Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Sunday, July 27, 2014

TAARIFA YA JESHI LA POLISI KUELEKEA SIKUKUU YA EID-EL-FITR


Jeshi la Polisi Tanzania linapenda kutoa shukrani za dhati kwa wananchi wote, vyama vya siasa, taasisi mbalimbali za serikali, madhehebu ya dini, asasi za kiraia na vyombo vya habari kwa ushirikiano wa dhati katika kusimamia masuala ya amani na usalama hapa nchini.

Tunapoelekea kipindi hiki cha kusherehekea sikukuu ya Eid-El-Fitr, Jeshi la Polisi linatoa wito kwa wananchi wote kuwa makini na kusheherekea sikukuu hiyo kwa amani na utulivu pasipo vitendo ama viashiria vyovyote vya uvunjifu wa amani.

Ikumbukwe kuwa, wananchi wenye imani ya kiislam na hata madhehebu mengine hutumia muda huo kwenda kuabudu pamoja na muendelezo wa sherehe hizo kwenye maeneo mbalimbali ya starehe. Uzoefu umeonyesha kuwa baadhi ya watu hutumia kipindi hicho cha sikukuu kama mwanya wa kufanya matukio ya uhalifu kutokana na mikusanyiko hiyo ya watu.

Jeshi la Polisi linapenda kuwaondoa hofu wananchi wote kuwa, limejipanga kikamilifu kuhakikisha wananchi kote nchini wanasherekea sikukuu hiyo kwa amani na utulivu. Ulinzi umeimarishwa kwenye maeneo yote ya kuabudia, fukwe za bahari, sehemu za starehe na maeneo mengine yote, aidha,  tunapenda kuwatahadharisha wale wote ambao watakuwa wakitumia barabara, kuwa makini kwa kuzingatia sheria za usalama barabarani na hasa kwa madereva wa magari na pikipiki kuepuka kwenda mwendo kasi na kutumia vilevi wawapo kazini.

Katika kuhakikisha usalama kwenye kumbi za starehe, wamiliki wa kumbi hizo wazingatie uhalali na matumizi ya kumbi zao katika uingizaji wa watu kulingana na uwezo wa kumbi hizo, badala ya kuendekeza tamaa ya fedha kwa kujaza watu kupita kiasi.
Jeshi la Polisi linapenda kuwashukuru wale wote ambao tayari wamefunga kamera za CCTV katika maeneo yao ya starehe, hususani yale yanayokuwa na mikusanyiko mikubwa ya watu, yakiwemo maduka, hoteli na maeneo ya benki. Aidha, Jeshi la Polisi linaendelea kuwasisitiza wale ambao bado hawajaweka kamera hizo, kuweka ili ziweze kusaidia kubaini wahalifu na hata kurahisisha ukamataji endapo uhalifu unatokea.

Vilevile, wazazi wawe makini na watoto wao na hasa disko toto, ili kuepuka ajali na matukio mengine yanayoweza kusababisha madhara juu yao.

Aidha wananchi wachukue tahadhari watokapo kwenye makazi yao wasiache nyumba wazi ama bila mtu na watoe taarifa kwa majirani zao, na pale wanapowatilia mashaka watu wasiowafahamu wasikae kimya bali watoe taarifa haraka kwenye vituo vya Polisi vilivyo karibu nao au kwa namba ya simu ifuatayo 0754 785557, ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa haraka.

Imetolewa na:
Advera John Bulimba - SSP
Msemaji wa Jeshi la Polisi.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...