Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Friday, June 21, 2013

Uhuru Seleman athibitishia kutua Coastal Union
KIUNGO mchezeshaji wa aliyekuwa akiichezea Azam kwa mkopo kutoka Simba, Uhuru Seleman ametua Coastal Union ya Tanga pia kwa mkopo kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Uhuru aliithibitishia MICHARAZO kwamba ametua Coastal kwa ajili ya ligi ijayo na kwamba anajifua vilivyo ili kuwapa raha mashabiki wa klabu hiyo aliyowahi kuichezea msimu wa 2007-2008 na kufikia kuzigombanisha Simba na Coastal wakimgombea kila mmoja alipodai ni mchezaji wake.
Kiungo huyo ambaye amewahi pia kutamba na Mtibwa Sugar, alisema amefurahi kutua Coastal kwa kuamini atapata nafasi nzuri ya kuonyesha kipaji chake baada ya kushindwa kupata fursa hiyo ndani ya Simba na hata Azam walipomchukua msimu uliopita.
"Ni kweli nimetua Coastal kwa mkopo na najiandaa kuichezea kwa msimu ujao, nimefurahi kwa sababu naamini nitarejesha makali yangu," alisema Uhuru.
Uongozi wa Coastal kupitia Mkurugenzi wake wa Ufundi, Nassor Binslum amethibitisha suala la kumnyakua kiungo huyo akidai wamezungumza na Simba ili wamchukue kwa mkopo na watasaidiana nao kulipa mshahara wa mchezaji huyo wakati akiichezea timu yao ambayo ilimaliza msimu wa ligi iliyopita katika nafasi ya 6.
Mabingwa hao wa zamani wa kandanda nchini mbali na kumnyakua Uhuru pia imewanasa wachezaji wengine wapya katika kukiimarisha kikosi chao baadhi yao ni beki Juma Nyosso na Haruna Moshi (wote Simba), Kenneth Masumbuko toka Polisi-Moro, Marcus Ndeheli na Said Lubawa (JKT Oljoro) na Abdallah Ally kutoka visiwani Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...