Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Wednesday, December 28, 2011

Hamad rashid agoma kuhojiwa na kamati ya mahadil cuf

Raymond Kaminyoge na Aziza Masoud

HALI bado tete ndani ya Chama Cha Wananchi (CUF) baada ya Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohamed, kugoma kuhojiwa na Kamati ya Nidhamu na Maadili ya chama hicho kuhusu tuhuma za kuvunja katiba. Mbunge huyo aliibua tuhuma nzito kwamba amekamata waraka wa siri wa viongozi wawili waandamizi wa chama hicho, waliokuwa wakipanga njama za kumfukuza.Hamad aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa ana sababu tano za kugomea kikao hicho, ambazo ni pamoja na waraka huo wa siri aliodai ulitoka kwa mmoja wa viongozi hao kwenda kwa mwenzake. Waraka huo ambao Hamad alidai kuunasa unasomeka, “Tuwe waangalifu tusiingie katika mtego” na uliandikwa Desemba 14 2011 na kutumwa kwa barua pepe.“ …anataka nifukuzwe kwenye chama, baadhi walioteua na walioteuliwa katika Kamati ya Nidhamu na Maadili wamekwishanituhumu hadharani na kunitia hatiani hivyo kikao hiki hakitatenda haki,” alisema Hamad.Alitaja sababu nyingine ya kukataa kuhojiwa kuwa ni kutoelezwa tuhuma zake hasa vifungu vya Katiba alivyodaiwa kuvikiuka. “ Ni vema nikaelezwa ni vifungu vipi vya katiba hiyo nilivyokwenda navyo kinyume,” alisema Hamad. Alifafanua kwamba, alitaka apewe hadidu za rejea za kikao kilichounda Kamati ya Nidhamu na Maadili kwa sababu kikatiba, hakuna chombo kama hicho.“Katiba ya CUF haina chombo kama hicho, kamati hii imeundwa na nani nikipewa hadidu za rejea za kikao kilichounda kamati hiyo zitanisaidia katika kumbukumbu,” alisema Hamad Rashid. Alisema alitaka pia apewe nakala ya uteuzi wa wajumbe walioteuliwa katika kamati hiyo.Mbunge huyo pia alisema amegomea kikao hicho hadi atakapopewa kanuni zitakazotumika katika kuendesha shughuli nzima ya kujibu tuhuma hizo na kupewa katiba iliyotumika ambayo ameivunja. “Nataka kupewa vitu hivyo ili niweze kuweka kumbukumbu sahihi kwa kila hatua inayochukuliwa na chama,” alisema mbunge huyo wa CUF.Akizungumzia kamati hiyo, mbunge huyo alisema kati ya wajumbe wanane, watano hana imani nao kwa sababu wamekuwa wakimtuhumu hadharani. “Hawa wajumbe sina imani nao uamuzi wao hautakuwa wa haki,” alisema Hamad. Juzi Hamad Rashid na wenzake 13 waliitwa na Kamati na Nidhamu ili kujibu tuhuma za kuvunja Katiba ya chama hicho. Hatua hiyo imekuja baada ya mvutano wa muda mrefu kati ya Katibu Mkuu na Mbunge huyo kutuhumiana hadharani.Waraka wa Siri

Hamad alisema hawezi kuhudhuria kikao hicho kwa kuwa tayari amebaini njama za kushughulikiwa zilizosukwa na vigogo wawili wa chama hicho dhidi yake.“ Nimeshauriana na Makamu na tumeona kuna haja ya jamaa yako (Rashid) na genge lake kuitwa katika Kamati ya Nidhamu na Maadili kuhojiwa,” inasema sehemu ya waraka huo ambao aliusambaza kwa vyombo vya habari.Waraka huo uliongeza, “ushahidi wa kutosha umekusanywa dhidi yake na wasaidizi wake wakuu na muono wetu ni kuwa tumfukuze uanachama.” Waraka huo ulisisitiza, “Wanachama walio wengi wanatudadisi kwa nini hatuchukui hatua, akishajulikana kuwa si mwanachama atakuwa hana mashiko muache aende CCM au Chadema.” Alipoulizwa Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili na Nidhamu wa CUF, Abdul Kambaya alisema taarifa za Rashid kukataa kuhojiwa na Kamati zitapelekwa katika Kamati ya Utendaji.“ Ni kweli Hamad amegoma kuhojiwa kuhusu tuhuma zinazomkabili, lakini tunachofanya ni kupeleka taarifa kwa kamati ya Utendaji itakayofanya maamuzi,”alisema Kambaya na kubainisha kuwa kamati hiyo inaendelea kuwahoji wanachama wengine wanaotuhumiwa kuvunja katiba ya chama hicho.Hivi karibuni Hamad Rashid alijikuta kwenye mgogoro na baadhi ya viongozi wa makao makuu ya chama hicho, baada ya kutangaza dhamira hiyo yake ya kugombea nafasi ya katiba mkuu mwaka 2014. Kuanzia hapo akajikuta ameingia kwenye mgogoro na chama hicho kiasi cha kunusurika kushambuliwa na watu wasiojulikana wakati akigawa misaada katika matawi ya chama hicho, kata ya Manzese. Mvutano huo ulisababisha vurugu katika tawi la Chechnya ambako wanachama wanaomuunga mkono walipambana na walinzi wa Blue Guard na kusababisha umwagaji damu.www.mwananchi.co.tz

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...