Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Friday, March 29, 2013

CRDB CHINA DESK YAZINDULIWA


 Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Dk.Charles Kimei (kushoto), Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji na Uwezeshaji, Dk. Mary Nagu na  Balozi wa China hapa nchini, Lü Youqing wakiwasili katika hoteli ya Serena.
 Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Dk.Charles Kimei akitoa hotuba yake wakati wa uzinduzi huo.
 Balozi wa China hapa nchini, Lü Youqing akitoa hotuba yake.

 Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji na Uwezeshaji, Dk. Mary Nagu akizungumza katika hafla hiyo.
Baadhi ya wageni waalikwa.


DAR ES SALAAM, Tanzania

MKURUGENZI Mtendaji wa Benki ya CRDB, Dk.Charles Kimei, amewataka wajasiriamali na wawekezaji wanaofanya biashara zao kati ya Tanzania na China, kuchangamkia fursa pana ya ukuzaji mitaji yao na pato kwa kutumia huduma mpya ya CRDB China Desk.

Dk Kimei aliyasema hayo jana wakati wa hafla ya uzinduzi wa China Desk, inayotolewa na CRDB, itakayo wahudumia wafanyabiashara, wajasiriamali na wawekezaji wanaofanyakazi zao baina ya mataifa hayo rafiki.
“China Desk, ni huduma yenye fursa inayoweza sio tu kusaidia kukuza mitaji na kutanua wigo wa maendeleo, bali kudumisha ushirikiano wa kiuchumi na maendeleo baina ya China na Tanzania, ambao uliasisiwa karibia nusu karne iliyopita,” alisema Dk Kimei katika hafla hiyo.

Aidha, akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika kwenye Hoteli ya Serena jijini, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji na Uwezeshaji, Dk. Mary Nagu, aliiomba CRDB kuboresha utoaji wa mikopo ya riba nafuu kwa wajasiriamali wadogo na wa kati, ili kuharakisha ukuaji wa pato la Mtanzania na Taifa kwa ujumla.

Dk Nagu alibainisha kuwa, taasisi za kipesa nchini zina mchango mkubwa kuwawezesha wajasiriamali wadogo na wa kati kukuza pato lao, kama zitakuwa tayari kuwapa mikopo yenye masharti nafuu na riba ndogo, ili kusaidia harakati zao za kujikwamua na kukuza uchumi wa taifa.

“CRDB mnastahili pongezi kwa huduma hii, inayokuja wakati ambao Tanzania kama Taifa, lilimpokea rais mpya wa China, Xi Jinping katika ziara ya kikazi. Taasisi nyingine za kifedha zitambue umuhimu wa ushirikiano baina ya mataifa haya na kubuni huduma kama hizi,” alisema Dk Nagu.

Aliongeza kwamba, kwa kuwa harakati za kumkomboa Mtanzania zimeshika kasi, huku China ikijitoa kadri iwezavyo kuisaidia Tanzania, kuna haja huduma kama hizo za China Desk zikaambatana na mikakati endelevu ya kimandeleo, na taasisi nyingine nazo zinastahili kuiga.

Kwa upande wake, Balozi wa China hapa nchini, Lü Youqing, aliipongeza CRDB kwa kufuata nyayo za waasisi wa China na Tanzania, kiasi cha kubuni na kuzindua China Desk – dawati litakalowanufaisha wajasiriamali na wafanyabiara wa kila upande.

“Huduma hii ni harakati chanya inayofuata nyayo za waasisi wa ushirikiano baina ya China, Rais Mao Tse Tung na Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere. Vizazi na vizazi vitabaki kujivunia na kila mmoja atajisikia yu nyumbani anapokuwa katika moja ya nchi hizo,” alisisitiza Youqing.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...