Na Onesmo Ngowi
Masumbwi
au kwa majina mwengine ndondi au ngumi na kwa majina ya mitaani ndogwa,
mawe n.k. ni mchezo unapoendwa sana na watu wengi. Aidha mchezo huu ni
kati ya michezo inayoogopwa sana duniani. Mchezo wa ngumi uko hatarini
kupoteza maana yake ya asili yaani kucheza kama burudani, kuwakilisha
nchi na kujenga ushupavu wa mchezaji. Mamilioni ya watu wanaojazana
kuutazama wasingependa kabisa kujiingiza kuucheza mchezo wa ngumi. Sasa
endelea………………………………….!
Afrika
inahesabiwa kuwa na mabondia shapavu wanaotumika kuwapandisha chati
mabondia wa nchi za Ulaya, Marekani na Asia. Kwa kuwa wengi wanatoka
kwenye famililia za kipato cha chini hawana cha kufanya ila kuingia
kwenye mtego huu na mwishoni wanaharibu rekodi na maisha yao kwa fedha
ndogo.
Wapo
mabondia toka Afrika ambao wameshatumika kuwapa mazoezi ya maandalizi
mabondia kama kina Mike Tyson, Mumahhad Ali, Lenox Lewis, Evander
Holyfield kwa malipo madogo sana. Mabondia hawa hulipwa kiasi
kisichozidi dola 20 – 50 kwa kila raundi wanayocheza.
Lakini
maumivu na madhara wanayopata ni sawa na kucheza pambano zima la raundi
8 – 12. Wakati wanalipwa dola 20 – 50 kwa raundi wenzao wanalipwa dola
milioni 3 – 20 kwa pambano ambalo wakati mwingine huchukua kati ya
dakika 1 – 20. Wengi wa mabondia hawa wamedhurika kwa kiwango kikubwa
kiasi kwamba hawawezi kuishi maisha ya kawaida na fedha za kujikimu
hawana.
Nchi
zinatakiwa kuweka sheria kali zinazowabana watu kuweza kuwatumia
mabondia wake hovyo. Tusipofanya hivi tutaishia kuwa na vijana wengi
walioharibika na walio mzigo kwetu sisi kama taifa.
Ni rahisi sana kwa kiongozi au mwananchi yeyote kupuuza jambo hili kwa madai kwamba “kwani ananihusu nini”. Lakini
inapotokea kuwa na watu wengi walio na uharibifu wa ubongo na ambao
hawawezi kujishughulisha na kazi za ujenzi wa taifa ni mzigo mkubwa kwa
kila mwananchi.
Nchini
Zambia walipata mzigo mkubwa sana kuwatunza kina Lottie Mwale na
wengine ambao walikuwa hawawezi kujihudumia wenyewe. Taifa haliwezi
kudharau kuwahudumia watu walioliletea sifa kemkem na matokeo yake
wanahangaika kila siku kuwatunza.
Urahisi
na njia za mkato kwa mabondia wa kitanzania kupelekwa nje ya nchi wengi
kwa siri kutalipelekea taifa hili pabaya. Mabondia wengi wa kitanzania
ama kwa urahisi wa kupata hati za usafiri au kwa msaada ya baadhi ya
viongozi wa serikali wanasikika kucheza kila kona ya dunia.
Mengi ya mapambano haya wanadhulumiwa wengine wakirudimhawana hata pesa za nauli za kwenda kwao kutokea Dar-Es-Salaam.
Labda
nieleze sababu kubwa ya TPBC kama msimamizi mkubwa wa taratibu, kanuni
na sheria za ngumi za kulipwa hapa Tanzania, inapohahakisha kuwa bondia
anatakiwa awe na vibali vyote kabla ya kwenda nje ya nchi.
1. Usalama wa afya: TPBC hutaka kupata vielelezo vya afya ya bondia anayecheza na bondia wa Kitanzania
ili kulinda afya ya bondia wetu asidhurike.
2. Uwiano: TPBC hutaka kupata rekodi za bondia mpinzani ili ione kama bondia wa kitanzania hapigani na
bondia mpinzani aliyemzidi sana ujuzi. Hili ni suala muhimu ili kulinda usalama wa bondia wa Kitanzania.
3. Mkataba: ni lazima TPBC kuhakiki mkataba kwa ajili ya mambo yafuatayo:
(a) Kuzuia kudhulumiwa.
