Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Saturday, January 21, 2012

TANZANIA YAWASILISHA UMOJA WA MATAIFA ANDIKO LA KUDAI NYONGEZA YA ENEO LA BAHARI


*




Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Anna Tibaijuka ( Mb) akimkabidhi kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mkurugenzi wa Idara ya Umoja wa Mataifa ya Masuala ya Bahari na Sheria ya Bahari, Sergei Tarassenko, kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Andiko la kudai nyongeza ya maili 61,000 nje ya eneo la maili 200 la Ukanda wa Kiuchumi wa Bahari wakati wa hafla fupi iliyofanyika jana jumatano katika ofisi za Idara hiyo zilizopo katika Umoja wa Mataifa, Jijini New York, Marekani

*************************************************



NA MWANDISHI MAALUM

NEW YORK


Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imewasilisha katika Umoja wa Mataifa, Andiko la kudai eneo la nyongeza lenye ukubwa wa maili 16,000 nje ya eneo la sasa la maili 200 za Ukanda wa Kiuchumi wa Bahari.




Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Anna Tibaijuka (Mb) ndiye aliyewasilisha Andiko hilo, kwa niaba ya serikali, katika hafla fupi na ya kihistoria iliyofanyika siku ya jumatano katika ofisi za Idara ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia masuala ya Bahari na Sheria ya Bahari.


Andiko hilo limepokelewa na Mkurugenzi wa Idara hiyo, Bw. Sergei Tarassenko kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.

ambaye aliipongeza Tanzania kwa hatua hiyo muhimu na kuahidi kwamba Idara yake kupitia, Kamisheni ya Umoja wa Mataifa inayohusika na mipaka ya baharí italifanyika kazi Andiko hili.



Aidha Mkurugenzi huyo ameielezea Tanzania, kama moja kati ya nchi inayoheshima sana na yenye historia nzuri katika Umoja wa Mataifa.



Akizungumza wakati wa kuwasilisha Andiko hilo, Waziri Anna Tibaijuka, amesema kwa kuwasilisha Andiko hilo, Tanzania si tu kwamba imefanya kazi ya uhakika ya maandalizi na hatimaye uwasilishaji lakini ni hatua kubwa kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa Tanzania.



Akabanisha kwamba mchakato wa maandalizi ya Andiko hilo ambao umechukua miaka mitano, umewashirikisha wataalamu mbalimbali wakiwamo wa ndani na nje , ikiwa ni pamoja na kuzihusisha nchi ambazo zinapakana kibahari na Tanzania.



Akizungumza manufaa ya kudai nyongeza ya eneo hilo, Waziri Tibaijuka anasema. “ Tanzania itanufaika kwa kuongeza ukubwa wa eneo la mipaka ya nchi lakini la msingi zaidi ni unufaikaji wa rasilimali zikiwamo za mafuta na gesi na madini ambazo zitakuwamo katika eneo hilo jipya, rasilimali ambazo kwa sasa zinaelekea kutoweka katika eneo la maili 200”.



Eneo ambalo Tanzania inadai liongezwe la maili 61, 000 ukubwa wake ni sawa na eneo la mikoa mitatu ikiunganishwa kwa pamoja.



Aidha kuongezwa kwa eneo hilo kutaisaidia pia serikali katika masuala ya ulinzi na usalama hasa katika kipindi hiki ambacho vitendo vya uharamia wa baharini vikiwa vimeongeza katika eneo la bahari ya Hindi.



“ Pamoja na kuwasilisha Andiko hilo, lakini nchi yangu inapenda pia kutoa ombi la pekee kwa idara yako, kuangalia uwezekano wa kuharakisha mchakato wa kupitia nyaraka na vielelezo tulivyowasilisha katika Andiko letu, kwani itatusaidia sana katika ulinzi wa eneo la mipaka yetu dhidi ya uharamia” akasisitiza Waziri .



Na kuongeza kwamba Tanzania, kama ilivyo kwa nchi nyingine ambazo zinaendelea zinatajitaji msaada mkubwa kutoka kwa wadau mbalimbali ikiwamo Idara ya Umoja wa Mataifa ya masuala ya bahari na sheria ya bahari katika kuukabili uharamia.



Faida nyingine ukiacha za kiuchumi ni kwa wataalamu wa fani mbalimbali kuwa na fursa ya kufanya utafiti katika eneo hilo hapo litakapokuwa limeridhiwa rasmi na kuwa sehemu ya Tanzania.



Baada ya kuwasilisha Andiko hilo, hatua inayofuatia ni kwa Tanzania kupitia wataalamu wake, itatakiwa kulitetea Andiko hilo mbele ya Makamishna wa Kamisheni ya Umoja wa Mataifa inayohusika na Mipaka ya Bahari utetezi huo utafanyika mwezi Agosti mwaka huu.



Tanzania imewasilisha Andiko hilo kwa kuzingatia Sheria ya kimataifa ya Bahari namba 76 kifungu kidogo cha 4, sheria hiyo inaziruhusu nchi ambazo ziko kando kando ya bahari kudai eneo la nyongeza iwapo zitakidhi vigezo vilivyotolewa na Umoja wa Mataifa.



Mchakato wa kuanda Andiko hilo ulianza mwaka 2007 ukiwashirikisha wataalamu wa kada mbalimbali kutoka Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Chuo Kikuu cha Ardhi na Mazingira, Wizara ya Sayansi na Teknolojia na Shirika la Maendeleo ya Petroli ( TPDC).



Sehemu kubwa ya Mradi imefadhiliwa na Serikali Kuu na kwa kusaidiwa na Serikali ya Norway.



Hafla ya kuwasilisha Andiko hilo imehudhuriwa na Balozi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Mhe. Ombeni Sefue, na waheshimiwa wabunge, Zakhia Meghji na Abulrahman Hassan Shah ambao ni wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira.



Wengine waliohudhuri hafla hiyo ni baadhi ya wataalamu waliohusika na maandalizi ya Andiko hilo ambao ni Dr. Sellasie Mayunga, Prof. Evelyne Mbende, Bw. Ayoub Mohamed Mahmoud kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Bw. Kelvin Komba na Bi. Verdiana Mashingia.



Tanzania inakuwa nchi ya 59 kuwasilisha Andiko la kudai nyongeza ya eneo la bahari na ikiwa ni nchi 10 kutoka Afrika kufanya hivyo.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...