Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Wednesday, June 26, 2013

FAMILIA YA MATUMLA YALALAMIKIA UMASKINIBondia Rashid Matumla alipotwaa ubingwa wa dunia wa WBU
Bondia Mbwana Matumla enzi zake alipokuwa akitamba katika ndondi za kulipwa
Bondia Hassan Matumla (kulia) alipokuwa akipigana masumbwi ya kulipwa

UNAPOZUNGUMZIA ngumi za kulipwa ama za ridhaa hapa nchini, si rahisi kuacha kulitaja jina ama ukoo wa Matumla. Ni familia ya mabondia walioweza kulitangaza vyema jina la Tanzania kimataifa tangu walipokuwa wakipigana ndondi za ridhaa hadi walipohamia kwenye ndondi za kulipwa.
Ni familia ya mzee Ally Matumla, inayoundwa na watoto zaidi ya 10, wakiwemo wawili wa kike, lakini ni wachache walioweza kuchomoza vyema katika mchezo huo, wakifuata nyayo za kaka yao, Rashid Matumla na Ally Matumla, ambaye kwa sasa ni marehemu.
Watoto wengine wa mzee Matumla walioweza kulitangaza vyema jina la Tanzania kimataifa kupitia ndondi za ridhaa za kulipwa ni Mbwana, Haji, Karim, Hassan, Mkwanda.
Hata hivyo, mtoto pekee aliyeweza kulitangaza vyema jina la familia hiyo ni Rashid, ambaye baada ya kung'ara kwenye ndondi za ridhaa miaka ya 1980, ikiwa ni pamoja na kutwaa ubingwa wa Afrika Mashariki na kushiriki Michezo ya Jumuia ya Madola na Michezo ya Olimpiki, aliamua kuhamia kwenye masumbwi ya kulipwa.
Ni katika ngumi hizo, ndipo Rashid alipoweza kuonyesha umahiri wake kwa kutwaa ubingwa wa Afrika, mabara, mkanda wa kimataifa na wa dunia, yote yakiwa chini ya WBU. Katika kipindi chote hicho, Rashid alikuwa akipigana chini ya udhamini wa Kampuni ya DJB Promotions, inayomilikiwa na Jamal Malinzi.
Licha ya kutangaza mara kwa mara kwamba atastaafu mchezo huo, Rashid bado anaendelea kuzipiga katika mapambano ya kulipwa na mara ya mwisho alidundwa kwa pointi na mpinzani wake wa jadi, Maneno Osward 'Mtambo wa Gongo'.
Kinachomfanya Rashid ashindwe kustaafu mchezo huo ni kuwepo kwenye damu yake. Anasema kila mara anajisikia hamu ya kupigana, si tu kutokana na mapenzi yake kwa mchezo huo, bali pia kujipatia riziki ya kuendesha maisha yake ya kila siku.
Kwa upande wake, Hassan ameshastaafu mchezo huo baada ya kuvunjika kidole cha mkono wake wa kushoto. Mbwana bado anaendelea kupigana, lakini si kwa kiwango alichokuwa nacho zamani, ambacho kilimvutia kocha Nolman Hlabane wa Afrika Kusini, aliyeamua kumchukua na kumtafutia promota nchini humo.
Mkwanda kwa sasa anaishi Sweden, ambako bado anaendelea kucheza ngumi za kulipwa wakati Karim aliamua kuzamia nchini Australia miaka kadhaa iliyopita alipokwenda huko kushiriki Michezo ya Jumuia ya Madola. Tayari Karim ameshacheza mapambano matatu ya kulipwa na kushinda yote.
Licha ya kushiriki katika ndondi hizo kwa miaka mingi, Rashid, Hassan na Mbwana wamekiri kuwa, hawana lolote la maana la kujivunia katika maisha yao zaidi ya kuambulia sifa kutokana na kufanya vizuri katika mashindano ya kimataifa.
Wanafamilia hao watatu wa ukoo wa Matumla, walisema hayo wiki iliyopita walipokuwa wakihojiwa katika kipindi cha Mkasi kilichorushwa hewani na kituo cha televisheni cha Channel Five.
"Kama familia yetu ingekuwa inaishi Marekani, nadhani tungekuwa matajiri sana,"alisema Rashid wakati wa mahojiano hayo.
