Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Tuesday, November 9, 2010

kongamano la muziki nchini,kuandaliwa na BASATA


Na Alistide Kwizela


Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) liko kwenye mikakati ya kuandaa kongamano kubwa la muziki linalotazamiwa kufanyika katika siku za hivi karibuni ili kujadili mwenendo mzima wa fani hii ikiwa ni pamoja na kujenga utambulisho wa muziki wa Tanzania.

Katibu Mtendaji wa BASATA Ghonche Materego aliweka wazi hilo wakati akifafanua masuala mbalimbali yaliyojitokeza kwenye Jukwaa la Sanaa linalofanyika kila Jumatatu kwenye Ukumbi wa BASATA ambapo alisema kwamba,kongamano hilo pamoja na mambo mengine litakuja na majibu kadhaa ya changamoto mbalimbali zinazoikabili fani ya muziki nchini sambamba na kujenga heshima ya wasanii wa Tanzania ndani na nje ya nchi.

“Tunakusudia kufanya kongamano kubwa ambalo litahusisha maproducer, wadau wa vyombo vya habari, mapromota, wasanii wote wa muziki na wadau mbalimbali wa sekta ya sanaa ili sasa kwa pamoja tujiulize ni muziki gani tunaoutaka, fani yenyewe iendeje na ni kwa vipi tutajenga utambulisho wa muziki wetu na hivyo kuuzika kimataifa” alisisitiza Materego.

Aliongeza kwamba, muda umefika sasa kwa wasanii wa muziki na wadau wote kukaa chini na kukuna vichwa juu ya muenendo mzima wa fani hii kwani kwa muda mrefu kumekuwa na changamoto nyingi ambazo zimekuwa zikiibuka na kuzua wasiwasi wa fani hii kudidimia na kukosa muelekeo kama jitihada za makusudi hazitafanyika.

Alihoji tabia inayokua kwa kasi ya baadhi ya wasanii wa kitanzania kunakiri vionjo (beats) vya miziki kutoka nje hasa Marekani na kuonesha wasiwasi wa wasanii wetu kuja kuburuzwa mahakamani na hata kutozwa faini kubwa za fedha kutokana na kitendo hicho kukiuka sheria za kimataifa za hakimiliki na hakishirikishi.

“Mimi najiuliza sana hivi siku wasanii wa Marekani wakija Tanzania na kuwaburuza wasanii wetu mahakamani kwa kosa la kunakiri kazi zao bila ruhusa nani atapona kiama hiki?Nasema hivi kwani hili haliko mbali kutokana na ukweli kwamba, tunaingiliana nao sasa.Ni lazima haya tuyaangalie mapema ndiyo maana BASATA inaona ni muda muafaka sasa wa kuwa na kongamano hili la wanamuziki wote” alimalizia Materego.

Mada ya wiki hii kwenye Jukwaa la Sanaa iliwasilishwa na Mtangazaji wa ITV/Radio One,Maulid Kambau na ilihusu Mchango wa Maprodyuza wa Muziki Katika Kukuza Utambulisho na Soko la Muziki Tanzania ambapo alilenga kuwakumbusha wasanii na waandaaji wa muziki kujikita kwenye muziki wenye vionjo vya kitanzania na kuacha kabisa tabia inayoota mizizi ya kunakiri kazi za watu wengine.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...