Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Monday, July 21, 2014

DAH! FLOYD MAYWEATHER NGUMI 221 ZAMFANYA ARUDI TENA KUZIPIGA NA MAIDANA


NA ALLY KAMWE.
RASMI!  Floyd ‘Money’ Mayweather atapanda tena ulingoni September 13 pale MGM Grand hotel, Las Vegas  kucheza pambano la marudiano na bondia Marcos Maidana. Kwa sasa ulimwengu wa masumbwi unaonekana kulihitaji zaidi pambano hili  kuliko pambano la Myweather na Mphilipino Manny Pacquiao.
Mayweather Maidana 2 Mayweather vs. Maidana 2  marcos rene maidana floyd mayweather jr Hii ni mara ya pili kwa Mayweather mwenye rekodi ya kushinda mapambano yote 46 aliyocheza mpaka sasa kukubali kucheza pambano la marudiano! Si kawaida ya Mayweather kupigana kwa mara ya pili na mpinzani aliyekwishampiga awali, lakini sasa imekua tofauti na imemlazimu kukubali  kutokana na utata uliopo baada ya matokea ya pambano la awali baina yake na Maidana ambapo Mayweather aliibuka mshindi kwa tofauti ya pointi.
Pamoja na matokeo kuonyesha kuwa Mayweather alishinda kwa tofauti ya pointi lakini wadau wengi wa mchezo huo wanaamini Mayweather alipoteza pambano lile kulingana na namna Maidana alivyoweza kucheza na kummiliki Mayweather katika raundi zote 12 za pambano lile.
Baada ya kukubali kucheza pambano hili  Floyd Mayweather  anayetafuta rekodi ya dunia ya kucheza mapambano 50 bila kupoteza alitoa sababu muhimu ambazo kwa kiasi kikubwa zimemfanya kutofikiria mara mbili katika uamuzi wake wa kucheza tena pambano la marudiano na Maidana.
NGUMI 221 ALIZOPIGWA NA MAIDANA ZAMCHANGANYA!
Huenda wengi wasilijue hili, lakini ndicho alichokisema bondia huyu sugu wa Kimarekani  kuwa makonde 221 aliyopigwa na Maidana katika pambano lao la kwanza  ndio yamemfanya kukubali tena kupanda tena ulingoni na mkali huyo kutoka Argentina.
Mayweather alisema kuwa idadi hiyo ya ngumi alizopigwa na Maidana ni idadi kubwa zaidi kupigwa katika historia yake ya masumbwi hali inayomfanya kujiuliza kila mara ni vipi Maidana alipata nafasi ya kumpiga idadi hiyo kubwa ya makonde.
Takwimu zimekua zikionyesha kuwa katika jumla ya makonde 858 yaliyotupwa na Maidana ambayo ni sawa na asilimia 26, makonde 221 yalifika katika mwili wa Mayweather. Hiki ndicho kinachompa wazimu Floyd Mayweather
“Alishinda kwa raundi tatu mpaka nne dhidi yangu, haijawahi kuwa hivyo kabla. Ni lazima nijiulize ni vipi hali hiyo ilijitokeza”  Alisema Mayweather
 
