Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Saturday, September 6, 2014

Uhaba wa walimu Elimu ya Dini tatizo kubwa nchini-IEPhttp://www.educatedanxiety.com/wp-content/uploads/2014/08/quran-2.jpgNA SULEIMAN MSUYA
JOPO la Elimu la Waislam (IEP) limesema pamoja na mafanikio yanayopatikana katika kuhakikisha kuwa elimu ya dini inapatikana nchini kote bado wanakabiliwa na changamoto kubwa ya uchache wa waalimu wenye taaluma hiyo.
Hayo yamebainishwa Afisa Mwandamizi wa (IEP) Suleyman Daud wakati akizungumza na mwandishi wa habari hii jijini Dar es Salaam.
Daud alisema tangu utaratibu huo wa kutoa elimu ya dini uanze wamepata mafanikio makubwa jambo ambalo linawapatia hamasa ya kuendelea kuboresha ili uweze kutoa tija kwa vijana wa Kiislaam hapa nchini.
Alisema jitihada zao zimejikita katika kuwapatia elimu ya dini vijana wakiislam ambao wanamaliza vyuo mbalimbali hapa nchini kuanzia ngazi ya cheti, stashahada na shahada ili waweze kutoa elimu kwa vijana wa shule za msingi.
“Napenda kuwaambia Watanzania jamii ya Kiislam kuwa juhudi zetu zinaenda vizuri za kuwapatia vijana wao elimu ya dini ila changamoto kubwa ni uchache wa walimu wenye elimu hiyo kuwafundisha” ,alisema.
Afisa Mwandamizi huyo wa (IEP) alisema pamoja na changamoto hiyo ya uchache wa waalimu mafanikio yamekuwa yakiiongezeka kwa shule nyingi kuongezeka katika kufanya mitihani hiyo ambayo haina athari yoyote katika matokeo ya darasa la saba.
Daud alisema katika mtihani wa mwaka jana mikoa 26, wilaya 94 na shule 2,100  ya Tanzania Bara na Visiwa zilishiriki watahiniwa walikuwa 68,096 ambapo ufaulu ulikuwa asilimia 38.04.
Aidha Afisa alisema kwa matokeo ya mwaka huu wa 2014  mtihani ambao ulishirikisha mikoa 26, wilaya 115, shule 2559 na wahitimu 74192 na ufaulu ni sawa na asilimia 46.45 ambao ni ongezeko la asilimia 8.
Alisema mitihani hiyo itakuwa ikifanyika kila mwaka kwa wanafunzi wa wakiislam wanaomaliza la saba  ambapo lengo lao ni kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2017 mitihani hiyo iwe inatambulika kwenye Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA).
Daud alisema pamoja na ukweli kuwa mitihani hiyo kutotambulika katika baraza la mitihani bado vijana wa kiislaam wamekuwa wakishiriki bila kuleta pingamizi hasa katika shule ambazo zinaendeshwa kwa taratibu za kiislaam.
Afisa Mwandamizi huyo alisema katika kufikia malengo hayo juhudi zinahitajika kutoka kila pande hasa kwa wazazi kwani ni wazi kuwa elimu hiyo inawajengea uadilifu na upendo vijana hao.
‘Unajua kwa muda mrefu elimu ya dini imekuwa ikitolewa kwa wanafunzi wa sekondari pekee jambao ambalo imeifanya NECTA kulitumia somo hilo katika kutafsiri matokeo ya mwanafunzi hivyo lengo letu ni kuhakikisha elimu hiyo inakuwa rasmi katika elimu ya msingi”, alisema.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...