Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Thursday, May 27, 2010

Suleimani Mwanyiro na gita la bess lake


Suleiman Mwanyiro 'Komputer '

Mpiga besi aliyetamba kwenye utunzi

# Alishindana na Tx Moshi kutunga

# Aliwaziba mdomo Twanga 2001



Na Seleman Mkangara



MWISHONI mwa wiki iliyopita watanzania waliazimisha miaka minne ya kifo cha mwimbaji na mtunzi mahili wa bendi ya Msondo Ngoma, Shabani Ally Mhoja Kishiwa maarufu kama Tx Moshi William.

Katika maazimisho hayo watanzania walimzungumzia Moshi kama mwanamuziki aliyetoa mchango mkubwa katika bendi ya Msondo na muziki wa kitanzania kwa ujumla hasa kutokana na uwezo wake mkubwa katika suala zima la utunzi.

Kauli hiyo ya wadau hao, imenifanya leo nimkumbuke mwanamuziki Suleimani Mwanyiro aliyekuwa anatambulika kama 'Compyuta' ama Internet ya Mwanyiro ambaye kama ilivyokuwa kwa Moshi William, naye ni mzaliwa wa Tanga.

Tofauti kubwa kati ya Moshi na Mwanyiro ni kwamba Moshi ni Mtanga kwa uzawa tu kwani baba yake ni Msukuma na Mama yake alikuwa Mngoni, lakini Mwanyiro ni mtanga halisi akitokea kwenye kabila la 'Wadigo'.

Na ndiyo maana katika nyimbo nyingi enzi zake akiwa na Msondo Mwanyiro aliyefariki dunia mwaka 2004 alikuwa anatambulishwa kwa kuitwa 'Mgosi Mwanyiro' 'Mzee wa Ngoto'.

Wengi wanamkumbuka Mwanyiro kama mpiga besi mahiri, na wengi walikuwa wanakunwa na mbwembwe zake awapo jukwaani akilikung'uta vilivyo gita hilo zito.Alikuwa ni mtu mwenye midadi ya hali ya juu na anapopiga gita, anaanza kucheza yeye.

Uwezo wake huo wa kupiga gita huku akicheza, ulikuwa ukiwachochea wapenzi wa muziki ambao walikuwa wakiwehuka na kuanza kucheza naye. Ama kwa hakika unapowangalia wapenzi hao unaona dhahiri kuwa akili yao imetekwa vilivyo na gita la Mwanyiro.

Lakini Mwanyiro ambaye kabla ya kuingia katika fani ya muziki wa dansi alikuwa ni mpiga taarabu katika bendi ya Golden Star ya Tanga sambamba na Tatu Said 'Shakira Saidi', hakuwa mahiri katika upigaji gita pekee, bali alikuwa mtunzi mahiri.

Na nyimbo zake nyingi alizotunga hasa akiwa na bendi za Msondo enzi hizo ikijulikana NUTA Jazz, JUWATA Jazz 'JJB' na OTTU Jazz pamoja na zile alizotunga akiwa na DDC Mlimani Park 'Sikinde' zilikuwa zimebeba ujumbe mzito na kukubalika vilivyo kwa wadau wa muziki.

Mwaka 1978 wakati yeye na wanamuziki wenzake Hassan Rehani Bitchuka na Muhidin Gurumo walipoondoka Msondo na kwenda Sikinde, Msondo waliwapiga vijembe kutokana na kuondoka kwao huko. Lakini Mwanyiro aliibuka na kuwalima kwa wimbo wa Duniani Kuna Mambo' wimbo ambao ulinogeshwa zaidi nna sauti ya Bitchuka ambayo ilitamba kwa kiasi kikubwa.

Wimbo huo ulikuwa na mashairi yafuatato.

Bitchuka

Aaaaah! Duniani kuna mambo Unapokuwa ukimya

watakufuata fuata kwa maneno ili wao wakupe sifa mbaya.

