Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Friday, April 27, 2012

WATANZANIA WAWILI WAOMBEWA ITC UGHAIBUNIWachezaji wawili Watanzania wameombewa Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) kwa ajili ya kucheza mpira wa miguu katika nchini za Denmark na Jamhuri ya Czech.


Chama cha Mpira wa Miguu cha Denmark (DBU) kimemuombea hati hiyo William Benard Okum kama mchezaji wa ridhaa ili ajiunge na timu ya Brabrand IF. Klabu ya zamani ya Okum ni Viko Pham FC ya Zanzibar.

Naye Samwel Jonathan Mbezi ameombewa hati hiyo na Chama cha Mpira wa Miguu cha Jamhuri ya Czech (FACR) ili aweze kuchezea timu ya Sokol Dolany akiwa mchezaji wa ridhaa. Katika maombi hayo, FACR imeonesha kuwa Mbezi kwa sasa hana timu anayochezea hapa nchini.

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linafanya mawasiliano na pande husika kabla ya kutoa hati hizo kwa wachezaji hao kama walivyoomba DBU na FACR.

MECHI KUCHANGIA TWIGA STARS MEI 4
Mechi maalumu ya hisani kwa ajili ya kuchangia timu ya Taifa ya wanawake (Twiga Stars), kati ya timu hiyo na wasanii wa filamu maarufu kama Bongo Movie itachezwa Mei 4 mwaka huu.

Kwa mujibu wa kampuni ya Edge Entertainment iliyoandaa mechi hiyo itafanyika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 jioni kwa kiingilio cha sh. 2,000, sh. 5,000 na sh. 10,000.

Twiga Stars kwa sasa hivi haina mdhamini na iko kambini katika kambi ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ya Ruvu mkoani Pwani inashiriki michuano ya Afrika kwa Wanawake (AWC) ambapo Mei 26 mwaka huu itacheza na Ethiopia jijini Addis Ababa. Fainali za AWC zitafanyika Novemba mwaka huu nchini Equatorial Guinea.

MECHI ZA LIGI KUU WIKIENDI HII
Ligi Kuu ya Vodacom inaendelea katika raundi ya 25 kesho (Aprili 28 mwaka huu) ambapo Coastal Union itakuwa mwenyeji wa Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga huku Mtibwa Sugar ikiwa mgeni wa African Lyon kwenye Uwanja wa Chamazi.

Aprili 30 mwaka huu Azam na Toto African zitacheza Chamazi wakati Mei 1 mwaka huu Villa Squad itaumana na Oljoro JKT kwenye Uwanja wa Chamazi.

Ligi hiyo itafunga msimu wa 2011/2012, Mei 5 mwaka huu ambapo timu zote 14 zitakuwa uwanjani. Simba vs Yanga (Uwanja wa Taifa), Oljoro JKT vs Polisi Dodoma (Sheikh Kaluta Amri Abeid, Arusha) na Ruvu Shooting vs Villa Squad (Mabatini, Mlandizi).

Mechi nyingine zitakuwa kati ya Coastal Union vs Toto African (Mkwakwani, Tanga), African Lyon vs JKT Ruvu (Manungu, Morogoro), Azam vs Kagera Sugar (Chamazi, Dar es Salaam) na Moro United vs Mtibwa Sugar (Jamhuri, Morogoro).

MKUTANO MAKOCHA SIMBA, AL AHLY SHANDY
Makocha wa timu za Simba na Al Ahly Shandy ya Sudan kesho (Aprili 28 mwaka huu) watakuwa na mkutano na Waandishi wa Habari kuzungumzia walivyoandaa vikosi vyao kwa ajili ya mechi ya Jumapili.

Mkutano huo utafanyika saa 4 kamili asubuhi kwenye ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF). Mechi hiyo ya Kombe la Shirikisho itachezwa Uwanja wa Taifa kuanzia saa 10 kamili jioni.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...