DAR ES SALAAM, TANZANIA
KAMPUNI ya Reli Tanzania (TRL) limesema kuanzia sasa Watoto chini ya
umri wa miaka saba, watasafiri bila malipo na watapewa viti yaani siyo
kama katika daladala za jiji la Dar es Salaam, ambako ni dhambi mtoto
kukaa kitini.
"Tunapenda kuwafahamisha wasafiri wetu wa Reli ya Kati wa daraja la tatu
kwamba kuanzia sasa watoto chini ya miaka saba watasafiri bure na
watapewa kiti/viti" limesema tangazo la TRL, lililotolewa na Afisi ya
Uhusiano kwa niaba ya Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TRL Mhandisi Kipallo
A.Kisamfu na kuchapishwa leo kwenye baadhi ya vyombo vya habari.
Kwa mujibu wa tangazo hilo watoto lazima wawe wamesafiri na wazazi au
walezi wao lakini kasheshe kubwa ni kwamba lazima wawe na vyeti vya
kuzaliwa au barua ya serikali za mtaa ya uthibitisho wa mhusika na mzazi
au mlezi.
TRL inasema, vitambulisho hiyo lazima vionyeshwe wakati mzazi au mlezi
anakata tiketi na msafiri anaruhusiwa kusafiri na watoto wawili tu kwa
wakati mmoja na watoto watapewa tiketi maalum za watoto na kwamba mtoto
atakayekutwa kwenye treni akiwa hayupo kwenye utaratibu, atalipishwa
nusu nauli ya mtu mzima.
No comments:
Post a Comment