Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Sunday, August 14, 2011

Serikali imsaidie Msama katika vita ya wanaorudufu kazi za wasanii


* Wabunge wampongeza kwa kazi nzuri kutetea hakimiliki Na Mwandishi Wetu BAADHI ya Wabunge, wamepongeza kazi inayofanywa na Mkurugenzi wa Kampuni ya Msama Auction Mart, Alex Msama kwa kuwa mstari wa mbele kudhibiti wizi wa kazi za wasanii nchini. Mbunge wa Viti Maalumu, Martha Mlata (CCM) alisema Msama anastahili kupongezwa kwa kazi anayofanya, na akaiomba Serikali kumuunga mkono katika mapambano hayo kwa ajili ya maslahi ya wasanii. Mlata alisema Msama amejitokeza kupambana na wezi wa kazi za wasanii nchini, na mpaka sasa amefanikiwa kukamata kazi zenye thamani ya zaidi ya sh. milioni 200. Naye Mbunge wa Viti Maalumu, Vicky Kamata (CCM) akichangia mjadala wa mapato na matumizi ya bajeti ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kwa mwaka 2011/12 bungeni mjini Dodoma wiki hii, alisema Msama anafanya kitendo cha kujitoa na kuhatarisha maisha yake, hivyo Jeshi la Polisi lina kila sababu ya kumuunga mkono na kumlinda. Kauli hizo zimetolewa baada ya hivi karibuni Serikali kusema imepanga kutekeleza utaratibu wa wasambazaji wote wa kazi za wasanii nchini kubandika stika ya usalama ijulikanayo kama HAKIGRAM. Stika hiyo itawekwa kwenye kila nakala ya kazi itakayosambazwa ili kuhakikisha kuwa kazi za wasanii haziibwi kwani kutokana na wizi wa kazi za wasanii, sh. bilioni 20 zinapotea kwa mwaka. Kauli hiyo ilitolewa bungeni na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Adam Malima kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Ester Bulaya (CCM) aliyetaka kujua mkakati wa Serikali katika kudhibiti wizi wa kazi za wasanii nchini. Akijibu swali hilo, Naibu Waziri huyo alisema kutokana na changamoto zilizojitokeza katika mpango wa awali wa kupambana na wizi wa kazi za wasanii, Serikali katika kipindi cha miaka mitano ijayo imepanga kutekeleza utaratibu wa wasambazaji wote nchini wa kazi za wasanii kubandika stika ya usalama. Pia Naibu Waziri huyo alieleza kuwa Serikali ilifanya tathmini na kubaini kwamba ukubwa wa soko la kazi za wasanii kupitia soko la kanda za sauti na CD ulifikia nakala milioni 20 kwa mwaka. Alisema hatua hiyo inatokana na ukweli kuwa kanda hizo zinazozalishwa nchini zilikuwa zinauzwa katika nchi za Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Malawi, Rwanda na Zambia na kuwa mauzo hayo hayakuwanufaisha wasanii wa Tanzania pamoja na Serikali kwa ujumla. Serikali imetoa utaratibu huo huku Kampuni ya Msama Auction Mart ikiendelea kukamata VCD za kughushi zenye thamani ya mamilioni ya fedha. Msama anasema mpaka sasa kazi zenye thamani ya sh. milioni 200 zimekamatwa kutoka kwa watu mbalimbali zikiuzwa kinyume cha sheria. Msama anasema,VCD hizo ni mchanganyiko wa zenye nyimbo za Injili, Bongo Fleva na miziki mingine, ambazo zinauzwa kuanzia sh. 1,000 mpaka sh. 700. Anasema, mmoja wa waliokamatwa ni msambazaji maarufu wa kazi za wasanii mwenye ghala la kudurufu na kuhifadhia VCD hizo maeneo ya Tandika, Dar es Salaam. Hakuna budi kumpongeza Msama kwa hatua hiyo, na pia kuwaomba wasanii kuungana na kuwazidishia ulinzi kwani kwa sasa wafanyakazi wa kampuni yake wanatishiwa maisha kwa madai ya kuingilia shughuli za watu. Kwa muda mrefu wasanii mbalimbali wamekuwa wakilalamika kuibiwa kazi zao, na hivi karibuni wameunda kampuni ambayo itakuwa msimamizi mkuu wa kazi zao. Hapana shaka taarifa hiyo imekuna wapenzi wa sanaa nchini kutokana na uamuzi wa wanamuziki wa Bongo Fleva kuunda kampuni kwa lengo la kukabiliana na wezi wa kazi zao na pia kutumia kampuni kushinikiza mabadiliko katika sheria inayolinda kazi za wasanii nchini. Napenda kuwapongeza wasanii hao kwa kuamua kushiriki wenyewe katika vita hiyo, na kutoa mwelekeo mpya katika mapambano dhidi ya maharamia wa kazi za wasanii. Kwa kuwa na kampuni ambayo inaundwa na wasanii wenyewe, wanaonesha nia ya kujitawala na kutoa msukumo mpya kwenye sekta ambayo kwa sasa imetawaliwa na migogoro ya malipo halali, kwa kazi za wasanii na wizi wa kazi za wasanii. Pamoja na ukweli wa kauli ya Mwenyekiti wa Kampuni ya Fleva Unit Tanzania (TFU), ambayo inaundwa na wasanii 104 nchini ya wao wenyewe kuamua kuingia kwenye vita vya kupambana na wezi wa kazi zao, kutokana na udhaifu uliopo unaowanyima kipato, napenda kuhadharisha juu ya mipango isiyozingatia kasoro zilizopo sasa. Nawaomba wasanii hao kuangalia kasoro za sheria ya hakimiliki iliyopo sasa, inavyowagusa wao wenyewe dhidi ya Taifa na kimataifa na kisha kuziba mwanya unaowezesha maharamia kutwaa kazi zao, kuzidurufu na kuwauzia watu wengine. Hapana shaka kwa kuelewa kasoro hizo, pia wataisaidia Serikali kufanya marekebisho si katika sheria, bali na taasisi zilizoundwa kwa lengo la kuwasaidia wasanii kusonga mbele kikazi na kimapato. Ni vyema wakatambua kasoro, kwa vile sababu zilizofanya wakashindwa kuunda vyama zinaweza pia kujitokeza baada ya muda ndani ya kampuni kwa namna nyingine na kuzidi kudhoofisha kwa sababu mtaji wao kwa sasa ni vipaji vyao. Kuna mambo mengi yanayotakiwa kuwa sawa ili kuingia vyema katika vita ya kumwezesha msanii kufanya shughuli zake kihalali na kujipatia kipato halali huku maharamia wakizidiwa maarifa kwa sheria, ukali na utekelezaji wake. Hapana shaka kampuni inaweza kuwa na nafasi kubwa si tu ya kujiuliza, bali kuwa na mipango mikakati inayokidhi ulinzi wa hakimiliki na kuwa na chata ya kutumia inayoweza kufuatiliwa kwa karibu zaidi na hivyo kuwanyima maharamia nafasi ya kuiba kazi hizo. Msama hana budi kupongezwa kwa hatua ya kampuni yake kupambana na maharamia hao, na pia nasisitiza kuwaomba wasanii wawe mstari wa mbele kumunga mkono ili kufanikisha kilichokusudiwa.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...