MASHABIKI WANAMPA ‘STRESS’,
Heshima imeshuka! Ndivyo anavyoamini Mayweather baada ya kuwepo kwa minong’ono mingi ya watu kudai kuwa alipendelewa katika pambano lake la awali. Wadau wengi wa mchezo huo wamekuwa wakiamini kuwa Mayweather alibebwa na majaji  wakati wa ugawaji pointi katika pambano lao la awali jambo linaloonekana kumnyima raha bondia huyo.
“ watu wameshindwa kuulewa mchezo wa ngumi, wametazama kwenye raundi tatu za mwanzo na kutoka maamuzi yao, hakuna anayejua nini kiliendelea  kwenye raundi 9 zilizobaki. Nilishinda, na nitashinda tena ili kumaliza utata huu” alisema  Mayweather kuonyeshwa kukerwa na maneno ya watu.
 “ Sirudi tena ulingoni kwa ajili yake, narudi kwa ajili ya mashabiki. Mashabiki wameonyesha kuhitaji sana hili pambano hivyo sinabudi kukubali. Sikubebwa wala sikubahatisha na nitalithibitisha hilo September 3”  aliongezea mwanamasumbwi huyo anayeongoza kwa kuwa na mkwanja mrefu zaidi duniani kwa sasa kwa upande wa wanamichezo
NGEBE ZA MAIDANA ZAMKOSESHA USINGIZI
Dogo anachonga sana! Tangu kumalizika kwa pambano la awali May 3 mwaka huu, bondia Marcos Maidana amekuwa akijitapa na kutangaza kuwa yeye ndie aliyestahili kutangazwa mshindi. Kama wengi wanavyoamini ndivyo Maidana anavyoamini  kuwa alimpiga Mayweather.
Jambo hili linaoneka kumkera sana Mayweather kiasi cha kuamini kuwa bila kurudi ulingoni kuzichapa tena na Maidana huenda akawa ameacha dosari katika rekodi zake za masumbwi duniani. Ni lazima aje amfunge mdomo Maidana katika hili
“ ametaka mechi nyingine, nimekubali. Silalamiki tena kuhusu ‘gloves’ zake. Anadai alishinda pambano la kwanza, hivyo ni bora aje afanye tena na ‘gloves’ zake zilezile” alisema Mayweather kuonyesha kuchukizwa na tambo za Maidana.
Awali Mayweather alionekana kulalamika juu ya ‘gloves’ alizokuwa akizitumia Maidana kuwa zimetengenezwa maalumu kwa ajili ya kuongeza uzito wa ngumi lakini sasa mkali huyo amekubali Maidana arudi tena ulingoni na ‘gloves’ zake zilezile alizotumia awali.
MAYWEATHER BWANA! ETI ATATUMIA MBINU ZA WAJERUMANI KWENYE ‘WORLD CUP’.
Haishi mikwara huyu! Baada ya kuwaangalia Wajerumani wakiwaangamiza Waargentina kwenye dimba la Estadio do Maracana pale nchini Brazil, Floyd Mayweather amesema safari hii atatumia mfumo uleule wa Wajerumani katika kumchakaza mpinzani wake Maidana anayetokea kwenye taifa la Argentina.
“ kama walivyofanya Wajerumani, ndicho nitakachokifanya kwa Muargentina mwingine (akimmaanisha Marcos Maidana)” alitamba Mayweather!
Ni Pambano muhimu kwa Mayweather kwa ajili ya kuzima ngebe za Maidana, ni pambano muhimu kwa Maidana pia kwa ajili ya kuionyesha dunia kuwa ni kweli alionewa kwenye mpambano wa awali. Dunia ya masubwi inasubiri kufika September 13 mwaka huu pale Las Vegas.
Nisisahau, hili pia ni pambano muhimu kwa rafiki yangu Yassin Ustadh kwa ajili ya kuwaonyesha vijana wake kuwa kupigwa ni sehemu ya changamoto ya mchezo. Lini Maugo amewahi kuzisifia ngumi alizopigwa na Mashali ama Mashali kuzisifia ngumi alizopokea kwa  Francis Cheka?  Ustadh, ngumi 221 alizopigwa Mayweather zimemrudisha ulingoni tena huku akijilaumu na kujishangaa! Vipi vijana wako, wanasemaga haya?
 
MATOKEO YA POINTI ZA MAJAJI ZILIZOZUA UTATA PAMBANO LA AWALI
                             MAYWEATHER VS MAIDANA
JAJI NAMBA 1               JAJI NAMBA 2                        JAJI NAMBA 3
117-111,                         116-112                                         114-114
kwa hisani ya gazeti la dimba
 .

JUMAPILI YA JULAI 20/ 2014

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...