Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Thursday, August 22, 2013

FILAMU YA “FOOLISH AGE” YAIKUTANISHA LULU NA BODI YA FILAMU.

PIX 2
Msanii wa filamu Elizabeth Michael (Lulu) akieleza jambo mbele ya Katibu Mtendaji Bodi ya Filamu Tanzania Bi. Joyce Fissoo wakati kampuni ya Proin Promotions ikiwasilisha filamu yake ya “Foolish Age” kwa ajili ya ukaguzi.
PIX 1Katibu Mtendaji Bodi ya Filamu Tanzania Bi. Joyce Fissoo akiwaonyesha wajumbe pamoja na wahusika wa Kampuni ya Proin Promotions baadhi ya maeneo muhimu ya kufanyiwa marekebisho wakati walipowasilisha filamu yao ya “Foolish Age” katika Bodi ya Filamu kwa ajili ya ukaguzi. 
……………………………………………………………
 Na Benedict Liwenga-MAELEZO.
KAMPUNI ya Proin Promotions imewasilisha filamu yake iliyopewa jina la “Foolish Age” kwa Bodi ya Filamu Tanzania kwa ajili ya ukaguzi ambapo baada ya kufanyiwa marekebisho filamu hiyo inaweza kuruhusiwa katika uzinduzi wa Kampuni hiyo hivi karibuni.
Bodi ilifikia hatua ya kuwaita wahusika yaani Proin Promotions na Elizabeth Michael (Lulu) kwa ajili ya kufanya majadiliano kuhusu maudhui na maadili katika filamu hiyo kabla ya kufanyia maamuzi.
Katika majadiliano hayo Bodi ya Filamu iliwakumbusha wahusika hao kufanya baadhi ya marekebisho katika filamu hiyo ili iweze kuwa kivutio kwa umma, pia Bodi ya Filamu iliwakumbusha juu ya umuhimu wa kuzingatia kifungu cha 14 cha Sheria ya Filamu na Michezo ya Kuigiza ambacho kinaipa Bodi mamlaka ya kukagua filamu, matangazo na maelezo yote na kile cha 24 (1) (d, n na t) cha Kanuni za sheria ya Filamu na Michezo ya Kuigiza kinachofafanua mambo yanayotakiwa na yale yasiyotakiwa katika filamu ambayo filamu hiyo imekwenda kinyume.
Kwa upande wake Mwanasheria wa Kampuni ya Proin Promotions Bi. Gift Msuya alikubaliana na ushauri uliotolewa na Bodi ya Filamu na aliiomba Bodi itoe muda kwao kwa ajili ya kufanyia marekebisho katika filamu hiyo.
Naye msanii Elizabeth Michael (Lulu) aliieleza Bodi ya Filamu kuwa Filamu hiyo aliitengeneza muda mrefu na kwa sasa atazingatia maelekezo ya sheria, Kanuni na taratibu hususani katika eneo la maadili. Aidha alikiri kuwa ni kweli maeneo yaliyobainishwa kweli yanahitaji marekebisho.
Katibu Mtendaji Bodi ya Filamu Bi Fissoo alimalizia kwa kuishauri Kampuni hiyo kutotumia filamu hiyo katika uzinduzi wa kampuni yao hadi hapo watakapofanyia marekebisho katika baadhi ya maeneo muhimu ndani ya filamu hiyo.
Proin Promotions ni Kampuni inayojikita katika kuandaa na kutengeneza filamu za kitanzania na kuzisambaza nchini, pia ni kampuni inayotarajiwa kutoa ushindani mkubwa katika tasnia ya filamu. Kampuni hiyo inatarajiwa kuzinduliwa hivi karibuni baada ya maandalizi rasmi kukamilika.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...