Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Friday, October 5, 2012

MCHEZO WA MASUMBWI, TAA INAYOZIZIMA – SEHEMU YA NANE




Na Onesmo Ngowi

Masumbwi au kwa majina mwengine ndondi au ngumi na kwa majina ya mitaani ndogwa, mawe n.k. ni mchezo unapoendwa sana na watu wengi. Aidha mchezo huu ni kati ya michezo inayoogopwa sana duniani. Mchezo wa ngumi uko hatarini kupoteza maana yake ya asili yaani kucheza kama burudani, kuwakilisha nchi na kujenga ushupavu wa mchezaji. Mamilioni ya watu wanaojazana kuutazama wasingependa kabisa kujiingiza kuucheza mchezo wa ngumi. Sasa endelea………………………………….!
MFUMO FEDHA, NA TAA INAYOZIZIMA
   Kama nilivyokwisha elezea hapo mwanzo ngumi zilichezwa kwa ushindani mkubwa kuwakilisha nchi za mabondia wapinzani. Miaka ya sasa tumeona kabisa mwelekeo tofauti wa ngumi na ambao kwa kiwango kikubwa kimeushusha kabisa hadhi mchezo wenyewe.
Mabondia wengi wa miaka ya sasa toka nchi za Afrika Mashariki wanashiriki tu kwenye mapambano kwa lengo la kupata fedha za kujikimu.
Wengi wa mabondia hawa hutoroshwa nchini mwao kimyakimya na mameneja feki wenye lengo la kuwatumia kujipatia fedha. Mabondia wengi wa zamani wamegeuka kuwa mawakala feki wa mameneja hawa wenye lengo la kuwatumia mabondia kwa manufaa yao.
Mabondia wengi toka nchi za Afrika Mashariki wamewahi kutapeliwa fedha nyingi na mameneja / mapromota hawa feki baada ya kucheza mapambano katika nchi za Ulaya, Asia na hata Afrika.
“Fedha” na sio kitu kingine chochote kinachokuwa msukumo wa wanamasumbwi wengi wa Kitanzania kucheza ngumi. Kuna mameneja / mapromota wengi wa nje wanaosema wazi kwamba wanamtaka bondia wa kushindwa na sio wakushindana.
Hii ni kwa sababu wanataka kuwatengenezea rekodi nzuri mabondia wao. Yapo maombi toka kwa mameneja hawa matapeli ambapo wanaomba bondia wa Kitanzania aandaliwe pambano feki hapa nyumbani ili rekodi yake ikubalike na shirikisho la nchi yake na hatimaye kumsaidia kumpandisha viwango bondia wake.
Mchezo wa ngumi umepoteza mwelekeo sio tu hapa Tanzania bali dunia nzima. Mameneja / mapromota wengi huwatengeneza mabingwa badala ya kuwaacha mabondia wake wawe mabingwa wa kweli.
Kwa kawaida bondia bingwa anatakiwa awe amewashinda mabondia karibu wote walio kwenye uzito / kiwango chake ndipo ajulikane kama bingwa.
Lakini mabingwa wa sasa wanatengenezwa toka pambano la kwanza kwa kupambanishwa na mabondia hafifu ili awashinde na kutengeneza rekodi nzuri. Wapo mabingwa wengi wa dunia waliotengenezwa kwa njia hii badala ya kuwa mabingwa kwelikweli. Hii yote ni kwa ajili ya fedha.
Bingwa yeyote anapotakiwa atetee ubingwa wake hupewa donge nono. Kwa  bingwa anayetambuliwa na mshirikisho kama WBA, IBF, WBO na WBC donge la fedha analopewa ni kubwa zaidi. Mameneja wengi hutumia fedha kuwaingiza mabondia wao kwenye viwango vya mashirikisho haya ili kuwaweka katika orodha ya kuelekea kwenye ubingwa.
Mara tu bondia anapokuwa bingwa hujihakikishia ulaji na meneja / promota wake anamchagulia wapinzani wasioweza kumnyang’anya ubingwa huo ili aendelee kutulia nao.
Bingwa huyu anawezza kukaa na ubingwa kwa muda mrefu sana. Mfumo wa sasa wa ngumi unalenga kuwanufaisha wale walio na bondia kama mamaneja, promota, wakala, matchmakers na bondia wengine. Mfumo fedha unadidimiza mchezo wa ngumi.
