Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Thursday, August 12, 2010

KOCHA WA POOL ATUA KUIFUNDISHA TIMU YA TAIFA
Denis Lungu akizungumza


Mwenyekiti wa TPA Isack Togocho kulia akimtambulisha kocha wa timu ya taifa Denis Lungu kutoka Zambia

BAADA ya kilio cha muda mrefu kuhusiana na kocha wa timu za Taifa za Pool table nchini, hatimaye kilio hicho kimesikika baada ya wadhamini wa mchezo huo nchini Safari Lager kukisikia na kuamua kusaidia ujio wa kocha kutoka nchini Zambia.

Kocha huyo kijana Denis Lungu ambaye ana umri wa miaka 27, amesaini mkataba wa miaka miwili ambao umeanza rasmi Agosti Mosi mwaka huu hadi Julai 28 mwaka 2012 huku akihaidi kuibadilisha Tanzania na kuifikisha katika medani za kimataifa kwenye mchezo huo.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa kumtambulisha kocha huyo katika mkutano uliofanyika kijiji cha Makumbushi jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa TAPA, Amos Kafwinga alisema uamuzi wao wa kumleta kocha huyo unatokana na jukumu walilonalo kama chama ni kuhakikisha wanafanya kila jitihada kuuinua mchezo huo na mojawapo ni kuwa na kocha wa uhakika.

“Lengo la kumleta kocha huyu ni kama inavyoeleza katiba yetu kuwa chama kitasimamia na kuendeleza mchezo wa Pool, hivyo kutokana na jukumu hili ni lazima tuwe na kocha wa uhakika mwenye uwezo mzuri wa kutufikisha kule tunakohitaji.

“ Na kama haitoshi, ni azma ya chama chetu kuhakikisha mchezo huu unachezwa kwa kufuata sheria na viwango vinavyoeleweka ili uwe na ladha hata mtazamaji afurahie kuangalia ili kutekeleza vema azma ya mdhamini wetu bia ya Safari Lager ya kuleta mapinduzi ya kweli na mafanikio makubwa katika mchezo wa Pool nchini” alisema Amos.

Akizungumzia mikakato yake katika kuundeleza mchezo huo nchini, Denis alisema atahakikisha anatumia uwezo wake wa hali ya juu ya kuucheza mchezo huo wa takribani miaka 15 kuhakikisha anaibadilisha Tanzania na kutamba katika medani za kimataifa.

“Matamanio yangu ni kuusogeza mbele na siku za usoni Tanzania itambulike kwenye ramani ya Dunia ya mchezo huo si kwa kuwa washiriki, bali wachezaji wake waweze kuucheza kwa kufuata sheria, kanuni na viwango vya hali ya juu” alisema Denis.

Hata hivyo aliwataka viongozi wa mchezo huo na Serikali kwa ujumla kuhakikisha mchezo huo unaasisiwa zaidi shuleni ili watoto waanze kujifunza huko na si kusubiri vijana wa umri wa kati ambao wanatuhusiwa kwenda baa ndio wajifunze maana ndipo meza za mchezo huo zinapopatikana jambo lililochangia mchezo huo kushindwa kupiga hatua za haraka.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...