Sasa Bima kulipiwa Kupitia Huduma za Zap
Dar es Salaam, Mai 25, 2010.
KAMPUNI inayoheshimika zaidi Tanzania, Zain, leo inatangaza kutanua zaidi huduma zake za kibenki kupitia simu za mkononi inayojulikana kama Zap, ambapo sasa wateja wataweza kulipia bima ya mali zao hapa nchini kwa njia hiyo.
Kwa hatua hii mpya, Zain kwa kushirikiana na kampuni ya bima ya Real Insurance wanawawezesha wateja wao kuweza kulipia huduma za bima kupitia mfumo wa Zap.
Kupitia simu zao za mikononi, watumiaji wa huduma ya Zap wataweza kulipia bima wakati wowote na mahali popote kila siku.
Akizungumza Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Huduma za Wateja wa Zain Tanzania, Irene Madeje Mlola, alisema huduma ya Zap itawasaidia wateja wenye kuhitaji kulipia bima zao kwa kampuni ya Real Insurance kuweza kuokoa muda ambao wangeutumia na kulazimika kwenda moja kwa moja hadi zilipo ofisi za bima.
“Tunaamini kuwa kupitia huduma hii ya malipo ya bima kwa njia ya Zap, wateja wetu watakuwa na wakati maridhawa wa kufurahia huduma hiyo kutokana na uharaka na wepesi wa kuipata,” alisema.
Zain Tanzania kila wakati imekuwa mbele katika ufumbuzi wa teknolojia katika sekta ya mawasiliano ambapo kwa sasa ina zaidi ya wateja milioni tatu waliojisajili na huduma za Zap.
Akizungumnzia usalama na udhibiti wa malipo ya bima kwa mfumo wa Zap, Mlola alisema huduma hii inalindwa na mfumo maalumu wa kudhibiti usalama wa mteja.
“Mojawapo ya njia za kuhakikisha usalama katika huduma hii ni kuwa na namba ya siri ambayo viambatanisho vyake vinalindwa na mfumo maalumu usiowezesha mtu mwingine kuweza kutumia,” alisisitiza Syed.
Kwa upande wake , Afisa Mtendaji Mkuu wa Real Insurance, George Sithole, alisema kuingia kwa Zap katika huduma zao kutasaidia wateja wao kuwa na njia ya rahisi zaidi ya kufanya malipo ikilinganishwa na ilivyokuwa hapo mwanzoni.
Novemba mwaka jana, Zain Tanzania ilikuwa kampuni ya kwanza ya mawasiliano kuzindua huduma za kibenki kupitia simu za mkononi ambapo wateja husika wamekuwa wakipata huduma hiyo kutoka benki yoyote na taasisi mbalimbali za kifedha nchini na duniani kwa ujumla.
Huduma za Zap kwa sasa zinaweza kutumika kulipa malipo ya Bima, kununua mafuta katika vituo vya Oilcom, Kulipia DSTV, kupokea na kutuma pesa, kulipia LUKU na ankara za maji Dawasco, kupokea na kutuma pesa kupitia benki ya Posta na kwamba huduma hiyo inapatikana karibu katika kila eneo nchini kupitia wakala zaidi ya 4000 wa huduma ya Zap nchi nzima.
Huduma ya Zap pia inaweza kutumiwa na wateja husika hata kama wapo nje ya nchi anayoishi chini ya huduma ya ‘OneNetwork’ .
Huduma ya OneNetwork inawawezesha wateja wa Zain kutumia huduma husika katika nchi yoyote ya ukanda wa Afrika Mashariki na Kati na kwingineko mtandao huo unapopatikana bila gharama za ziada ambapo huweza kupiga na kupigiwa simu ikiwa ni pamoja na kununua muda wa maongezi.
Kujisajili na huduma za Zap ni bure ambapo wateja wa Zain wanatakiwa kujaza fomu maalumu kwa mawakala wa huduma hiyo waliopo katika maeneo tofauti nchini kote.
Baada ya kujisajili Zain hutoa kadi maalumu kwa mteja husika ambayo itamwezesha kupata huduma za kibenki kupitia simu yake ya mkononi kwa kufuata maelekezo malumu yaliyopo katika kadi husika ya jinsi itakavyoweza kutumia simu yake katika huduma hiyo.
No comments:
Post a Comment