Na Thobias Mwanakatwe Kyela
SERIKALI imeendeleza utamaduni wa kutowalipa mishahara wafanyakazi 480 wa Mgodi wa Makaa ya Mawe Kiwira uliopo mkoani Mbeya kama ilivyokuwa ikifanya Kampuni ya Tan Power Resource iliyonyang’anywa kuundesha ambapo hadi sasa hawajalipwa miezi sita fedha zinazofikia zaidi ya Sh.Milioni 60.
Katibu wa Chama cha Wafanyakazi wa Migodini, Thomas Cheyo, akizungumza na Nipashe mjini Kyela juzi alisema tangu serikali itangaze kuurejesha serikalini mgodi huo mwezi Oktoba mwaka jana wafamyakazi hawajalipwa mishahara yao hadi sasa na hivyo kuendelea kukabiliwa na hali ngumu kimaisha.
Alisema kutokana na hali hiyo wafanyakazi wa mgodi huo wamedai hakuna manufaa yoyote wanayoyaona baada ya serikali kuuchukua mgodi huyo kwasababu imeiga tabia za kampuni ya Tanpower Resource Ltd ambayo ilikaa miezi 15 bila kuwalipa mishahara iliyofikia zaidi ya Sh.bilioni 1.8.
“Tangu mwezi Novemba mwaka jana baada ya serikali kutangaza kuuchukua mgodi huo na kutulipa malimbikizo ya mishahara ya miezi 15 yaliyolimbikizwa na kampuni ya Tanpower Resource Ltd zaidi ya Sh.bilioni 1.8 lakini cha kushangaza hatujalipwa tena hadi sasa na wafanyakazi wamerudi katika mateso ya tangu awali waliyokuwa wakiyapata kipindi mgodi upo chini ya mwekezaji,”alisema Cheyo.
Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, akizungumza na Nipashe kwa simu akiwa Dodoma alikiri serikali kutowalipa mishahara wafanyakazi wa mgodi huo na kwamba hata hivyo ipo katika mchakato wa kushughulikia malipo hayo.
“Ni kweli hatujawalipa mishahara wafanyakazi hao tangu kunzia mwezi Novemba mwaka jana lakini suala hili tunaendelea kulishughulikia kwa kushirikiana na Mbunge wa Kyela, Dk.Harrison Mwakyembe na bila shaka wiki hii suala hilo litakuwa limepatiwa ufumbuzi,”alisema Ngeleja ambaye hata hivyo hakuelezea sababu zilizosababisha kuchelewe kulipwa kwa mishahara hhiyo.
Azma ya serikali kutaka kurejesha mgodi wa Kiwira mikononi mwake, mara ya kwanza ilitangazwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda wakati wa mkutano wa 16 wa Bunge mwaka jana .
Alisema serikali itachukua hisa zote za Kiwira ili kuondoa lawama zinazomkabili kiongozi huyo wa serikali ya awamu ya tatu.
Awali mwezi Oktoba mwaka jana Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, alitangaza kuwa serikali inauchukua ramsi mgodi huo alipokutana na Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini katika ofisi ndogo ya Bunge jijini Dar es Salaam kutoa taarifa ya serikali kuhusu mgodi huo na kuahidi kulifanyia kazi wakati wa mkutano wa 16 wa Bunge mjini Dodoma.
“Kimsingi serikali imeshauchukua mgodi huo na inaumiliki kama tulivyoliahidi Bunge, kuanzia sasa ni mali ya serikali na hakuna mtu mwenye mkono pale,” alisema Waziri Ngeleja.
Alisema baada ya kuuchukua mgodi huo, hatua ambayo inafuata ni kuwalipa wafanyakazi wake ambao walikuwa wakifanya kazi kwa muda mrefu bila kulipwa kutokana na waliokuwa wamiliki kusimamisha uzalishaji.
“Tunawataka wafanyakazi wote wa Kiwira watuelewe kuwa tunaanza kuwalipa kuanzia wiki hii. Kabla ya Novemba mosi, mwaka huu/mwaka jana , wanatakiwa wawe wamelipwa fedha zao zote za malimbikizo,” alisema Waziri Ngeleja.
Alisema fedha zitakazolipwa kwa wafanyakazi hao ni mishahara ya miezi 15, ambayo ilikuwa haijalipwa kwa kipindi chote ambacho mgodi huo ulisimama.
Alipotakiwa kueleza kama waliokuwa wamiliki wa mgodi huo, wameshalipwa na wamelipwa kiasi, Waziri Yona alisema hilo litafahamika zaidi mjini Dodoma wakati atakapowasilisha ripoti yake katika mkutano wa 17 wa Bunge unaotarajiwa kuanza Oktoba 27.
Mgodi huo ulijengwa na Serikali ya China na kukabidhiwa kwa Serikali ya Tanzania kabla ya kuuzwa kwa wawekezaji wapya wa kampuni ya Tanpower Resource Machi 2007 ambapo yaliungana kuununua ambayo ni Choice Industries, ambayo wamiliki wake ni Joe Mbuna na Goodyeer Francis .
