Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Saturday, July 17, 2010

JENGO LA MACHINGA COMPLEX LAANZA KAZI RASMI


UGAWAJI wa maeneo ndani ya Jengo la Machinga Complex umeanza leo ambapo wafanyabiashara 4,500 wanatakiwa kuingia ndani ya jengo hilo na leo wamekabidhiwa namba zao rasmi za usajili ndani ya jengo hilo.

Akizungumza na gazeti hili leo asubuhi, Mwenyekiti wa Chama Cha Wafanyabiashara Ndogondogo (ASBO), Dangama Dangama, amesema ugawaji wa maeneo umeanza leo kwa vyama vyote ambapo wasio na namba hizo hawaruhusiwi kuingia ndani ya jengo hilo.

Amesema kilichochelewesha kugawa maeneo ni kutokana na wahusika kutakiwa kupewa vitambulisho maalumu kwa ajili ya kazi hiyo.

“Walitakiwa wahusika wapewe vitambulisho lakini kutokana na wahusika wengi kuwa kwenye mkutano bungeni imeamriwa wapewe kadi za muda ili waanze kazi ndani ya jengo hilo,” amesema.

Dangama amesema Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, William Lukuvi, ametoa agizo la wafanyabiashara kuingia haraka ndani ya jengo hilo baada ya kuwapo kwa tatizo la ucheleweshaji wa vitambulisho.

“Mkuu wa Mkoa ametoa amri wafanyabiashara waingie ndani ya jengo huku maandalizi ya vitambulisho kutoka Halmashauri ya Jiji yakiendelea na ndio maana tumeamua kuwapa kadi na tayari baadhi ya wanachama wameonyesha maeneo yao,” amesema.

Amesema pamoja na ASBO kutarajia kuwaingiza wanachama 200, wafanyabiashara wengine wataingizwa kupitia vyama vya VIBINDO, TAMADA, UWAMADA, MUMADA ambavyo vimeteuliwa.

Wakati baadhi ya wamachinga wakifurahia kufunguliwa rasmi kwa jengo hilo wengine wamelalamikia kukosa nafasi katika jengo hilo licha ya kuwa wanachama wa kudumu na hai ndani ya vyama vilivyosajiliwa.

Ugawaji wa maeneo ndani ya jengo hilo umechukua muda mrefu na kuzua maswali mengi kutoka kwa wahusika jambo lililosababisha Mkuu wa Mkoa kuingilia kati, jengo hilo limejengwa kwa mkopo wa sh. bilioni 12 toka Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF).

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...