Hata ukifanya jambo zuri, wao wanalikashifu

Kwa vile wamezoea kusema ooh wasema mwisho watachoka x2

Kiitikio

Waache waseme mwisho watachoka
Ngoma ya Sikinde tunaiendeleza
Duniani tuacheni maneno maneno
Tutizame duni, inakokwenda mbele

Kiitikio
Gurumo: "Kutetana tetana hakuna maana yoyote
Nawaaombeni walimwengu tushirikiane jamaniii

Aliporudi Msondo kwa mara ya pili hapo ndipo Mwanyiri alipodhihirisha kuwa ana kipaji cha hali ya juu katika utunzi, kwani ndiye mwanamuziki pekee ndani ya bendi hiyo aliyekuwa anachuana na Moshi katika utunzi.
Naamini wengi tunakumbuka wimbo wa kauke Nikuvae. Wimbo huu uliotingisha vilivyo katika miaka ya 1990 ulimkuna kila mpenda muziki nchini na hata wale wasiopenda muziki. Hii inatokana na ujumbe mzito ambao Mwanyiro ameuweka ndani mashairi yake.

Wimbo huo ulikuwa na maneno yafuato.
Mume wangu katafute kazi, naona tabu zinatuzidi
Maisha yetu yakiwa hivi bila ya kibarua, tutazidi kuteseka x2
Ona hata hawa ndugu zetu hafiki kwetu
Kwa vile hatuna kitu, mume wangu eeeh!x2

Oooooh Katafute kazi kwa juhudi namaarifa eeh!
Yoooo! Mume wangu nakuambia
oooh Katafute kazi kwa juhudi na maarifa
Naona aibu watoto viraka vimejaa kama matangazo gazetini nawe kazi hunaa
Oooh katafute kazi kwa juhudi na maarifa
Naona aibu Kuvaa kauka nikuvae kwa jumbe kuna ngomaa, ngoma ya Msondo

Hayo ndiyo maneno yaliyomo kwenye wimbo huo ambao umejaa maneno ya hekima ya mwanamke kwenda kwa mumewe.Kutokana na ugumu wa maisha waliyonayo watanzania wengi, wimbo huo ulitokea kupendwa vilivyo.



Mwaka 2000 katika albamu ya Demokrasia ya Mapenzi mwanamuziki huyo alifunga kazi kwa kushindana na Moshi kwa kutunga nyimbo nne kati ya nyimbo 8 zilizomo katika albamu hiyo.



Miongoni mwa nyimbo alizotunga ni ule wimbo wa Chombo Kimeumbika,wimbo ambao ametumia tafsida ya hali ya juu, kwani unapousikiliza unadhani kuwa anazungumzia chombo cha majini, lakini ukweli ni kwamba anamzungumzia mwanamke.



Mwaka 2001 alifunga kazi katika albamu ya Rabana, ambapo alitunga nyimbo mbili ambazo zilikuwa kijembe kwa African Stars 'Twanga Pepeta', na ndiyo nyimbo zilizodhihirisha ubora wa Msondo mbele ya Twanga Pepeta.



Unajua nini?. Mara baada ya kuibuka kwa Tanga Pepeta mwishoni mwa miaka ya 1990, baadhi ya wadau na wanamuziki wa Twanga, walikuwa wanatangaza kuwa Twanga ndiyo bendi bora Tanzania na hakuna bendi ambayo inaweza kufanana ama kuishinda Twanga.



Maneno hayo yalitokana na ukweli kuwa Twanga ndiyo ilikuwa inaongoza kwa wanamuziki wake kuwa nadhifu na wenye kipato kikubwa. Lakini pia bendi hiyo ilikuwa inaongoza kwa kuwa na wapenzi wengie wanaohudhuria katika maonyesho yao na kiingilio chao kilikuwa juu ukilinganisha na Msondo. Kiingilio cha Twanga kilikuwa sh. 3000 huku Msondo ikiwa sh. 500.



Maneno hayo yaliwauma sana Msondo na waliamua kuwadhihirishia wadau wa muziki kama Msondo ni bendi kongwe na kamwe haina mpinzani katika suala zima la muziki. Muhidin Gurumo kiongozi wa Msondo alisema kuwa Twanga inaizidi Msondo katika promosheni kwani nyimbo zao zinapigwa na kutangazwa zaidi na vyombo vya habari, lakini kwenye suala la muziki, Msondo haina wa kufananishwa naye.