Kampuni nyingine ni Universal Technologies, ambayo inamilikiwa na Willfred Malekia na Evance Mapundi, wabia hawa ndio waliounda Kampuni ya Tanpower Resources Ltd iliyokuwa inamiliki mgodi huo uliouzwa kwa familia ya Rais Mstaafu Benjamin Mkapa na Waziri wa zamani waNishati na Madini Daniel Yona kwa bei ya kutupa ambapo mwaka jana ilitangaza kuinyanganya kampuni hiyo baada ya kushinda kuundesha.
MWISHO
Siasa za kyela balaa tupu,viongozi wanasusiana hadi misibani
Na Thobias Mwanakatwe, Kyela
HALI ya kisiasa katika Wilaya ya Kyela Mkoani Mbeya imefikia hatua mbaya kiasi cha kusababisha makundi mawili yanayorumbana kususiana misiba ambapo hilo limejidhihilisha wakati wa mazishi ya Mwenyekiti wa CCM wa wilaya hiyo, Jafeth Makasumi baada ya viongozi kadhaa wandamizi wa wilaya hiyo kushindwa kuhudhuria mazishi hayo.
Mazishi ya mwenyekiti huyo wa CCM Wilaya ya Kyela aliyefariki Mei 19 jijini Dar es Salaam yalifanyika Mei 21 mwaka huu katika kijiji cha Lubele kata ya Ikolo wilayani Kyela.
Viongozi wa wilaya ambao hawakuhudhuria mazishi hayo na kusababisha manung’uniko makubwa ya wananchi kutokana na kile kilichoelezwa kuwa Mwenyekiti huyo alikuwa kundi la Mbunge wa Kyela, Dk.Harrison Mwakyembe ambaye kipindi hiki amekuwa katika wakati mgumu kutokana na kundi la pili kumwandama ambalo hivi karibuni kupitia Kamati ya Siasa ya Wilaya lilifikia hatua ya kumwazimia apewe onyo.
Viongozi wa wilaya ya Kyela ambao hawakuhudhuria mazishi ya Mwenyekiti huyo wa wilaya ni pamoja na Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Kyela, Watson Majuni, Mwenyekiti wa Wazazi wilaya ya Kyela,Visk Mahenge ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Kyela mjini alikokuwa akiishi marehemu (Mwakasumi).
Wengine ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyela, Mhando Senyagwa,Mjumbe wa Kamati ya Tendaji ya UWT Mkoa ambaye pia ni Diwani wa Viti Maalum Kyela mjini, Zuhura Omari pamoja na madiwani kadhaa wa wilaya ya Kyela pia hawakuhudhuria mazishi hayo.
Hata hivyo viongozi hao baada ya kukacha kuhudhuria mazishi ya Mwenyekiti wao wa CCM walionekana wakihudhuria mkutano ulioitishwa na Waziri wa Viwanda ,Biashara na Masoko, Dk.Mary Nagu pamoja na kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC).
Baadhi ya wananchi waliohudhuria mazishi hayo walieleza kuwa pamoja na kwamba mikutano hiyo ilikuwa na umuhimu lakini viongozi hao walistahili kushiriki mazishi ya mwenyekiti wao na kuwatuma wasaidizi wao wawakilishe katika vikao hivyo.
Wananchi hao walisema kitendo cha viongozi hao kutoshiriki mazishi ya mwenyekiti huyo kimeonyesha dhahili kwamba walikuwa na chuki dhidi ya marehemu Mwakasumi hasa kutokana na kuwepo katika kundi linalomsabikia Dk.Mwakyembe.
“Kinachotushangaza mbona Mkuu wa Wilaya ya Kyela, Abdallah Kihato, alikwenda Mbeya kushiriki mkutano huo na akaomba ruhsa kwa wakubwa wake na kufanikiwa kuja kushiriki mazishi ya Mwenyekiti wa CCM, kwanini nao hawakufanya hivyo kama siyo chuki ya kisiasa,”alisema Mwakitalima Mwaifani wa mji wa Ipinda.
Waliongeza kuwa kama viongozi wa Chama cha Mapinduzi CCM mkoa na taifa hawatafanya jitihada za kumaliza mtafaruku wa kisiasa na makundi yanayoitafuna CCM Wilaya ya Kyela kuna hatari uchaguzi mkuu wa mwaka huu wilaya hiyo itaweza kutawaliwa na vurugu kubwa.
Katika mazishi hayo Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa, Deo Danga, alimwakilisha Rais Jakaya Kikwete ambapo alikabidhi rambirambi ya Sh. Milioni 2.5,Katibu wa CCM wa Mkoa,180,000 na Mbunge wa viti Maalum Mkoa, Frolence es Kyendesya aalitoa Sh.30,000
No comments:
Post a Comment