeanza kuvuta hisia za
mashabiki wa muziki wa dansi nchini ambao wanatarajia kumiminika kwa wingi siku
ya Iddi Mosi kwenda kushuhudia mpambano huo iliyodhaminiwa na kinywaji cha
Konyagi.
No comments:
Post a Comment