Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Thursday, March 10, 2011

MAKAMU MWENYEKITI WA KLABU YA YANGA AJIUZULU RASMI


ALIYEKUWA MAKAMU MWENYEKITI YANGA, DAVIS MOSHA
MAKAMU Mwenyekiti wa Yanga, Davis Mosha ameamua kubwaga manyanga katika nafasi hiyo kwa kile alichosema kuwapisha wengine wenye uwezo kuongoza klabu hiyo, kwani kuwepo kwake madarakani kumekuwa kikwazo kwa wengine kutimiza malengo yao.
Mosha aliyeingia madarakani kupitia uchaguzi mkuu wa klabu hiyo wa Julai 18, mwaka jana, tayari amekabidhi barua ya kujiuzulu kwa Mwenyekiti wake Lloyd Nchunga tangu juzi kwa kile alichosema kulinda hadhi na heshima yake ndani ya klabu hiyo na jamii.
Akithibitisha kujiuzulu kwake jana kwa njia ya simu, Mosha alisema ni kweli amefanya hivyo kwa hiari yake baada ya kushauriana kwa kirefu na familia yake pamoja na jamaa zake wa karibu, kwa lengo la kulinda heshima na hadhi yake ndani ya Yanga na jamii.
Mosha alisema kwa vile amekuwa na mapenzi ya dhati na klabu yake, ameamua kubaki kuwa mwanachama mwaminifu, akimini viongozi wenzake waliobaki chini ya Mwenyekiti Nchunga, watailetea Yanga mafanikio ya kiuchumi na kisoka yaliyotarajiwa.
“Ndiyo, nimeamua kujiweka kando kwenye uongozi, na tayari nimeshamwandikia barua mwenyekiti kuhusu uamuzi wangu, unaotokana na kuchoshwa visa na vitimbi ambavyo vimekuwa vikizushwa kila kukicha, kama binadamu nimefika mahala nimeona yanini? Heri nijiondoe kwenye uongozi,” alisema Mosha na kuongeza:
“Pamoja na kujiondoa kwenye uongozi, nawaahidi wanachama wa Yanga nitabaki kuwa Mwanayanga mwaminifu kwani kujiweka kwangu kando ni kulinda hadhi na heshima yangu katika jamii na kufanya shughuli zangu kwa uhuru na amani.”
Kwa muda mrefu ndani ya Yanga kumekuwa na msigano wa kifikra ndani ya uongozi wa klabu hiyo kati ya Mosha na Mwenyekiti wake Nchunga kwa upande mmoja na aliyekuwa mfadhili na Mjumbe wa Bodi ya Udhamini wa klabu hiyo, Yusuf Manji kwa upande mwingine.
Nchunga amekuwa akionekana kukosa ujasiri katika uongozi wake na kujikuta akitimiza matakwa ya Manji pasipo ridhaa ya Kamati ya Utendaji kwa mfano uteuzi wa Francis Kifukwe kupewa jukumu la kufufua mfumo wa kampuni suala ambalo liliteta mvutano ndani ya kamati ya utendaji.
Suala jingine ambalo Nchunga alipitisha bila Kamati ya Utendaji kujua, ni uteuzi wa Mbunge wa Temeke, Abbas Mtemvu kuwa Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini kwa lengo la kushirikiana na Manji, Kifukwe na Mama Fatma Karume.
Kwa upande wa Manji, Mosha alionekana kuwa na msimamo katika kupigania hadhi na heshima ya uongozi uliopo maradakani kwa mujibu wa katiba, kwamba pamoja na umuhimu wa Manji ndani ya klabu hiyo, kila mmoja anapaswa kutimiza wajibu wake kulingana na mipaka.
Akielezea kiini cha kuachia ngazi, Mosha alisema ni hatua ya baadhi wasiopenda msimamo wake ndani ya klabu hiyo, kufikia hatua ya kuwatuma mashabiki kumfanyia fujo akirejea tukio la gari yake kushambuliwa alipokwenda kuokoa gari ya wachezaji kutopigwa mawe baada ya Yanga kuchapwa bao 1-0 na Mtibwa, Uwanja wa Uhuru, Februari 2, mwaka huu.
Alisema, kibaya zaidi ni kuona baada ya tukio lile, bado kumekuwa na mipango ya kutaka kumfanyia fujo tena kwa lengo la kumdhalilisha, hivyo hana sababu ya kubaki katika nafasi hiyo ya uongozi isipokuwa kubaki kuwa mwanachama mwaminifu wa klabu hiyo.
Juhudi za kumpata Nchunga kuthibitisha kama amepata barua ya kujiuzulu kwa Mosha, ziligonga mwamba kutokana na simu yake kuita bila majibu.

kwa habari zaidi tembelea http://mamapipiro.blogspot.com/

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...