Katika kudhihirisha hilo, ndipo Kamanda Gurumo na jeshi lake walipoamua kukaa chini na kuandaa albamu hiyo ili kudhihirisha kile wanachosema. Mwanyiro alitunga nyimbo mbili maalumu za kuwapasha Twanga ambazo ni 'Chuma kikoli Moto' na Rabana.
Wimbo wa Chuma Chikoli Moto ambao maana yake ni chuma Kimapamba moto una maneno yafuatayo.

Usinichezee yaya, usicheze chuma cha moto
Usinichezee yaya usichezee chuma cha motK

Wameshindwa waganga na waganguzi
Sembuse wewe mwanakiwa
Jiepushe mama na Masimango
Nimevuka bara na nyika
Usinichezee yaya, usicheze chuma cha moto
Yeye yeye dadi, Chuma chikoli moto
Yeye yeye dadi Chuma chikoli moto
Usilete ujuaji utaumia bure
nimevuka maji ya shingo mgongo haukuloa,
wewe bwana mdogo umeipata hiyo,
Bwana mdogo utaumia bure.
Akaja kufunga kazi na wimbo wa Rabana ambao ndiyo uliobeba jina la albamu wenye maneno yafuatayo.
Rabana kaumba dunia aahaaahaa
Kaumba dunia lenye umbo la duara
na kujaza vitu vyoye vilivyomo ndani yake

Kaumba binadamu wa aina mbili jama, mwanamke na mwanaume
Kati yao katoa uwezo wa aina mbili, masikini na matajiri
Kaumba dunia yenye umbo la duara,
na kujaza vitu vyote vilivyomo ndani yake.
Kaumba binadamu wa aina mbili jama, mwanamke na mwanaume
Kati ya hao katoa uwezo wa aina mbili, masikini na matajiri
Kaumba dunia yenye umbo la duara,
na kujaza vitu vyote vilivyomo ndani yake.
Watoto hawa wanataka kuchezea anga hizi za wakubwa
Watoto hawa wanataka kuchezea anga hizi za wakubwa
aaaaaaaa

hayo yote ni mapenzi yake rabana
Wala siujanja, kwa wale walio matajiri
Na si ujinga kwa wale walio mafukara
Tuache kudharauliana kwa wenye kipato
Na wasiyo na kipato mtoa ni Rabana.

Ndani ya wimbo huu utasikia sauti za kina Gurumo na Tx Moshi zikiwaonya vijana na kuwaeleza hiyo ni Discipline kwa watoto ambao wanataka kuleta mzaha na bendi hiyo, na kuwambusha kuwa bendi hiyo iko tangu mwaka 1964 hadi sasa wapihe hesabu wenyewe.
Kama ilivyokuwa lengo lao, albamu hii yenye nyimbo kama Ndoa Ndoano, Arabia Fadhili, Isihaka Kibene na Lucy Bandawe, ilimaliza majigambo ya Twanga na kuufanya uuma kutambua kuwa Msondo ni Baba ya Muziki Tanzania.
Mwaka 2003 yeye na Bitchuka walipoihama Msondo na kwenda Sikinde, Msondo walitunga wimbo wa kuwapiga vijembe uitwao 'Mtoto Makutubu', ambao umo kwenye albamu ya Kilio cha Mtu Mzima ukiwa ni utunzi wake kiongozi wa Msondo, Said Mabela. Katika wimbo huo, mapera anamuonya Bitchuka kuacha kuisema Msondo kwa kuwa ni sawa na mzazi wake. Lakini pia wanawapiga vijembe Bitchuka na Mwanyiro kwa kibwagizo cha Mizigo. Mwanyiro alikaa chini na kujibu mapigo kwa kutunga wimbo wa Gere.

Kwa kuwa Mwanyiro si muimbaji, wapenzi wengi wanamzungumzia kama mpiga besi mahiri, lakini wamesahau kazi yake nyingine kuwa ni utunzi uliotukuka. Kama ingekuwa kwenye mchezo wa soka, tungesema kusema kuwa ni mfungaji wa mabao muhimu katika mechi muhimu.Huyo ndiyo suleiman Mwanyiro.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...