Kuna makubaliliano na ushirikiano mkubwa sana wa siri kati ya meneja, promota na baadhi ya mashirikisho husika ili bondia aweze kuwa bingwa na atetee ubingwa wake kwa muda mrefu. Hali hii japokuwa inadhibitiwa kwa kiasi kikubwa miaka ya karibuni bado imechangia kwa kiasi kikubwa kushuka kwa mchezo huu kidunia.
Miaka ya karibuni makundi (rackets) kama hizi ziligundulika na kuwekwa wazi kwenye Shirikisho la Ngumi la Kimataifa (IBF). Rais wa zamani wa IBF Bob Lee Sr. pamoja na maofisa wengine walitiwa hatiani kwa kosa la kuwatengenezea mabondia ulaji kama huu.
Walisemekana kuwa walidai kiasi cha dola kama 300,000 ili bondia apandishwe kiwango na achezee ubingwa. Bob Lee Sr. na wenzake walikumbwa na kashfa hii na kuondolewa IBF.
Japokuwa mashirikisho mengi ya ngumi bado yanaendelea na uozo huu ni juhudi ndogo sana zinazofanywa kuwabana. Ilikuwa rahisi kwa IBF kubanwa kwa kuwa sheria za nchi ya Marekani zilitumika. Mengi ya mashirikisho ya ngumi yapo nje ya sheria za Marekani na sio rahisi kuwadhibiti. Badala yake juhudi nyingi zinafanywa na mabondia wachache kwa kufungua kesi za madai mahakamani ili kuweza kupata haki zao.
Mameneja / mapromota nao hawako nyuma kwenye kashfa mbalimbali za ngumi zinazohusu utumiaji wa fedha za mabondia na hata kuwatibulia kuwa mabingwa. Ziko kesi nyingi kwenye mahakama huko Ulaya na Marekani ambazo mabondia wanawadai mameneja / mapromota mamilioni ya fedha. Mara nyingi kesi hizi humalizwa nje ya mahakama kwa makubaliano.
Sheria kali zinazoendesha mchezo huu zinatakiwa zifuatwe na udhibiti uwe wa hali ya juu. Sio rahisi kupata mafanikio katika mchezo huu bila sheria hizi kufuatwa na kila mdau.
“Niletee bondia asiye mkali ili asimpe shida bondia wangu. Mtengenezee pambano la kumpandisha rekodi yake. Mtengenezee leseni mpya inayoonyesha rekodi nzuri”
Haya ni baadhi tu ya maelekezo yanayotoka kwa mameneja wa nje wanapotafuta bondia wa Kitanzania kwenda kucheza huko nje. Kuna kundi kubwa la mameneja hawa wachwara ambao wanashirikiana na mawakala wa kila aina hapa Afrika.
Wengi wa mawakala hawa kama nilivyokwisha eleza hapo mwanzo ni mabondia wa zamani na wafanya biashara wanaotumia nafasi ya kumpeleka bondia nje ili wakanyooshe mambo yao.
Inapotokea safari ya nje kwa bondia wafanya biashara hawa hawawezi hata kuwa-sekondi (kuwahudumia) mabondia kwenye kona zao na badala yake wanawaachia wageni wa nchi wanayochezea kufanya kazi hiyo. Ni wazi kwamba bondia anapohudumiwa na mgeni tena anayetaka ashindwe ana nafasi ndogo sana ya kufanya vizuri. Wengi wa wahudumu hawa hawaelewani hata lugha na bondia mwenyewe!
Safari nyingi za mabondia wetu siku hizi wanatakiwa wasafiri wenyewe ili eti wawakute wahudumu nchi wanayokwenda. Kwa kawaida kila bondia wanatakiwa asafiri na meneja na kocha wake. Hii ndiyo kawaida ya safari za mabondia wa ngumi za kulipwa. Lakini hili halitokei siku hizi. Iaendelea………………………….!
Mwandishi wa makala haya ni; Rais wa Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBC), Shirkisho la Ngumi za Kulipwa Afrika Mashariki na Kati (ECAPBF), Shirikisho la Ngumi la Kimataifa bara la Afrika, Masharilki ya Kati, Ghuba ya Uarabu na Uajemi (IBF/AFRICA) na Mkurugenzi wa Baraza la Ngumi la Jumuiya ya Madola (CBC) E-mail: ibfafrica@yahoo.com

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...