Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Tuesday, August 30, 2011

Msondo Ngoma, Twanga Pepeta kunogesha idi TCC Club

Na Mwandishi Wetu


Bendi maarufu nchini za Msondo Ngoma na African Stars “Twanga Pepeta” zinatarajia kukonga nyoyo za wapenzi wao zitakapotumbuiza leo na kesho katika ukumbi wa TCC Club Chang’ombe, Temeke Dar es Salaam.


Bendi hizi mbili maarufu nchini hazijafanya maonyesho katika ukumbi huu kwa kipindi chote cha mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani, jambo ambalo limefanya wapenzi wao kuwa na kiu ya burudani.


Msondo Ngoma ndiyo itakuwa ya kwanza kutumbuiza leo (Iddi Mosi) mchana kwenye onyesho la Konyagi Idd Bonanza.


Onyesho hilo litaanza saa nane mchana ambapo mwanamuziki nguli hapa nchini Muhidin Gurumo ataonekana tena kwenye jukwaa la Msondo Ngoma baada ya kutoonekana jukwaani kwa muda mrefu kutokana na kuugua.


Bonanza hilo pia litatumiwa na Msondo kusheherekea tuzo yao ya kuwa bendi bora ya muziki wa rumba Afrika Mashariki na Kati.


Wiki iliyopita Msondo ilizibwaga bendi maarufu za JB Mpiana na Werason Ngiama Makandi, kwenye tuzo zilizofanyika Nairobi, Kenya hivi karibuni.


Twanga Pepeta, itatumbuiza kesho usiku (Iddi Pili) kwenye ukumbi huo wa TCC Club kwenye onyesho lingine iliyodhaminiwa na Konyagi pia.


Mratibu wa monyesho hayo, Joseph Kapinga, amesema jana kuwa maandalizi ya shoo zote mbili zimekamilika. Maonyesho yote mawili yameaandaliwa na Keen Arts ikishirikiana na Bob Entertainment chini ya udhamini wa Konyagi.


Naye mkurugenzi wa Twanga Pepeta, Asha Baraka, amesema kuwa onyesho hilo litatumika kutangaza albamu yao mpya inayotarajiwa kutambulishwa rasmi baadaye mwaka huu.


Nyimbo zilizomo kwenye albamu mpya ya Twanga Pepeta ni pamoja na “Kauli, Kiapo cha Mapenzi, Umenivika Umasikini, Mtoto wa Mwisho, Dunia Daraja” na “Penzi la Shemeji.”


Asha alisema kuwa onyesho la TCC pia litatumika kumtambulisha Kimwana wa Twanga Pepeta 2011 Mary Khamis ambaye amejiunga na bendi hiyo kuchukua nafasi ya mnenguaji Aisha Madinda aliyetimkia katika bendi ya Extra Bongo

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...