Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Wednesday, December 26, 2012

KLABU YA SIMBA YASIKITISHWA NA KIFO MWAIMU


KLABU ya soka ya Simba imepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Katibu Mwenezi wake wa zamani, Robert Charles Sechawawa Mwaimu, kilichotokea juzi Jumanne nyumbani kwake Oysterbay jijini Dar es Salaam.

Makamu Mwenyekiti wa SIMBA, Geofrey Nyange Kaburu, kwa niaba ya uongozi wa Simba amesema msiba huo umeleta pengo kubwa kwa klabu kwani mchango wa Mwaimu ulikuwa bado unahitajika kutokana na uzoefu wake mkubwa katika medani ya soka na michezo kwa ujumla.

"Kwa kweli Simba imepata pengo kubwa sana kutokana na msiba huu wa Mwaimu. Pamoja na kwamba hakuwa kiongozi wa Simba kwa muda mrefu sasa, lakini bado alikuwa akijitahidi kutoa mchango wake wa hali na mali kila ambapo ilihitajika. Msiba huu umemgusa kila ambaye anaitakia mema Simba," alisema.

Mwaimu alikuwa Katibu Mwenezi wa Simba mwishoni mwa miaka ya 1990 wakati Simba ikiwa chini ya uenyekiti wa Yusuf Hazali na Katibu Mkuu akiwa Halfani Mazi Matumla.

Zaidi ya Simba SC, Mwaimu alipata kuwa mfanyakazi katika Mamlaka ya Bandari Tanzania, Mamlaka ya Mkonge Tanzania kabla ya kwenda Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) alikokuwa akifanya kazi hadi wakati anaanza kuwa Katibu Mwenezi wa Simba.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka katika familia ya Mwaimu, marehemu atazikwa kesho Ijumaa katika makaburi ya Kinondoni jijini Dar es Salaam majira ya saa 9:30 alasiri.

Shughuli zote za ibada ya mazishi zitafanyika nyumbani kwa marehemu, Kenyatta Drive Namba 22, Oysterbay kuanzia saa tano asubuhi.

Kaburu amewaomba wana Simba kushiriki kwa nguvu katika mazishi ya marehemu ikizingatiwa kwamba kesho itakuwa siku ya mapumziko kwa sababu ya Sikukuu ya Iddi.

Mola na ailaze roho ya marehemu mahali pema. Amina

Imetolewa na

Ezekiel Kamwaga
Ofisa Habari
Simba SC

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...