Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Tuesday, October 2, 2012

KLABU YA KAYUMBA YA ILALA MABINGWA WAPYA WA SAFARI POOL 2012


 Mkurugenzi wa Wizara ya Habari,Utamaduni ,Michezo na Vijana, Leonard Thadeo (wapili kushoto) akimkabidhi Kikombe Nahodha wa Klabu ya Kayumba kutoka Mkoa wa kimichezo wa Ilala, Emmanuel Martin mara baada ya kutwaa ubingwa wa Taifa wa mashindano Safari Pool 2012.

Mabingwa wa Taifa Safari Pool 2012, Klabu ya Kayumba kutoka Mkoa wa kimichezo wa Ilala jijini Dar es Salaam wakishangilia na Kikombe mara baada ya kutwaa ubingwa huo jijini Mwanza juzi.
**************************
Na Mwandishi Wetu,Mwanza.
TIMU ya mchezo wa pool ya Klabu ya Kayumba kutoka mkoa maalum wa kimichezo wa Ilala jijini Dar es salaam, juzi ilitawazwa kuwa mabingwa wapya wa taifa wa  mashindano ya 'Safari Lager National Pool Championship 2012' baada ya kuikung'uta Meeda ya Kinondoni magoli 13-2 katika mchezo wa fainali ya mashindano hayo.
Fainali hizo za taifa ambazo zilishirikisha jumla ya timu 16 ambazo zilikuwa mabingwa kwenye mikoa yao katika mashindano hayo ngazi ya mikoa, zilifanyikia kwenye ukumbi wa hoteli ya Monarch mkoani hapa na kudhaminiwa na wadhamini wakuu wa mchezo huo nchini, Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia bia yake ya Safri Lager.
Kabla ya mchezo huo wa fainali ambao ulizikutanisha timu za mkoa  wa Dar es salaaam, mashabiki kibao ambao walikuwa wanausubiri kwa hamu kubwa walitegemea kuona upinzani wa hali ya juu lakini hali ilikuwa tofauti baada ya Meeda kukubali kufungwa kirahisi tofauti na mategemeo ya wengi.
Kayumba kwa kutwaa ubingwa huo walizawadiwa fedha taslim Sh.Mil. 5, kikombe kikubwa cha ubingwa huo na medali za dhahabu.
Meeda wenyewe kwa kushika nafasi ya pili waliondoka na fedha taslim Sh.Mil.2.5 , 2eyes ya Arusha iliyoshika nafasi ya tatu ilijinyakulia Sh.1,250,000 na Anatory ya mkoa wa Morogoro iliyoshika nafasi ya nne ilipewa Sh.750,000.
Kwa upande wa mchezaji mmoja mmoja (wanaume), bingwa wa mkoa wa Mbeya, Solomon Elias ambaye ni bubu alitwaa ubingwa huo wa taifa baada ya kumkandamiza, Athuman Seleman wa Morogoro magoli 5-1 katika mchezo wa fainali na kujinyakulia Sh.500,000.
Athumani Seleman kwa kushika nafasi ya pili ilizawadiwa Sh.250,000, wakati ambapo Fayuu Staniley wa Arusha alipewa Sh.200,000 kwa kushika nafasi ya tatu na Ally Nada wa Manyara aliyeshika nafasi ya nne aliambulia Sh.150,000.
Mkoa wa Mbeya walionekana kujiandaa vizuri kwa upande wa mchezaji mmoja mmoja baada ya Betty Sanga naye wa mkoa huo kutwaa ubingwa wa taifa wa mashindano hayo baada ya kumchapa Cecilia Kileo wa Kilimanjaro magoli 5-2 katika mchezo wa fainali.
Betty kwa kutwaa ubingwa huo alijinyakulia fedha taslim Sh.350,000, wakati ambapo Cecilia aliyeshika nafasi ya pili aliondoka na Sh.200,000, Sada Tulla wa mkoa wa Shinyanga aliyemaliza fainali hizo akiwa nafasi ya tatu alizawadiwa Sh.150,000 na Anna kutoka mkoa wa Iringa aliyeshika nafasi ya nne alipewa Sh.100,000.
Mbali ya zawadi kwa washindi hao lakini pia timu zote ambazo hazikushika nafasi hizo nne za juu zilizawadiwa fedha taslim kulingana na nafasi zilizoshika pamoja na wachezaji wote wa mchezaji mmoja mmoja ambao nao hawakushika nafasi za juu.
Zawadi zote kwa washindi zilikabidhiwa na Mkurugenzi wa Michezo Tanzania, Leonard Thadeo ambaye ndiye aliyekuwa mgeni rasmi katika kilele cha fainali hizo.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...