Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Tuesday, January 31, 2012

WIMBO MPYA WA ISHA MASHAUZI NI MOTOOO..


KIONGOZI na mwimbaji nyota wa kundi la Mashauzi Modern Taarab la jijini Dar es Salaam, Isha Ramadhani “Isha Mashauzi” ameachia wimbo wake mpya “Si bure una mapungufu” mwishoni mwa wiki iliyopita.

Kwa mara nyingine tena Isha amedhihirisha kuwa habahatishi katika kazi zake, ni ngoma kali iliyoimbwa kiufundi, vijembe vya kufa mtu na rap zilizojaa elimu huku upande wa vyombo ukichagizwa na mirindimo itakayokufanya uwe na hamu ya kuusikiliza tena na tena.

Vituo vingi vya radio vimekuwa vikipokezana kuucheza wimbo huo na kuufanya uwe gumzo jijini huku wasikilizaji wengi wakituma meseji vituoni humo kumpongeza Isha kwa kazi nzuri aliyoifanya.

Katika wimbo huo, Isha amemzungumzia mtu mwenye majivuno anayejiona anajua kila kitu, asiyependa maendeleo ya wenzake, asiyependa kukosolewa na mwenye kupenda kutukuzwa siku zote.

“Tulivyokuzoea tofauti na ulivyo, tuna wasiwasi ni mwezi mchanga, mambo yako sera zako sasa hivi ni ovyo, mara karudi tena kwa waganga, si bure una mapungufu tunakuhurumia, umekuwa kama fukufuku kila shimo waingia” ndivyo anavyotiririka Isha katika mashairi yake.

Alipoulizwa na Full Shangwe juu ya vijembe vilivyotawala ndani ya wimbo huo, Isha alisema hakumlenga mtu yeyote bali amesimama kama mwakilishi wa wale wote wanaokerwa na watu wenye tabia kama hizo ambao anaamini wamejaa kila kona.

Isha aliongeza kuwa ukitaka kuupata live wimbo huo basi jitose Mango Garden -Kinondoni Kila Alhamisi.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...