Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Thursday, February 24, 2011

WAKAZI WA KOTA ZA BANDARI WAMTAKA MKUCHIKA KUKANUSHA KAULI YAKE


WAKAZI wa Gerezani wamemtaka Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Bw.George Mkuchika kuwaomba radhi ndani ya siku saba wakazi hao kwa kauli ya kuwataka wahame haraka iwezekanavyo wakati kesi yao ipo Mahakamani.

Wakizungumza na Waandishi wa Habari leo wakazi hao wamesema kuwa, kitendo cha waziri Mkuchika kutamka kauli hiyo kinaonyesha jinsi gani anavyoingilia uhuru wa Mahakama na kuiweka demokrasia pembeni.

Mwenyekiti wa kamati ya wakazi hao,Bi.Fatma Msindi amesema kuwa, kauli ya waziri huyo kusema kuwa waondoke wenyewe kwakuwa Serikali imeshinda kesi ni cha kuwadanganya wananchi na kuingilia uhuru wa Mahakama.

Alisema kuwa, taarifa hiyo si sahihi kwakuwa kesi ya msingi namba 213 ipo Mahakama Kuu kitendo cha Ardhi Kanda ya Dar es Salaam.

Aliongeza kuwa, zuio la Mahakama liliwekwa Agosti 20 mwaka jana liendelee mpaka shauri litakapoanza kusikilizwa na kesi hiyo itatajwa tena Machi 3, mwaka huu ambapo tarehe hiyo ilipangwa mbele ya mwanasheria wa serikali na mwanasheria wa TBA.

Alisema kuwa kama Bw. Mkuchika hatawaomba radhi watamwagiza mwanasheria wao kuiomba Mahakama Kuu kumfungulia mashtaka ya kuidharau mahakama.

" Sisi tunashindwa kumuelewa Bw.Mkuchika kwakuwa kama anafahamu kuwa, kesi ipo Mahakamani na inaendelea amethubutu vipi kutangaza kuwa wameshinda kesi hiyo na tunatakiwa kuondoka wenyewe haraka iwezekanavyo,tunaomba atuombe radhi haraka iwezekanavyo,"alisema Bi.Msindi.

Aliongeza kuwa, wanashangaa mradi wa mabasi yaendayo kasi (DART) kung'ang'aniwa kuwekwa katika eneo hilo la ekari tano walilouziwa na serikali kihalali wakati yapo maeneo mengi ambayo yangefaa kutumika kwenye mradi huo.

Bi.Msindi alisema kuwa waliwahi kuishauri serikali kuwa, kama mradi huo unahitajika sana kuwepo eneo hilo basi wao pia wana kampuni yao ya Kibasila ambayo ina mradi hivyo vyote viende sambamba.

" Sisi tuna mradi wa ujenzi wa maghorofa yatakayogharimu bilioni 60 ambapo kila mkazi atanufaika na gawio la sh.milioni 63 kwa mwaka na tumepata tayari wafadhili sasa iweje wakatae kuungana nasi na watutake sisi tuondoke kama siyo wana mpango wa kujinufaisha wao wenyewe,"alisema mwenyekiti huyo.

Aliwataka wakazi hao kuendelea kutetea haki zao na kusimama kidete ili kuhakikisha wanapata haki zao na haidhurumiwi na watu wachache kwakuwa serikali ndiyo iliyowashawishi wao kununua nyumba hizo na si wao.

Kwa upande wake, Mwanasheria wa wakazi hao, Dk.Sengondo Mvungi alisema kuwa, mkataba wa manunuzi wa nyumba hizo kwa wakazi na serikali ulikuwa sahihi na haukuwa na shaka yoyote.

Alisema kuwa, kutokana na mkataba huo wakazi wa eneo hilo wana haki kisheria kumiliki ardhi hiyo hivyo ni jitihada zao kuhakikisha kuwa wanasimamia sheria na hawayumbishwi na mtu yoyote.

Alisema kuwa, wakazi 106 ambapo 76 hawajalipwa fidia yoyote na 30 walichukua fidia zao hivyo Serikali ina wajibu wa kutambua kuwa iliwauzia kihalali wakazi hawa na madai yao ni ya msingi.

Aliongeza kuwa anashindwa kutambua kama waziri huyo analielewa fika suala hilo kwakuwa kwa akili zake timamu asingeweza kutamka amri hiyo wakati akifahamu kuwa kesi ipo Mahakamani.

" Huu si utawala bora nadhani waziri Mkuchika kwa hili amekurupuka na anatakiwa kutuomba radhi sisi wakazi na ahakikishe kesi yetu inakwenda kama ilivyopangwa vingine atakuwa anamuingilia jaji kazi yake,"alisema Dkt.Mvungi.

Jana Waziri Mkuchika alikakaria na baadhi ya vyombo vya habari vya TBC na Habari Leo la leo , akiwataka wakazi wa eneo hilo kuondoka wenyewe kwakuwa serikali imeshinda kesi wakati kesi hiyo inadaiwa kuwa bado inaendelea Mahakamani.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...