Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Thursday, August 22, 2013

MAMA TUNU PINDA AZINDUA MRADI WA KUSAIDIA WATOTO WA KIKE NCHINI Mgeni rasimi  Mama Tunu Pinda akikata utepe kuashiria uzinduzi wa huduma ya kumsadia mtoto wa kike (kushoto) kwake ni mkururugenzi Mtendaji wa Tmarc, Bibi Diana Kisaka, ambao ni waandaaji wa mradi huo (kulia)  kwa mama Pinda ni Ludovicka Tarimo, mshauri wa masuala ya jinsia kutoka USAID anayefuatia ni Mkuu wa Vodacom Foundation, Yessaya Mwakifulefule.  Sherehe hizo zimefanyika mkoani Mtwara jana. Picha na Chris Mfinanga
 Meneja wa Vodacom Foundation,  Mwakifurefure, akiwahutubia wageni waalikwa.
Mama Tunu Pinda, akishiriki na kufurahia kucheza  ngoma ya asili maarufu ya kimakonde ambayo ilikuwa ikiburusha wageni katika uzinduzi wa mradi wakumsaidia mtoto wa kike.
**********************************************************
MKE WA WAZIRI MKUU Mama Tunu Pinda amewataka Watanzania washirikiane na wazazi na walimu kuhakikisha watoto wa kike wanasoma kwa bidii na kutimiza ndoto zao za ukubwani.
 
Ametoa kauli hiyo leo mchana (Jumanne, Agosti 20, 2013) wakati akizindua Mradi wa Hakuna Wasichoweza katika Shule ya Msingi Chilongola, iliyoko Manispaa ya Mtwara Mikindani, mkoani Mtwara. Mradi huo unafadhiliwa na Taasisi ya T-MARC inayojihusisha na Masuala ya Afya na Maendeleo, umelenga kuwafikia wasichana 10,513 katika wilaya mbili za mkoa wa Mtwara, yaani Manispaa ya Mtwara Mikindani na Wilaya ya Mtwara Vijijini.
 
Kabla ya kuzindua mradi huo, Mama Pinda aliwaita wasichana watatu na kupanda nao jukwaani na kuwahoji mmoja baada ya mwingine kwamba wangependa kufanya nini wakiwa wakubwa.
 
Mwanafunzi wa kwanza, Rahma Jamaldini (14) anayesoma darasa la saba katika shule ya msingi Chikongola alijibu kwamba yeye angependa kuwa rubani na akaambiwa na Mama Pinda ajitahidi katika masomo ya sayansi na hisabati ili asome hadi Chuo Kikuu kuweza kutimiza ndoto yake hiyo.
 
Wa pili alikuwa ni Eliza Paulo (8) mwanafunzi wa darasa la pili katika shule ya msingi Chikongola aliyesema angependa kuwa mama. Aliwavunja mbavu watu waliohudhuria uzinduzi huo alipoulizwa tena ni kitu gani angependa kufanya mbali ya kuwa mama kwa kujibu kwamba angependa kupika. Alipoulizwa mara ya tatu kitu kingine ambacho angependa kufanya, akajibu kuosha vyombo. Mama Pinda allimhimiza asome kwa bidii ili awe mama mzuri.
 
Wa tatu alikuwa ni Bora Hamisi (8) ambaye pia ni mlemavu wa ngozi. Bora anasoma darasa la pili katika shule ya msingi Msufini mjini Mtwara. Yeye alisema angependa fundi wa kushona nguo. Naye aliambiwa asome kwa bidii hasa somo la stadi za kazi.
 
Mama Pinda alisema amewaita watoto hao ili wawe mfano wa kudhihirisha ndoto na matamanio ambayo watoto wa kike wanayo na kwamba wasiposaidiwa kwa kuwekewa mazingira mazuri yatakayowafanya wahitimu masomo yao, kamwe hawataweza kutimiza ndoto zao.
 
“Watawezaje kutimiza ndoto zao kama hawahudhurii masomo kama wanafunzi wengine? Wanapaswa wasome vizuri, waende sekondari na hata vyuo vya elimu ya juu. Tuweke miundombinu itakayowasaidia kuhudhuria masomo bila kukosa,” alisema.
 
Mapema, Mkurugenzi Mtendaji wa TMARC, Bi. Diana Kisaka alisema mradi huo umelenga kuinua uelewa wa wasichana kuhusu miili yao na mabadiliko yanayotokea katika kipindi cha balehe; kuwapa ufahamu kuhusu makundi mbalimbali miongoni mwa jamii iliyowazunguka na kuwapa upeo wao kuhusu umuhimu wa kuzingatia malengo yao katika maisha.
 
Naye Mkuu wa Vodacom Foundation, Bw. Yesaya Mwakifulefule alisema Vodacom Foundation imechangia sh. milioni 160 kwenye Mradi wa Hakuna Wasichoweza kwani inatambua umuhimu wa elimu na suala zima la kuendeleza wasichana kielimu.
 
“Vodacom Foundation inashugulika na masuala ya elimu kwa kuchangia madawati na teknolojia ya habari na mawasiliano katika shule mbalimbali hapa nchini. Hapa Mtwara tumetoa kompyuta 20 kwenye shule ya sekondari ya wasichana ya Mtwara ambazo zimeunganishwa na intaneti ya Vodacom,” alisema.
 
Naye mwakilishi kutoka Shirika la Misaada la Maendeleo la Marekani (USAID), Bi. Ludovicka Tarimo, alisema taasisi yake imechangia Dola za Marekani 196,650 kwenye  mradi huo ambao wanaamini kupitia utekelezaji wake, utawasaidia mamilioni ya watoto wa kike hapa nchini kupata mafunzo ya kujitambua na hatimaye kufanikiwa kielimu.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...