Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Tuesday, January 31, 2012

BASATA, JESHI LA POLISI WAUNDA KIKOSIKAZI KUDHIBITI UHARAMIA KWENYE SANAA


Kaimu Katibu Mtendaji wa BASATA, Godfrey Lebejo akisisitiza jambo kwenye programu ya Jukwaa la Sanaa inayofanyika kila wiki makao makuu ya Baraza hilo Ilala Sharif Shamba na kuhudhuriwa na wadau wa Sanaa. Kulia kwake ni Afisa Uhusiano wa Uhamiaji Bi. Tatu Burhan.
Ssp Edson Kasekwa kutoka Jeshi la Polisi Makao Makuu, Kitengo maalum cha Operesheni uzuiaji uhalifu akitoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali kuhusu matumizi ya Sanaa katika Polisi Jamii na Ulinzi Shirikishi. Kulia kwake ni Mkurugenzi wa Ukuzaji Sanaa, BASATA Bi. Vivian Shalua.

Afisa Uhusiano wa Idara ya Uhamiaji Tatu Burhan akieleza haja ya Jamii kushirkiana na Idara yake katika kupambana na tatizo la Uhamiaji haramu nchini. Kushoto kwake ni Bw. Lebejo.
Kikundi cha Ngoma cha Jeshi la Polisi kikitumbuiza kwenye Programu ya Jukwaa la Sanaa ambapo elimu kuhusu dhana ya Ulinzi Shirikishi na Polisi Jamii ilitolewa kwa Wadau zaidi ya 140.
Sehemu ya Maafisa wa Jeshi la Polisi wakifuatilia matukio mbalimbali kwenye Programu hiyo ya Jukwaa la Sanaa.
Mkongwe wa Sanaa za Maonyesho Mzee Nkwama Bhallanga akielezea masuala mbalimbali kuhusu Sanaa Shirikishi katika Polisi Jamii na Ulinzi Shirikishi.
Wadau wa Sanaa wakiifuatilia Programu ya Jukwaa la Sanaa wiki hii.

Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) na Jeshi la Polisi nchini wameunda kikosikazi maalum kitakachokuwa kikifuatilia uharamia na maovu mbalimbali katika shughuli za Sanaa na Burudani.

Kikosikazi hicho kimeundwa baada ya Jeshi la Polisi nchini kutumia Sanaa shirikishi katika kutoa elimu kwa wadau wa Sanaa kuhusu dhana ya polisi jamii na ulinzi shirikishi kwenye Jukwaa la Sanaa linalofanyika kila wiki makao makuu ya BASATA Ilala Sharif Shamba.

Akizungumza kuhusu kikosikazi hicho, Mkurugenzi wa Ukuzaji Sanaa, BASATA Bi. Vivian Shalua alisema kuwa, kazi kubwa ya kikosi hiki itakuwa ni kufuatilia maonesho yasiyokuwa na vibali, uharamia kwenye kazi za wasanii na wasanii kutoka nje wanaoingia nchini kinyume cha sheria.

Aliyataja majukumu mengine ya kikosikazi hicho kuwa ni pamoja na kudhibiti maonesho yanayodhalilisha utu na maadili ya mtanzania, kusimamia utoaji vibali kwa wasanii wa kitanzania wanaoenda kufanya maonesho nje ya nchi na majukumu mengine yatakayojitokeza.

“Kikosikazi hiki kitakuwa tayari kufuatilia taarifa yoyote ya uharamia kwenye kazi za wasanii, maonesho yanayodhalilisha utu na maadili ya mtanzania na wasanii wanaoingia ndani ya nchi na kufanya maonesho bila vibali” alisisitiza Shalua.

Kikosikazi hicho kinaundwa na Shani Kitogo (Afisa Utamaduni Ilala), Tatia Ramadhan (Polisi, TAZARA), Afande Jeremiah (Polisi Kati), Koplo Juma Mashauri (Polisi Airport), Michael Kagondela (Idara ya Utamaduni), Afande Deus Matoro (Reli) na Afande Swai (Traffic),
Wengine ni Vivian Shalua (BASATA), Jonathan Abel na Tatu Burhan (Uhamiaji), Deus Kessy (Polisi Reli), Koplo Josephat Syllively (Polisi – Maji), Masanja Nyalali (Polisi – Airport) na PC Mwakajaby (Polisi – TAZARA)

Akizungumza kwenye Jukwaa hilo la Sanaa, Asp Edson Kasekwa kutoka Polisi Makao Makuu Kitengo maalum cha Operesheni uzuiaji uhalifu,alisema kuwa, Jeshi la Polisi linawategemea wadau wa Sanaa wakiwemo wasanii katika kutoa taarifa juu ya matukio ya uharamia na uhalifu kwa ajili ya ufuatiliaji na udhibiti.

“Ni vema Wasanii na wadau wa Sanaa kwa ujumla wakaonesha ushirikiano kwa Jeshi la Polisi katika kutoa taarifa na kudhibiti uharamia na maovu kupitia sekta ya Sanaa. Hii ndiyo maana ya dhana hii ya polisi jamii na ulinzi shirikishi ya polisi kushirikiana na jamii” alisema Afande Kasekwa.

Kikosikazi hiki kimeundwa huku kukiwa na taarifa za uwepo wa vikundi mbalimbali vinavyofanya maonesho yenye kudhalilisha utu na maadili ya mtanzania huku uharamia kwenye kazi za Sanaa ukizidi kushika kasi.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...