Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Friday, October 25, 2013

MJENGWABLOG INAWAKARIBISHA WAHARIRI MKOANI KWETU IRINGA


Ndugu zangu,
Kwa niaba ya Wana-Iringa na hususan wadau wa habari wa mkoani Iringa, Mtandao wa KwanzaJamii.com na Mjengwablog. com unachukua fursa hii kuwakaribisha mkoani kwetu Iringa, wahariri wanachama wa Jukwaa la Wahariri hapa nchini.

Ni heshima kubwa kwetu Wana-Iringa kwa Jukwaa la Wahariri kuichagua Iringa kama mahali pa kufanyia Mkutano wao Mkuu wa Mwaka.

Ni faraja pia, tukikumbuka tukio la kuawa kwa ndugu yetu na mwanahabari mwenzetu Daud Mwangosi mwaka mmoja uliopita. Tukikumbuka pia tukio la miezi ya karibuni la kujeruhiwa vibaya kwa mwanahabari na mhariri wa miaka mingi hapa nchini, Absalom Kibanda.

Ni jambo la kutia matumaini pia, kuwa moja ya ajenda za Mkutano huo wa Wahariri unaoanza leo Ijumaa na kumalizika kesho Jumamosi ni kujadili masuala ya Usalama wa Wanahabari.

Ni matumaini yetu, kuwa Wahariri kupitia Mkutano wao huu wa Iringa , na wakiwa Iringa yenye hali ya hewa nzuri, Iringa yenye amani, utulivu na isiyo na hata foleni za barabarani.

Naam, wakiwa mbali sana na news rooms zao, Wahariri hao watapata fursa ya kujadiliana kwa kina na hatimaye kutoka na ' Azimio La Iringa' lenye maslahi kwa tasnia ya habari nchini na jamii kwa ujumla.
Na huko mitaani Iringa wahariri muwachangie Wana-Iringa kwa kununua bidhaa zinazotengenezwa Iringa. Msisahau pia kula vyakula vyetu vya Iringa ikiwamo na vinywaji pia.

Si mnajua, Iringa tuna maji ya chemchem kama vile Maji Afrika, ya Mufindi, Image na yale yanayotirika kutoka kwenye miti...! Tuna pia bidhaa bora zitokanazo na maziwa ya ng'ombe wafugwao hapa Iringa. Hii ni pamoja na jibini na maziwa bora na maarufu nchini yenye chapa ya 'Asas Milk'.

Na kwenye mechi yenu ya kesho dhidi ya wanahabari wa Iringa matokeo hayahitaji utabiri wa Sheikh Yahya. Kwa vile kuna ng'ombe anashindaniwa, basi, ndugu zangu Wahariri mtambue, kuwa, kwa Mnyalukolo, kwenye kugombania nyama, hakubali matokeo mengine isipokuwa ushindi tu..!

KwanzaJamii.com na Mjengwablog inawatakia ukazi mwema mkiwa Iringa.

Maggid Mjengwa.
Mwenyekiti Mtendaji.
IkoloMedia.
Iringa.
0754 678 252

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...