(b) Kuangalia vipengele vinavyoweza kumfunga bondia kwa promota. Mara nyingi mikataba ya ngumi ina
vifungu vinavyomtaka bondia awe chini ya promota wa pambano kama atashinda, hivyo kumfunga kwenye
mkataba huo. Mabondia wengi hawawezi kutafsiri hili na memeneja wengi huwaficha ukweli huu.
(c) Mikataba mingi haifafanui faida nyingine bondia anazotakiwa kupata mbali na malipo ya pambano. Kwa
mfano kama pambano husika linarushwa kwenye televisheni au linarusha matangazo, bondia anatakiwa alipwe
asilimia kadhaa ya mapato haya mbali na fedha za pambano lenyewe. Hili ni suala la ufundi ambalo mabondia
wengi hawajui na hivyo kupoteza haki zao kwa mameneja hawa waajabu.
Sisi
tunao uwezo wa kusoma mkataba na kudai haki za bondia kabla ya pambano
kwa kushirikiana na chama cha mchezo huo nchi unakochezwa. Lakini bondia
anapotoroshwa na kurudi akilia baada ya kudhulumiwa (mara nyingi
hutokea hata kutolipwa fedha hata senti tano) sisi kama Kamishrni
hatuwezi kufanya lolote.
Kama
nilivyokwisha eleza kwenye kurasa za mwanzo inakuwa rahisi sana kwa
mameneja feki kuwapata mabondia kutokana na njaa zao kali. Mabondia
wengi hawapati mapambano ya ngumi hivyo kukaa kwa muda mrefu na hawana
njia nyingine ya kujipatia pato lolote mbali na kucheza ngumi.
Wanapofuatwa
na hawa mameneja feki kwao ni kama mungu kawaletea mkombozi (bila kujua
kwamba ni kiama) hivyo wanakubaliana nao bila hata ya kuuliza maswala
mengi mbali na fedha wanazopigania.
Wengi
hawana haja ya kujua wanacheza na bondia wa kiwango kipi, pambano ni la
aina gani (ubingwa au lisilo la ubingwa). Wakishajua tu nchi
wanayotakiwa kucheza, tarehe na uzito basi wanaingia kazini na kumwachia
meneja kufanya mambo mengine muhimu.
Muda
wanaopewa kujiandaa ni mdogo sana hivyo maandalizi kuwa madogo sana sawa
na kutoa jasho tu kwa wiki 2 au 3 kabla ya pambano.
Wengi wao
wakishapata tu uhakika wa kucheza huanza kukopa fedha za kujiandaa na
imeshatokea mara nyingi kwa mabondia kuingia ulingoni kucheza na kulipwa
fedha zote zinazoenda kulipa madeni waliyokopa na mara nyingi hata
hazitoshi. Wanaporudi nyumbani huwa mikono mitupu.
Tabia hii
haipo tu hapa kwetu Tanzania hata nchi kubwa kama Marekani na nchi za
Ulaya zipo. Kuna mifano mngi ambayo bondia analazimika kucheza ili alipe
madeni mbalimbali anayodaiwa kama fedha alizopoteza kwenye kamari,
fedha za kuwatunza watoto anaodaiwa kuzaa na kina mama mbalimbali, madai
ya kodi za serikali n.k. Huko Marekani mabondia wengi waliokwisha kuwa
mabingwa wa dunia kama kina Roberto Duran na Mike Tyson wamo kwenye
mkumbo huu.
Ni rahisi
sana kwa bondia kuingia kwenye mkumbo huu kwani wakati akiwa kwenye
chati anawaachia watu wengine kumeneji fedha zake. Watu hawa wanaoachiwa
nao wana shida zao binafsi zinazohitaji fedha pia hivyo huzitumia kwa
faida zao wenyewea.
Mabondia
wengi mabingwa wa dunia waliopata kupeta sana waliishia kudaiwa
mamilioni ya fedha baada ya kutoka kwenye chati. Wengi walikuta kwamba
fedha zilizodaiwa kulipia kodi n.k. kazikutumika kwa malipo hayo hivyo
kubakiwa na madeni makubwa ajabu.
Aidha ni
kawaida kwa bondia kupoteza fedha nyingi kwenye matumizi ya kawaida. Kwa
kuwa bondia ni shujaa kama nilivyokwisha sema hapo mwanzo ni mtu
anayeheshimika na kupendwa. Daima huzungukwa na wapambe ambao hawaleti
lolote mbali na kumla tu.
