TFF yafagilia kombe la Taifa
Na Addolph Bruno
SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania, (TFF) limesema michuano ya Ligi ya Taifa 'Taifa Cup' iliyofanyika wiki iliyopita katika vituo sita nchini, ilifanikiwa kwa kiasi kikubwa.
Mafanikio hayo yalitokana na waandaaji kutoa kanuni za michuano hiyo wiki moja kabla ya kuanza kwa mashindano hayo.
Kauli hiyo ya TFF imekuja siku chache baada ya baadhi ya timu kukata rufani zikilalamikia mashindano hayo kuwa, yalianza vibaya kutokana na ucheleweshwaji wa kanuni.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa TFF, Fredrick Mwakalebela, alisema timu zinazolalamika kuhusu ucheleweshaji wa kanuni, zitakuwa hazina ufahamu wa mpira.
"Kumekuwepo na malalamiko ya hapa na pale kuhusu ucheleweshwaji wa kanuni katika Kombe la Taifa, tulitoa kanuni wiki moja akbal ay mashindano, nadhani hawakuwa makini wenyewe," alisema.
Alisema TFF inaamini kuwa, mashindano hayo yalianza vizuri katika hatua ya makundi na kwamba, itaendelea vizuri hatua inayofuata mpaka atakapopatikana bingwa wa mwaka huu.
Hatua ya robo fainali ya michuano hiyo, itafanyika Dar es Salaam baada ya kuwapata washindi kutoka katika makundi sita ambayo ni Mwanza, Mtwara, Arusha, Dodoma, Tanga na Shinyanga.
No comments:
Post a Comment