Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Thursday, June 20, 2013

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akagua ujenzi wa barabara ya Cheju - Jendele - Kaebona


  Msimamizi wa Mradi wa Bara bara tatu za Vijijini za Unguja kutoka Wizara ya Miundo Mbinu na Mawasiliano Mhandisi Suleiman Abdulla Ali akimpatia maelezo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliyetembelea mradi huo katika Bara  bara ya Cheju – Jendele – Kaebeona.Kati kati yao aliyevaa kofia ya Kiua ni Waziri wa Wizara hiyo Rasdhid Seif na pembeni ya Mhandisi Suleiman ni Mshauri Muelekezi waMradi huo Kutoka Kampuni ya Newtech Consulting Group ya Nchini Sudan El- Tayeb Rabah Mohammed
Mshauri Muelekezi wa Mradi huo Kutoka Kampuni ya Newtech Consulting Group ya Nchini Sudan El- Tayeb Rabah Mohammed akimuhakikishia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif  ujenzi wa bara bara zenye kiwango katika mradi wa bara bara tatu za Vijiji za Unguja huko Cheju Wilaya ya Kati, Mkoa Kusini Unguja.Picha na Hassan Issa-Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar
--
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amewaagiza wataalamu wanaopata fursa za Ujenzi wa Bara Bara Nchini kuhakikisha kwamba bara bara wanazozijenga zinakuwa katika kiwango kinachokubakila Kimataifa ili ziwe na uwezo wa kudumu kwa kipindi kirefu.
Agizo hilo amelitoa wakati wa ziara fupi ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Bara bara ya Jendele-Cheju hadi Kaibona yenye urefu wa Kilo mita 11.741  ambayo ni miongoni mwa bara bara iliyomo  ndani ya mradi wa ujenzi wa bara bara tatu za vijijini katika Kisiwa cha Unguja.
Balozi Seif alisema wapo baadhi ya wahandisi wa ujenzi wa Bara bara wasio waaminifu ambao baadhi ya wakati hudiriki kuondoa njiani miradi ya ujenzi wa bara bara wanayopewa bila ya kuzingatia masharti na mikataba waliyoiridhia.
Alisema hali hiyo huleta kero kwa wafadhi wa miradi hiyo na mara nyingi kuyatia hasara Mataifa yenye miradi hiyo ambayo mengine yanashindwa kuihudumia Miradi husika kutokana na ufinyu wa uchumi wao.
“Baadhi ya  Makandarasi wamekuwa na tabia ya kuondosha njiani kazi wanazopewa za ujenzi tabia ambayo huwakera wafadhili wa miradi hiyo na kwa upande mwengine kuyaongezea mzigo Mataifa  yenye kusaidiwa ufadhili wa miradi hiyo “. Alisisitiza Balozi Seif.
Akizungumzia suala la fidia ya vipando, mali pamoja na majengo ya wananchi wanaoathirika na miradi hiyo Balozi Seif aliiagiza Wizara ya Miundo Mbinu na Mawasiliano Zanzibar kuwa makini ya baadhi ya watu wajanja wenye tabia ya kujipandikiza katika madai ya fidia hizo.
Alisema tabia hiyo ambayo hujichomoza mara kwa mara wakati wa uanzishwaji wa miradi tofauti katika maeneo mbali mbali Nchini imekuwa ikiitia hasara kubwa Serikali kwa vile haimo ndani ya jabeti iliyokubalika kwa pande zote mbili.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliipongeza Kampuni ya ujenzi wa Bara bara hiyo ya D.P Shapriya +Co. Ltd ya Dara es salaam kwa hatua iliyofikia ya ujenzi wa mradi huo licha ya kuchelewa kidogo kutokana na msimu wa mvua za masika.
Mapema Msimamizi wa Mradi huo wa Bara bara tatu za Vijijini Unguja kutoka Wizara ya Miundo Mbinu na Mawasiliano Zanzibar Mhandisi Suleiman Abdulla Ali alisema Serikali kupitia Wizara husika tayari imeshawalipa fidia wananchi wote waliohusika na ile bara bara ya Jendele- Cheju- hadi Kaebona.
Mhandisi Suleiman alimueleza Balozi Seif kwamba tathmini ya fidia imeshafanywa pia kwa bara bara ya Koani – Jumbi yenye urefu wa Kilo Mita 6.3 kwa kushirikiana na masheha wa shehia zinazopita bara bara hiyo na Wizara husika italipa fidia mara tuu fedha zitakapopatikana.
Alifahamisha kwamba ufinyu wa bajeti ya kazi za ujenzi wa Bara bara hizo za Vijijini Unguja umepelekea kutolewa kwenye mradi huo kwa Bara bara ya Kizimbani – Kiboje yenye kilo mita 7.
Msimamizi huyo wa mradi wa ujenzi wa bara bara hizo alieleza kuwa ujenzi wa kazi hiyo ulioanza mapema mwezi Januari mwaka huu wa 2013 umegharamiwa na Benki ya Maendeleo ya Kiislamu { Badea } kwa kushirikiana na SMZ  kwa kiasi cha  Shilingi za Kitanzania Bilioni 14,834,615,889.06/-.
Akitoa maelezo Mshauri muelekezi wa Mradi huo kutoka kampuni ya Newtech Consulting Group ya Nchini Sudan El-Tayeb Rabah Mohammed alisema kuwa mradi huo umepangwa kuchukuwa takriban miezi 17  hadi kukamilika kwake mwezi Mei mwaka ujao.
El – Tayeb alimuhakikishia Makamau wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kwamba ana matumaini makubwa ya kupatikana kwa kiwango kizuri cha ujenzi kitakachokidhi mahitaji yaliyokusidiwa kwa pande zote mbili.
Alieleza kuwa Wataalamu hao wa ujenzi wameshasafisha eneo la wastani wa Kilo mita 10 na kufanya kazi za kutengeneza Tabaka la Chini kwa wastani wa Kilo mita mbili kwa Bara bara ya Cheju –Jendele – Kaebona.
Wizara ya Miundo Mbinu na Mawasiliano Zanzibar ilitilianasaini Mkataba na Kampuni ya DP Shapriya + Co Ltd ya Dar es salaam kwa kazi za utekelezaji wa ujenzi wa Bara bara tatu za Vijijini Unguja mnamo tarehe 11 Septemba mwaka 2012.
Kukamilika kwa bara bara hizo  na hasa ile ya Cheju-Jendele- Kaebona kwa kiasi kikubwa itawaondoshea usumbufu wakulima wa zao la mpunga ambao walikuwa wakipata usumbufu kwa miaka kadhaa sasa
 Na 
Othman Khamis Ame,
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...