Naye kwa
ajili ya kutunza sifa hawezi kuruhusu mtu yeyote (mpambe) ajigharamie
mwenyewe. Watu wa kila aina wanaume kwa wanawake humzunguka na wengi wao
wanayo malengo yao wanayotaka awatimizie au wanamtumia kuyatimiza.
Kazi nzito
hutokea wakati chati ya bondia huyo inapofikia kikomo na kuanza kuona
wapambe wake wakiyoyomea mmoja baada ya mwingine. Lakini kama bado anazo
fedha watazidi kumzinga ili wazichangamkie. Wapambe ni watu wa kwanza
kabisa kujua wakati fedha zinapoishia kabla hata ya mhusika mwenyewe.
Wapambe
wana pua ndefu zinazonusa mifuko kuanzia chini kabisa. Kitu rahisi
kabisa kwao kuanza kuona ni wakati mtirirko wa huduma unapopungua. Kama
ni wanywaji waliokuwa wanakunywa bia 20 kwa siku inapofikia kuambulia
chupa 10 basi wanaanza kujiandaa kutimka.
Lakini
wapambe ni watu wasio na faida yoyote mbali na kukaa tu kumsifia bondia
na kumdanganya kwamba hakuna mtu mwingine kama yeye. Ili wamle vizuri
wengine wanadiriki hata kumfananisha na Rais wa nchi. Wapo wanaoenda mbali na kumfananisha bondia wanayemla na watakatifu fulani.
Bondia
anapoisha na kwa bahati mbaya awe hakuwekeza fedha zake au anao ujuzi
mwingine mbali na ngumi basi huishia mahala pabaya sana. Wapo wanaoishia
kuwa walinzi (korokoroni), madobi, mabaunza, makuli na fani za kila
aina.
Ninilisema
hapo mwanzo kuwa elimu ndogo ndilo tatizo kubwa la mabondia wetu. Kwa
kukosa elimu inayoweza kuwapa ujuzi mbalimbali wanapoisha kimchezo basi
inakuwa ndio mwisho wao. Nataka nieleze wazi kuwa tatizo hili sio hapa
kwetu Tanzania peke yake.
Hata nchi
zilizoendelea pia wana tatizo hili. Tofauti ya wenzetu ni kwamba wakati
bondia akiwa kwenye chati huingizwa kwenye mifuko mbalimbali ya Pensheni
na akiba hivyo baada ya kutoka kwenye chati basi wanaendelea kulipwa
fedha za mafao.
Japokuwa
wapambe ndo basi tena lakini angalao wana fedha za kujikimu. Vile vile
utakuta wanawekeza fedha kwenye bima mbalimbali au makampuni mbalimbali
ya biashara yanayowapa faida kila baada ya vipindi kadhaa. Mfumo huo
hapa kwetu Tanzania bado hakuna.
Lakini ni
muhimu kuweko na sheria zinazowataka wanamichezo wetu kuwekeza fedha zao
kwa kujiunga na mifuko mbalimbali ya Pensheni. Tusipofaya hivyo
tutaishia kuwa na ma-stars wetu waliong’ara duniani kama mabaunsa,
walinzi, madobi na hata makuli.
Ni wazi
kwamba watakuwa sio mifano ya kuigwa kwenye jamii hata kidogo. Hii
inadidimiza sana michezo (kwani hakuna mzazi atakayediriki kumwachia
mwanae ajiunge na michezo kwa hofu ya kuwaona kwenye hali mbaya).
Lazima
kuwe na mifumo itakayobadilisha kabisa maisha ya wanamichezo wetu, hata
kama itabidi serikali kutumia gharama kubwa kuiweka mifumo hii. Kwa hali
ya sasa ni vigumu kwa Watanzania wengi kujitokeza kujiunga na michezo
kama ajira kwani hakuna watu wengi wa kuigwa. Tungekuwa na wanamichezo
wenye mafanikio na wanaoendesha maisha yao vizuri basi karibu kila
Mtanzania angejiunga na michezo.
Watokee tu wanamichezo 10 wanaomiliki Benzi jijini Dar-Es-Salaam basi kila mtu anagejiunga na michezo.Inaendelea…………..!
No comments:
Post a Comment