Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Tuesday, March 22, 2011

TUZO ZA MUZIKI ZA KILI KUFANYIKA JUMAMOSI


Maandalizi kwa ajili ya onyesho la Tuzo za Muziki za Kili yamekamilika ambapo waandaaji wa Tuzo hizo, Kampuni ya Bia Tanzania TBL, kupitia kinywaji chake cha bia ya Kilimanjaro Premium Lager wametangaza wasanii watakaotoa burudani katika onyesho la utoaji wa Tuzo hizo litakalofanyika Jumamosi ya Tarehe 26, Machi 2011 katika Ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam kuanzia saa moja jioni.

Mkurugenzi wa Masoko wa Kampuni ya Bia Tanzania TBL, David Minja aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana ya kuwa Utoaji wa Tuzo za mwaka huu utapambwa na burudani tofauti kutoka kwa wasanii mbalimbali na kuogezea kuwa mwaka huu onyesho litakuwa katika mwonekano wa kisasa zaidi kulinganisha na miaka ya nyuma.

“Tumekuwa tukidhamini Tuzo hizi kwa miaka kadhaa sasa na kila mwaka tumekuwa tukionyesha staili tofauti katika uboreshaji wa Tuzo hizi. Mwaka huu tumeziboresha zaidi na nina uhakika wale watakaofika kushuhudia onyesho hili watakuwa mashahidi,” Alisema Minja

Minja alisema kuwa wasanii wanaowania tuzo hizo na wale watakaotoa burudani watakaribishwa katika ukumbi huo kwa njia ya kipekee, na kuhojiwa na vyombo vya habari. “Tumeamua kutumia wasanii wa ndani na tuna imani na wanachokifanya katika suala zima la kutoa burudani,” Alisema Minja.

Alisema lengo la Tuzo hizi zinazodhaminiwa na Bia ya Kilimanjaro Premium Lager ni kufikisha muziki wa Tanzania katika kilele cha mafanikio, na kuongezea kuwa mwaka huu wameona ni vyema kuwapa nafasi kubwa wasanii wa hapa nyumbani kutoa burudani kama sehemu ya kuwapa nafasi ya kuonyesha vipaji vyao katika sanaa ya muziki,” alisema Minja.

Wasanii watakaotumbuiza katika utoaji wa Tuzo hizo ni Ali Kiba, THT, Banana Zoro, Linah, Diamond, Joe Makini, C Pwaa, 20%, Mzee Yusuf pamoja na Mapacha Watatu na Stara Thomas. Halikadhalika kutakuwa na burudani ya pamoja kutoka kwa washindi wa Tuzo za Kili kwa mwaka jana.

Kwa mujibu wa Minja, Tiketi kwa ajili ya onyesho hilo zimeshaanza kuuzwa katika vituo mbalimbali jijini Dar es Salaam kwa bei ya 25,000/- kwa tiketi za VIP na 15,000/- kwa tiketi za kawaida.

Minja alisema kuwa watu watakaolipa kiingio cha VIP watapata bia za Kilimanjaro Premium Lager bure, wakati kutakuwa na bia mia moja za Kilimanjaro Premium Lager kwa watu mia moja wa kwanza kuingia ukumbini.

Tuzo zinazoshindaniwa kwa mwaka 2010/ 2011 ni Msanii wa kike bora wa Muziki, Msanii wa Kiume Bora wa Muziki, Mwibaji bora wa Kike, Mwimbaji Bora wa Kiume, Wimbo Bora wa Taarab, Wimbo bora wa Mwaka.
Nyingine ni Wimbo bora wa Kiswahili (bendi), Wimbo bora R&B, Wimbo bora wa Hip Hop, Wimbo bora wa Ragga, Rapa bora wa Mwaka (Bendi), Msanii bora wa Hip Hop, Wimbo bora wa Africa Mashariki, Mtayarishaji bora wa Muziki, Video bora ya muziki ya Mwaka na Msanii mpya anayechipukia, Wimbo bora wa Kushirikishwa/ Kushirikisha, Wimbo bora wa asili na Wimbo bora wa Rhumba.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...