"Familia yetu ni maarufu kwa mchezo wa ngumi, lakini ni maskini. Maisha tunayoishi, siyo yale tuliyopaswa kuishi," aliongeza bondia huyo, ambaye aliwahi kupigana nchini Hungary na Italia na kuwadunda mabondia kadhaa wa nchi hizo katika mapambano ya uzani wa middle.
Pamoja na kutopata mafanikio makubwa kimaisha kutokana na mchezo wa ndondi, Hassan alisema lengo lao kubwa ni kuupromoti mchezo huo kwa lengo la kuibua vipaji vya mabondia chipukizi na kuwaendeleza.
Kwa mujibu wa Hassan, tayari wameshaanza kusaka ufadhili kwa ajili ya kutimiza lengo lao hilo na kuongeza kuwa, wanatarajia kuianza kazi hiyo hivi karibuni.
Hassan alisema kukosekana kwa ufadhili ndiko kunakosababisha bondia kama vile Francis Cheka, ambaye amekuwa akifanya vizuri hapa nchini, kushindwa kwenda nje kuwania mikanda ya kimataifa, kama ilivyokuwa kwa Rashid, alipokuwa chini ya DJB Promotions.
Alisema Cheka ni bondia mzuri, lakini uzuri wake umekuwa ukiishia ndani ya mipaka ya Tanzania bila ya kupata nafasi ya kuonyesha uwezo wake kimataifa. Alisema ana hakika iwapo Cheka angepata udhamini wa uhakika, angeweza kutwaa ubingwa wa dunia.
Cheka ndiye bondia pekee nchini aliyewahi kuwadunda mabondia kutoka familia ya Matumla. Alianza kuonyesha umwamba wake kwa Rashid kabla ya kumdunda Hassan. Hakuna bondia wa familia hiyo aliyeweza kumdunda Cheka.
Kwa upande wake, Mbwana aliitaja faida pekee, ambayo familia yao wameweza kuipata kuwa ni kuajiriwa ndani ya vyombo vya ulinzi na usalama kupitia mchezo wa ndondi. Wapo walioajiriwa katika Jeshi la Polisi na wengine Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).
"Tuliweza kupata ajira kirahisi kwenye vyombo vya usalama kwa sababu ndiko kulikokuwa rahisi kuajiriwa kupitia michezo. Karibu sisi sote tulikuwa askari,"alisema Mbwana.
Akizungumzia udhamini wa ndondi za kulipwa ulivyokuwa enzi zake, Rashid alisema ulikuwa mzuri na wa uhakika na kuongeza kuwa, hakuwahi kusumbuliwa ama kudhulumiwa haki zake na mapromota.
Alimtaja promota Phillemon Kyando 'Don King' kuwa ndiye aliyemwingiza kwenye ndondi za kulipwa na kumsaidia mambo mengi kabla ya kuchukuliwa na Malinzi, ambaye alimwendeleza zaidi kwa kumwandalia mapambano ya kimataifa.
"Kusema ule ukweli, tangu nilipoanza kupigana ndondi za kulipwa, sijawahi kugombana na promota yeyote. Walikuwa wakinitimizia na kunipatia kila nilichokuwa nikikihitaji,"alisema Rashid.
Alipoulizwa sababu ya Tanzania kufanya vibaya katika mashindano ya kimataifa ya ndondi za ridhaa, Rashid alisema ni kutokana na maandalizi duni na ya zimamoto.
Rashid alisema mara nyingi mabondia wa Tanzania wanaoshiriki kwenye mashindano ya kimataifa wamekuwa wakipelekwa kambini miezi michache kabla ya kwenda kushindana na hivyo kukosa uzoefu wa kutosha.
Alisema ni vigumu kwa bondia anayekwenda kushindana katika Michezo ya Olimpiki na Jumuia ya Madola kuweza kufanya vizuri iwapo hatapata maandalizi ya kutosha na ya muda mrefu.
Rashid kwa sasa anao watoto wanne, mmoja akiwa amerithi kipaji chake. Mtoto wake huyo wa kwanza anajulikana kwa jina la Mohamed na hivi karibuni alimdunda mtoto wa Cheka, Cosmas Cheka kwa pointi walipozipiga mjini Morogoro, ikiwa ni kulipiza kisasi cha vipigo walivyopata baba zake, Rashid na Hassan.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...