MABINGWA
watetezi na vinara Ligi Kuu ya Bara, Simba, leo wanashuka kwenye Uwanja wa
Mkwakwani jijini hapa kuwakabili Coastal Union katika mechi inayotarajiwa kuwa
yenye ushindani mkubwa kwani wakali hao wa Msimbazi, watakuwa wakipigania
ushindi ili kuendeleza rekodi ya kutofungwa.
Tangu kuanza
kwa ligi hiyo Septemba 15, Simba imecheza mechi sita na kushinda tano na sare
moja, hivyo kuongoza kwa pointi 16 huku Coastal Union ikiwa nafasi ya saba
baada ya kujikusanyia pointi tisa katika mechi sita.
Kikosi cha
Simba chini ya Mserbia Milovan Cirkovik, tayari kimewasili mjini humo tangu
juzi kwa mechi hiyo ambayo itachezeshwa na mwamuzi Simon Mberwa wa Pwani
akisaidiwa na Godfrey Kihwili na Abdallah Uhako wote kutoka jijini Arusha.
Akizungumza
mechi hiyo kutoka jijini Tanga, Meneja wa Simba, Nico Nyagawa, alisema kikosi
kipo fiti kupigania pointi tatu kuendeleza wimbi la ushindi.
Nyagawa,
nyota wa zamani wa Simba na Taifa Stars, alisema licha ya ubora wa kikosi chao,
wanataraji kupata upinzani mkali kutoka kwa Coastal Union kwani ni kati ya timu
zenye kiwango kizuri kwenye ligi hiyo na ndiyo maana wamevuna pointi tisa
kwenye mechi sita.
“Tupo vizuri
katika kila idara…mechi itakuwa ngumu kwani Coastal nayo ni moja ya timu nzuri,
lakini vijana wamekamia kushinda,” alisema Nyagawa.
Alisema
Simba itawakosa nyota wake watano akiwemo Emmanuel Okwi aliyekwenda kuitumikia
timu ya taifa ya Uganda
‘The Cranes’ inayojiandaa na mechi ya kuwania tiketi ya fainali za Mataifa ya
Afrika, Mrisho Ngasa, Koman Keita, Kigi Makassy na Haruna Shamte ambao ni
wagonjwa.
Naye Ahmed
Khatib anaripoti kutoka Tanga kuwa, Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Halima Dendego,
amewataka wachezaji wa Coastal Union iliyopiga kambi kwenye Hoteli ya In by the
Sea iliyopo eneo la Raskazone, kucheza kwa juhudi kubwa ili kushinda na kuwapa
raha wapenzi na mashabiki wao na wakazi wa jiji hilo kwa ujumla.
“Nasema
kutokana na maendeleo yenu mazuri katika mechi zilizopita, nimewaona ni wazuri
na mna uwezo wa kushinda mchezo wa leo dhidi ya Simba bila kuangalia ukubwa wa
timu husika,” alisema Dendego kabla ya kukabidhi kiasi cha sh 300,000 kwa
wachezaji wa timu hiyo.
Akipokea
fedha hizo, Nahodha wa Coastal Union, Said Sued, alimshukuru kiongozi huyo na
kuahidi kucheza kwa juhudi kubwa ili kushinda mechi hiyo na kuzidi kujiweka
kwenye nafasi nzuri katika vita ya kupigania ubingwa wa ligi hiyo inayofanyika
chini ya udhamini wa Kampuni ya Vodacom-Tanzania.
Mechi
nyingine leo itakuwa kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro kwa Polisi Moro kuwakaribisha
Azam FC. Inatarajiwa kuwa ya ushindani mkubwa kwani wakati maafande wakitaka
kushinda kuondoka mkiani mwa ligi hiyo, wapinzani wao watakuwa wakitaka
kushinda kufikisha pointi 13.
Kwenye
Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, wenyeji Tanzania Prisons iliyo nafasi ya
tano kwa pointi tisa watawakaribisha maafande wenzao wa JKT Orjoro, pia yenye
pointi tisa.
Nayo Ruvu
Shooting iliyo nafasi ya 11 kwa pointi sita, itakwaana na African Lyon kwenye
Uwanja wa Mabatini mjini Mlandizi huku mabingwa mara mbili wa Ligi Kuu (1999 na
2000), Mtibwa Sugar watakuwa wenyeji wa Mgambo Shooting kwenye Uwanja wa
Manungu, Turiani, Morogoro.
No comments:
Post a Comment